TANZANIA NA MAFANIKIO YA KUSADIKIKA





              Watanzania nchini kote tumeungana kushangilia na kufurahia mafanikio ya timu yetu ya taifa. Nikisema wote namaanisha wadau wa soka hata wale wasiokua na mapenzi ya soka. Ni heshima kubwa timu ya taifa imeleta ndani ya nchi yetu baada ya kufuzu kwenye mashindano ya  kombe la dunia. Ni tukio la kihistoria ndani ya nchi yetu,na hakuna mtanzania  yeyote atakayeusahau mwaka huu 2022. Kila kona ninayopita ni nderemo na vifijo,mabosi ofisini,wachuuzi mtaani,wakina mama sokoni,wabunge bungeni  wote wamejisitiri kwa nguo zenye rangi moja zinazofanana.
Kila kona jezi za timu ya taifa zimevaliwa, Jezi ya timu ya taifa imekua sare ya watanzania wote. Hakika kila jambo lina wakati wake, kuna wakati wa kulia na kupata maumivu ya soka umeshapita, sasa  ni wakati wa kufurahia matunda ya soka.

             Napenda kuchukua fursa hii kumpongeza rais wa TFF wa sasa pamoja na uongozi wote wa Soka la Tanzania. Nitakua mchoyo wa fadhila kwa kutokutambua mchango wa hali na mali aliyeutoa mheshimiwa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Rais wetu wa awamu ya 6 kwa muda huu mfupi tangu ameingia  madarakani amekua bega kwa bega na Tff pamoja na wadau wote wa soka  kuhakikisha Tanzania tunahitimisha kiu ya safari ya kwenda Qatar tuliyokua tunaingoja kwa muda mrefu. Napenda kuwashukuru wana habari wote nchini kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuhamasisha watanzania kuishangilia timu yao ya taifa. Pia napenda kushukuru makampuni yote Tanzania kwa mchango wao mkubwa wa fedha waliotoa kuisaidia timu yetu ya taifa. Bila kusahau Kampuni kubwa Inayojishughulisha na Maswala ya Soka Tanzania WAPENDA SOKA CO.LTD

             Dhumuni la makala hii ni kutoa pongezi za dhati kwa aliyekua rais wa TFF bwana Jamal Malinzi sambamba na uongozi wote wa TFF uliokua chini ya bwana Malinzi sambamba na uongozi wote wa serikali za awamu ya 4 na ya 5 ambayo ilikaa madarakani kwa muda wa  mitano tu lakini ilifanya mambo makubwa na kukumbukwa na wapenda soka wote nchini na waTanzania kwa ujumla

              Bila shaka ndugu Jamal Malinzi hatosahaulika ndani ya vichwa vya watanzania na wapenda soka kwa ujumla kwa maono yake sahihi yaliyoleta mafanikio haya ndani ya nchi yetu. Baada ya kombe la Dunia mwaka 2014 ndugu Jamal Malinzi alijifunza mengi ndani ya kombe hilo na kuanza mara moja  kufanyia kazi mambo hayo. Jambo kubwa alilolifanya bwana Malinzi ni kujizatiti kwenye soka la vijana hasa vijana walioko mashuleni. Nakumbuka mnamo mwaka 2015 bwana Jamal Malinzi aliunda kikosi cha makocha gwiji nchini kumsaidia aliyekua kocha wa timu ya taifa ya vijana kusaka vipaji katika mashindano ya umitashumta na umiseta yaliyofanyika mjini kibaha mkoa wa pwani.Baada ya mashindano hayo walipatikana wachezaji wasiopungua thelathini ambao walitengeneza timu ya taifa ya vijana ambao walifahamika kwa jina maarufu la future generation(kizazi kijacho). Vijana hao waliochaguliwa walikua na wastani wa umri  wa miaka 17.

