SOL CAMPBELL KUCHEKI MECHI YA NGAO YA HISANI TANZANIA
Wakati mang’amung’amu
hayo ya ujio wa Everton yakiwa bado vichwani mwa mashabiki wa soka, tayari kuna
taarifa ya ujio mwingine mkubwa nchini kwa udhamini wa SportPesa.
Ikiutumia vyema
ushirika wake na vilabu vya EPL, SportPesa sasa inamleta nguli na balozi wa
klabu ya Arsenal kutoka jijini London ambao ni mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya
Uingereza huku pia wakiwa ni mabingwa wa kihistoria wa kombe la FA ambao
wamelitwaa mara 13.
Mwaka 2001 alijiunga na miamba hiyo ya London akitokea Tottenham Hotspurs, Moja ya Mafanikio anayojivunia ni kuisaidia Klabu yake ya Arsenal kuweza kucheza michezo 49 bila kupoteza hata mchezo mmoja, ulikuwa ni msimu wa 2003/04 na kutwaa ubingwa wa ligi kwa staili ya aina yake kabisa. Huyu si mwingine bali ni Sol Campbell
Alifanikiwa Kucheza michezo 200 akiwa na Arsenal na kufunga magoli 12, tulizoea kumuona kwenye runinga akisakata kabumbu safi na la kibabe haswaa, pia alipostaafu bado tulimuona akiuchambua mpira kwa ustadi wa hali ya juu.
Kupitia kampuni ya mchezo wa kubashiri ya SportPesa, wamefanikiwa kumleta Gwiji huyo Tanzania. Sol Campbell anatarajia kutua katika ardhi ya Tanzania na kufungua njia ya mahusiano mazuri ya kimichezo kati ya Tanzania na Klabu Ya Arsenal kupitia SportPesa ambao ni washirika rasmi wa Arsenal katika michezo ya kubashiri kwa bara la Afrika.
Arsenal na SportPesa waliingia mkataba wa miaka mitatu
na nusu ambao utaishuhudia klabu hiyo ya Arsenal ikileta maofisa wake wa benchi
la ufundi kwa ajili ya kuendesha kliniki za soka kwa makocha na wachezaji
barani Afrika na tayari wameshafanya hivyo mara kadhaa nchini Kenya.
Atakapokuwa nchini, Sol
Campbell atapata nafasi ya kutembelea klabu ya michezo ya walemavu ya Muungano
na kubadilishana nao mawazo na kisha siku ya tarehe sita pia atatembelea shule
ya soka ya Magnet katika viwanja vya Gymkhana ambapo atapata nafasi ya kukutana
na wachezaji chipukizi, kucheza nao na pia kuwapa hamasa katika safari yao ya
soka.
Kubwa zaidi ni pale
ambapo Campbell ataongoza jopo la wapenzi wa klabu ya Arsenal nchini kutazama
mechi ya Ngao ya Hisani siku ya Jumapili ya Agosti 6 kati ya klabu ya Arsenal
ambao ni mabingwa wa FA dhidi ya Chelsea ambao ni mabingwa wa EPL.
Hakika itakuwa ni fursa
adhimu kwa wapenzi wa mpira nchini hususani wale wa Arsenal kukutana na nyota
wao huyo wa zamani, kuongea na kupiga nae picha ikiwa ni ndoto ya kila shabiki
wa soka duniani kukutana na nyota anayemkubali.
Ikumbukwe kuwa Arsenal
ni klabu inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini Tanzania hali kadhalika
barani Afrika. Hivyo naona jinsi ambavyo ujio huu wa Sol Campbell unavyotimiza
ndoto za kundi kubwa la mashabiki wa soka nchini. Upo tayari?
No comments