SIMBA YAIADHIBU STAND UNITED NA KUREJEA KILELENI MWA MSIMAMO VPL


Wekundu wa Msimbazi Simba wameweza kuibuka na ushindi wa bao 2-1 katika mchezo wao wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Wenyeji Stand United.

Mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Kambarage mjini Shinyanga ulikua mgumu kwa Simba na haikua kazi rahisi kuibuka na ushindi huo.

Shiza Ramadhani Kichuya alitangulia kuipa Simba bao la kwanza dakika ya 18 ya mchezo baada ya kupiga shuti kali akipokea pasi ya mpira wa kichwa wa John Bocco bao ambalo lilidumu mpaka mapumziko.

Kipindi cha pili Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Simba Joseph Omog ya kumtoa Emmanuel Okwi na kumwingiza Laudit Mavugo yaliwapa bao la pili Simba dakika ya kwanza tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili likifungwa na Mavugo akitumia vyema pasi ya Mdhamiru Yasin huku mfungaji akiwapita katikati mabeki wawili wa Stand United na kupiga shuti kali lililotinga nyavuni.

Makosa ya beki Ally Shomari yaliwapa Stand United bao la kufutia machozi baada ya refa kuizawadia Stand United penati na Aishi Manula akajaribu kuudaka mpira lakini mpigaji
Mtasha Mnashe akamalizia baada ya mabeki kuzubaa.

Kwa Matokeo haya Simba sasa wanarudi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 11 sawa na Mtibwa na Azam lakini Simba ikiwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ligi hiyo itasimama kupisha mechi za kimataifa na itarejea tarehe 14 ambapo viwanja mbalimbali vitakua katika wakati mgumu.

No comments

Powered by Blogger.