"MCHEZAJI ASIYEJULIKANA" AINYIMA MAN UNITED USHINDI UGENINI
Eric Maxim Choupo-Moting ni jina lisilojulikana sana katika ulimwengu wa soka tofauti na majina kama Romelu Lukaku,Alvaro Morata, Alexandre Lacazette ambao walitikisa vichwa vya habari katika uhamisho wao mwezi uliopita.
Choupo-Moting mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon anayeichezea Stoke City hatasahaulika midomoni mwa mashabiki wa Manchester United baada ya kufunga magoli yote mawili ya Stoke City katika sare ya bao 2-2 na Vinara wa Ligi kuu ya England Manchester United.
Mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Britania ulikua mchezo wa mwisho leo katika mzunguko wa nne wa ligi kuu ya England.
Man United ikisafiri mpaka jijini Stoke ilitaka kuendeleza wimbi la ushindi baada ya kufanya vyema kwenye michezo yake mitatu iliyopita lakini wakakutana na Stoke City iliyokamilika chini ya Mchezaji wa zamani wa Man United Mark Hughes na kujikuta ikiambulia sare ya bao hizo 2-2.
Stoke City walitangulia kupata bao dakika ya 43 likifungwa na Choupo-Moting baada ya kazi nzuri ya Birami Diof lakini dakika mbili baadae Man United wakasawazisha kwa goli la Marcus Rashford ambaye mpira ulimgonga baada ya kichwa kilichopigwa na Paul Pogba.
United waliongeza bao la pili dakika ya 58 likifungwa na Romelu Lukaku lakini Choupo-Moting akairejesha Stoke City mchezoni akiunganisha mpira wa kona ya Xherdani Shaqiri na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare hiyo ya bao 2-2.
Matokeo hayo yanawafanya Man United kuendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 10 sawa na Manchester City wenye pointi 10 pia huku Stoke City wao wakifikisha pointi 5 katika nafasi ya 10.

No comments