LICHA YA KUPOTEZA, YANGA YATINGA HATUA YA MAKUNDI AFRIKA

Yanga wamefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kuvuka hatua ya mtoano na kuingia katika hatua ya makundi.

Yanga wamefika hatua hiyo baada ya kuitoa Welayta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa jioni ya leo huko Ethiopia.

Yanga wamefaidika kutokana na ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mchezo wa kwanza waliocheza nyumbani jijini Dar es salaam

Haikua rahisi kwa Yanga kufuzu katika mchezo wa leo kwani Welayta waliandika bao mapema mnamo dakika ya pili tu ya mchezo huo kupitia kwa Djako Arafay baada ya makosa ya walinzi wa Yanga kushindwa kuondoa hatari langoni kwao.

Bao hilo lilipelekea presha kubwa langoni kwa Yanga kwa takribani dakika 20 za kwanza kabla ya Yanga kutulia na kuanza kujibu mashambulizi huku wakijilinda kwa nidhamu.

Hadi mchezo huo unamalizika, Welayta walibaki na ushindi huo wa bao 1-0 ambao hata hivyo haukutosha kuitoa Yanga mashindanoni.

Yanga sasa watasubiri droo ya makundi ya michuano hiyo ili kujua ni timu zipi watapambana nazo katika safari mpya ya michuano ya kombe la shirikisho.

No comments

Powered by Blogger.