BAADA YA KUUMIA JUZI HIZI NDIZO MECHI ATAKAZOKOSEKANA PAUL POGBA

Paul Pogba
Moja kati ya wachezaji waliocheza mechi zote kwenye kikosi cha Manchester United msimu huu ni Paul Pogba ambaye dakika ya 20 kwenye mchezo wa juzi dhidi ya FC Basel katika michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya aliumia misuli ya paja na kulazimika kutolewa nje.

Pogba ambaye juzi alikua ndiyo nahodha wa United ilimlazimu kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Maroane Fellaini na sasa imethibitika baada ya vipimo kwamba atakaa nje kwa muda wa wiki sita.


Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye miaka 24 atakosekana si tu kwa klabu yake ya Manchester United lakini pia kwa timu ya taifa ya Ufaransa kwenye michezo yake miwili ijayo.


Pogba atakosa michezo kadhaa wakati huu akiwa majeruhi ikiwa ni pamoja na mchezo wa Jumapili hii dhidi ya Everton lakini pia mechi dhidi ya Southampton na Crystal Palace katika ligi kuu ya England, atakosa pia mchezo wa wiki ijayo dhidi ya Burton katika kombe la Ligi hatua ya tatu na mechi ya Ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya CSKA Moscow Septemba 27.


Ukiacha mechi hizo za klabu lakini Pogba atakosa pia mechi za timu yake ya Taifa kwaajili ya kufuzu kwa fainali zijazo za kombe la Dunia dhidi ya Bulgaria na Belarus ambazo Ufaransa inahitaji ushindi kupata nafasi ya kufuzu.


Kama hali yake itaimarika kabla ya Oktoba 14 basi ataweza kuikabili Liverpool kwenye mechi ya ligi kuu ya England itakayopigwa tarehe hiyo 14 Oktoba jijini Liverpool.

No comments

Powered by Blogger.