KAMA KIJANA HIKI NDICHO UNACHOPASWA KUJIFUNZA KUHUSU WAYNE ROONEY

Rooney aliondoka nyumbani akiwa mdogo wa kiumri ila akiwa mkubwa kifikra. Akili zake zilikuwa zimekomaa, hakusita kuondoka nyumbani kwao na kwenda kutafuta maisha.
Kwa umri mdogo wa miaka 18 ngozi ya mwili wake ilitamani kupaka mafuta yenye kunukia na kunawirisha.Damu yake ilikuwa changa lakini iliyokuwa ya moto, umoto ambao ulikuwa unafanya tumbo lake liwe na njaa ya mafanikio kila wakati.

Kwa umri ule hakuona faida ya kukaa nyumbani alipokuwa anapapenda kwa sababu moja tu.
Kwa wakati ule hakuona chungu cha maji kilichokuwa kinauwezo wa kubeba maji ya kutosha kukata kiu yake. Maghala ya chakula yaliyokuwepo nyumbani kwao hayakuwa na uwezo wa kuinyamazisha njaa aliyokuwa nayo.

Miguu yake haikuwa mizito pale moyo wake ulipomwambia dunia yake imara kamwe haitojengwa kwa kukaa nyumbani. Hakusita kupiga hatua za kuondoka pale na kwenda kuishi nyumbani kwa adui wa rafiki yake. Lilikuwa jambo gumu kwake kwenda kuishi sehemu ambayo anajua imejaa maadui wa rafiki yake mpendwa.

Kuishi kwa maadui wa rafiki yake mpendwa ilikuwa na maana kuwa Rooney alitakiwa kuanza kumchukia rafiki yake tena . Hii yote tu ni kwa sababu alikuwa katika utafutaji.
Aliziba masikio yake, akaziba mdomo wake pia akaamua kutembea kama kiziwi asiyesikia lakini anaona.
Alibakiza macho kwa ajili ya kuona njia ya mafanikio na yeye akabakiza kuikimbilia njia hiyo kuelekea kwenye kilima cha nafanikio.

Hakujali ni kiasi gani rafiki yake ataumia kutokana na yeye kwenda kuishi kwa adui wa rafiki yake, hakujali ni kwa kiasi gani rafiki yake atamsema vibaya na kumtukana ila yeye alichoangalia ni kipi anakipata katika maisha yake kwa ajili ya furaha yake.

Jambo muhimu katika maisha yake lilikuwa kujipa furaha mwenyewe.
Macho yake yalimwongoza vyema kutimiza kazi ya ubongo ulivyokuwa unafikiria.
Macho yake yalimuongoza kuliona goli akawa anafunga sana mpaka akawa mfungaji bora wa muda wote wa adui wa rafiki yake, akawa mfungaji bora wa taifa lake.

Ugenini alipokimbilia alifanikiwa kupata kila kitu , kombe la EPL, UEFA, FA, EUROPA, EFL na kikombe cha mabingwa wa dunia ngazi ya klabu. Hivi vyote alivipata akiwa mbali na nyumbani.

Inawezekana leo hii nisingeandika mafanikio ya Rooney kama angebaki nyumbani kwao.
Aliamua kwenda kujenga ufalme wake sehemu nyingine tofauti na nyumbani kwao akiamini nyumbani kwao baba yake ndiye mfalme .

Hakuwa tayari kupata ufalme wa kurithishwa.Hakuwa tayari kusubiri ndevu zake zimjae ndiyo aondoke nyumbani, hakuwa muoga wa kukimbia nyumbani kama vijana wengi tulivyo.

Tumeumbiwa moyo wa kutodhubutu kufanya maamuzi ambayo yatakuwa na manufaa kwenye maisha yetu. Wengi wetu tumekuwa tukizeekea nyumbani kwa wazee wetu na kuogopa kuondoka kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Wengi wetu tunaziogopa changamoto, na kusahau kuwa maisha bila changamoto ni sawa na mboga bila chumvi, hakuna ladha ya maisha kama changamoto ikikosekana.
Tumekuwa watu wa kupenda kukaa sehemu ambayo ni comfort zone ( sehemu ya kujifariji). Sehemu ambayo itakufanya usiumie kwa kukosa kuingiza hata shilingi elfu moja kwa kujifariji kuwa ugali nyumbani upo.
Hatuna maandalizi sahihi ya mawio na machweo, na kibaya zaidi hatujui kusoma nyakati na kushindwa kufanya kitu sahihi wakati wa mawio na machweo.

Rooney aliona wakati wake sahihi ni upi, akaamua kukimbia nyumbani akajenga ufalme wake nje ya kwao. Leo hii anarudi nyumbani akiwa mfalme.
Awali kulikuwa na ujio wa Everton ila baada ya Rooney kurudi Everton, habari ikabadilika, ikawa tena siyo ujio wa Everton, ikawa ujio wa Rooney na Everton.
Kuna uwezekano mkubwa aliyewasukuma watu waende uwanja wa taifa ni Rooney kwa asilimia kubwa na Everton kwa asilimia ndogo.
Heshima huwezi ijenga kwa kukaa nyumbani, unatakiwa utoke upigane uonje ugumu wa maisha ndipo hapo utafanikiwa kwa kiasi kikubwa

Imeandaliwa na Martin Kiyumbi

No comments

Powered by Blogger.