             Kwa kua bwana Jamal Malinzi aliamua kuweka nguvu zake zote kwenye timu hii,aliamua kutengeneza akademi ya soka kwa ajili ya timu hiyo ya vijana iliyochaguliwa. Vijana hao walianza kukaa pamoja mnamo mwaka 2015,pamoja na mafunzo ya soka  vijana hao walipata kuendelea na masomo yao ambao wachache walikua wakimaliza elimu ya msingi na wengine kuendelea na masomo yao ya sekondari kama kawaida.

             Mnamo mwaka 2016 ndugu Jamal Malinzi aliamua kuhamisha kambi ya timu ya taifa ya vijana na kuipeleka nchini Brazil,Vijana hao walikaa nchini brazil kwa muda wa mwaka mmoja ambapo walipata nafasi ya kujifunza zaidi mbinu mbali mbali  za soka katika nchi hiyo ya kisoka ya brazil. Mwaka 2017 timu hiyo ilirejea nchini na kuanza kushiriki michuano mbali mbali ikwamo kutafuta nafasi ya kombe la dunia la timu za vijana chini ya umri wa miaka  miaka 20,Vijana hao walikaribia kufuzu mashindano hayo ya Dunia lakini bahati haikuawa yao baada ya kutolewa na Ghana katika hatua ya mwisho. Lakini Mungu si athuman timu hiyo ilipata nafasi ya kushiriki mashindano ya mataifa ya afrika ya timu chini ya umri wa miaka 20 yaliyofanyika nchini Misri. Timu hiyo ilitolewa na wenyeji misri katika hatua ya nusu fainali, lakini ikafanikiwa kulipiza kisasi kwa timu ya taifa ya Ghana baada ya kuifunga timu hiyo na kukamata nafasi ya tatu katika mashindano hayo.

              Macho na akili za watanzania zikahamia katika timu hiyo ya vijana al maarufu future generation. Makampuni mengi yakajitokeza kuidhamini timu hiyo ya taifa ya vijana. Watu wengi wakawa na imani kuwa timu hiyo ndio mkombozi wa soka la Tanzania. Mnamo mwaka huo huo 2017 uliitishwa uchaguzi mkuu wa Tff uliomrudisha tena bwana Jamal Malinzi kuendelea kuiongoza TFF, Jamal Malinzi alipata ushindi wa kishindo kwasababu ya kutekeleza sera zake zilizomuweka madarakani mwaka 2013 hasa sera ya kukuza soka la vijana.



             Utaratibu wa kusaka vipaji kupitia mashindano ya umiseta na umitashumta uliendelea kama kawaida. Mnamo mwaka 2018 timu ya taifa ya vijana(future generation) ilipelekwa nchini  ufaransa chini ya udhamini wa makampuni mbalimbali ambapo timu hiyo ilikaa kwa muda wa miezi tisa kabla ya kurejea na kushiriki mashindano ya CECAFA yaliyofanyika nchini Kenya na kufanikiwa kufika hatua ya fainali kabla ya mwaka unaofuta kushinda kombe hilo.

         Timu hiyo iling’aa katika mashindano mbali mbali barani afrika, lakini kubwa zaidi ni pale timu hiyo ilipofanikiwa kufuzu mashindano ya Olympic 2020 mjini Tokyo na kufanikiwa kunyakua medali ya dhahabu. Mwaka huo huo 2020 timu hiyo iliingia katika mechi za awali za kufutafuta nafasi ya kucheza kombe la dunia,Tanzania chini ya bwana Jamal Malinzi ilifuzu kuingia hatua ya makundi.
Siku ambayo haitasahaulika ni mwaka 2021 ambayo Tanzania ilikua ikitupa karata yake ya mwisho dhidi ya timu ya taifa ya Nigeria, nakumbuka siku hiyo hakukuwa na kiingilio kuingia ndani ya uwanja,uwanja wote ulifurika mashabiki na wapenzi wa soka kuishangilia timu ya taifa(Future generation), nakumbuka ndio kwanza vijana hao walikua na wastani wa umri wa miaka 23. Nigeria walikokua wanaongoza kundi hilo wakiwa na point 13 moja zaidi ya Tanzania waliokua na point 12,Nigeria wakihitaji sare kuweza kufuzu kombe la Dunia nchini Qatar huku Tanzania wakihitaji ushindi wa aina yeyote.

