EMMANUEL OKWI WA SIMBA NDIE MCHEZAJI BORA ZAIDI MWEZI AGOSTI
Mshambuliaji wa Simba ya Dar
es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Agosti wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Okwi alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda
wenzake wawili katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam jana (Jumatano) na
Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na
mapendekezo kutoka kwa makocha wa viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo
inachezwa. Wachezaji wote hao timu zao zilishinda.
Walioshindana na Okwi katika
hatua hiyo ya mwisho ni kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa ambaye alisaidia
timu yake kupata pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo dhidi ya
Stand United uliofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, ambapo alikuwa nyota wa
mchezo huo. Mwingine aliyeshindana na Okwi ni Boniface Maganga wa Mbao FC.
Maganga alitoa mchango mkubwa
katika ushindi wa ugenini wa bao 1-0, ambao timu yake iliupata dhidi ya Kagera
Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ikiwa ni pamoja na kufunga bao
hilo.
Ushindi wa Okwi unatokana na
kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 7-0,
huku Okwi akifunga mabao manne.
Pia Okwi amekuwa mchezaji wa
kwanza msimu huu kufunga hattrick (mabao matatu katika mchezo mmoja)
katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 16, ambapo hat trick
hiyo alifunga ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Mwezi huo ulikuwa
na raundi moja tu iliyochezwa Agosti 26 na 27 mwaka huu ambapo kila timu
ilicheza mechi moja.
Kutokana na kutwaa tuzo hiyo,
Okwi ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) atazawadiwa
kitita cha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc.

No comments