              Sikumbuki ilikua dakika ya ngapi ila nakumbuka ilikua mwishoni mwa kipindi cha pili beki mahiri na nahodha wa timu hiyo aliruka kichwa kuunganisha kona iliyopigwa na kuiwezesha timu ya Tanzania kwa mara ya kwanza kufuzu kwenye mashindano ya kombe la Dunia. Nderemo na vifijo vilienea kila kona ya Tanzania.Siku hiyo ilikua sikuu kubwa kuliko zote kuwai kutokea nchini mwetu.

            Bwana Malinzi alimaliza muda wake ndani ya mwaka huo huo 2021 na kuitisha uchaguzi mkuu wa TFF uliomuweka madarakani rais wa sasa wa TFF. Lakini mafanikio haya yote ni maono ya bwana Jamal Malinzi katika kuwekeza katika soka la vijana. Nakumbuka miaka ya 2013 na 2014 nilikua naandika sana makala kuhusu soka la vijana,sijui kama bwana Malinzi kama alisoma au hakusoma makala hizo,Lakini ombi langu kubwa kwa yeyote atakayesoma makala hii kama yupo karibu na bwana Jamal Malinzi ampelekee makala  hii asome pongezi zangu za dhati kwake.



             Hakika 61 ina maana kubwa kwa watanzania,Nchi yetu ilipata uhuru mwaka 1961 na bwana Jamal Malinzi akiwa na miaka 61 aliiwezesha Tanzania kufuzu kombe la dunia kwa mara ya kwanza (mnamo mwaka 2021 ambapo tulicheza mechi ya mwisho ya kufuzu),Na baadae mwaka huu 2022 tutasherekea miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika. Kama ilivyokua kwa hayati baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ndugu pia jamal malinzi ni baba wa soka la Tanzania.

                                                                              Na

                                                        Allen Kaijage a.k.a middle ya juu

                                                                kaijagejr@gmail.com

                                                                       0655106767          
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

2 comments:

  1. Kweli hii ni ndoto, anything can happen as long as nia ikiwemo

    ReplyDelete
  2. Kwa akili ya kawaida unaweza kudhani kuwa mwandishi ameandika hili kwa kujifurahisha kwani ameishi miaka mingi ijayo katika wakati uliopo. Ni kama unaangalia filamu ya matukio ya mwaka 2021 wakati wewe upo kwenye mwaka halisi 2014.

    Lakin kwa jicho langu la tatu mwandishi alikuwa na lengo maalumu la kutukumbusha jamii kuwa ili tuweze kufanya vizuri katika medani ya soka la kimataifa tunatakiwa tuwekeze kwa vijana. Ni vijana tu ndiyo watakao tutoa kwenye hichi kilio cha kushindwa na kutupeleka kwenye kilele cha mafanikio.

    Nigeria walipotea kwenye anga za soccer, ila wakajiuliza na kuona walipokosea wakawekeza kwa vijana sasa wamerudi kwenye soka, Misri walitesa sana kwa sababu ya kuwekeza kwa vijana. Ghana walitikisa Africa na dunia nzima kwani waliwekeza kwa vijana

    Brazili inajivunia kuwa na vijana wengi katika timu ya taifa, ujerumani vivyo hivyo, ubeligiji nd usiseme. Muda wa kuwatumia watu wenye miaka 28 - 29 (ya mpira umekwisha) sasa tuamke na kuwekezeka kwa vijana.

    Asante mwandishi kwa kumkumbusha JAMALI MALINZI na kamati yake ya utendaji kuwa mafanikio ya nchi yetu yanategemea nguvu yetu ya kuwekeza kwa vijana. Kubadili jezi na jina la taifa ni nadharia tu tunahitaji mafanikio zaid ya kubadili jezi na jina la timu.

    Muhsin hero

    ReplyDelete

Powered by Blogger.