NYOTA 10 WALIONG'AA ZAIDI KATIKA MECHI ZA NUSU FAINALI YA KLABU BINGWA ULAYA


10: KAMIL GLIK.

Watu wengi wanaongelea safu imara ya ushambuliaji ya Monaco kitu ambacho ni kawaida katika kizazi hiki tulichopo kwa sababu imekuwa ngumu kurudi enzi za kina Fabio Cannavaro ndiyo maana imekuwa rahisi kwetu sisi kumsifia zaidi Antoinne Griezmann na kumsahau kabisa Diego Godin. Na ndicho kitu kinachotokea kwa Monaco, Kamil Glik hatumuoni ila huyu ni moja ya mabeki bora na ni kiongozi mzuri katika safu ya ulinzi ya Monaco.

9: MARIO MANDZUKIC.

Massemiliano Allegri ameamua kututengenezea kiumbe kipya, kiumbe ambacho kinafanya kazi mbili kwa wakati mmoja tena katika kiwango kizuri  anakaba na kuua kwa wakati mmoja, katika mfumo wa 4-2-3-1 amekuwa na ushirikiano mzuri na Alex Sandro. Ilikuwa ni vigumu kuamini kama Mario Mandzukic atacheza pembeni tofauti na nafasi yake aliyoizoea ya mshambuliaji wa kati lakini amekuwa akitimiza vizuri majukumu yake ya kujilinda na kushambulia upande wa kushoto na kitu kikubwa kinachomuongezea nguvu ni uwezo wake mkubwa wa kucheza mipira ya juu.

8: RADAMEL FALCAO

Tulikuwa tumeshaandaa mengi kwa Falcao, kwanza kifo chake tulikitabiri kutokea maana mwisho wake ulikuwa unaonekana baada ya yeye kushindwa kufanya vizuri akiwa Chelsea na Manchester United na kibaya zaidi jeneza na sanda yake tulikuwa tumeshanunua lakini mchungaji Leornado Jardim alifanya maombi ambayo yamemponesha aliyekuwa mgonjwa mahututi. Kuzaliwa upya kwa Falcao kumekuwa msaada mkubwa sana katika timu ya Monaco ni kiongozi mzuri kwa kina Kylian Mbappe.

7: Barzagli, Bonucci, Chiellin (BBC).

Nimewaweka hawa kwa pamoja kwa sababu ni mnyonyoro nati moja kati ya hizo ikidondoka mnyonyoro unakatika. Jana ndiyo walikuwa mhimili dhidi ya safu imara ya ushambuliaji ya Monaco. Wamefanikiwa kutengeneza ukuta imara uliojengwa kwa Chokaa.

6: BUFFON.

Kukamilisha dakika 600 bila nyavu zake kutikiswa haiwezi kuwa sababu kubwa ya yeye kuwa kati ya wachezaji nyota kwangu kwa michezo ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa, uimara wake mkubwa langoni ndiyo sababu kubwa ya kumpa heshima kubwa kwenye orodha yangu, ukifikiria kuwapita kina Barzagli, Bonucci na Chiellin kunaweza kukukatisha tamaa lakini mtihani huja baada ya kufikiria kuwa nikiwapita hawa golini kuna kina Barzagli, Bonucci na Chiellini wengine wanaotumia miguu na mikono kwa pamoja, kwa kifupi hawa wazee waliumbwa na mifupa ya kina Daudi ndicho kinachowafanya wawe imara katika uwanja wa vita.

5:  KYLAN MBAPPE.

Unatamani nimwite Thierry Henry mpya ? Nafsi yangu inasita sana kumwita hivi, ana vitu vingi sana vya kujifunza ingawa maendeleo yake ni mazuri na yanatia tumaini , katika umri wa miaka 18 pekee ameuvaa U Joshua ni jasiri kwa kila hatua aliyopo vitani, kinachotakiwa apate Musa wakumuongoza vizuri na kumuonesha njia ya kwenda Kanani.

4:  PJANIC na PAOLO DYABALA.

Hawa ndiyo wakandarasi wa nyumba ya vibibi vizee wa Turin, ubora na uzuri wa nyumba ya bibi kizee kizee cha Turin imejengwa na hawa mafundi, kadri siku zinavyozidi kwenda wanajenga sinagogi zuri lenye nusu ya thamani ya sinagogi lililojengwa na Mfalme Selemani, busara na ubunifu wao ndiyo unaendesha maisha mazuri ya Juventus. Ubunifu wa kuunganisha safu ya kiungo cha kuzuia na kiungo cha kushambulia anao Pjanic, na ubunifu wa kuunganisha kiungo cha kushambulia na safu ya ushambuliaji anao Dyabala.
Na kitu ambacho kinambeba zaidi Dyabala ni kucheza katika eneo huru linalompa nafasi yeye kuwa mbunifu zaidi.

3: MARCELO.

Ni miaka imepita tangu aondoke Roberto Carlos, Mungu ameamua kutuletea mfano wa Roberto Carlos na kitu kizuri zaidi ametoka kwenye nchi ile ile ya Brazil na klabu ile ile ya Real Madrid ambapo Roberto Carlos alikuwa akiishi. Waweza ukaona wachezaji wawili ndani ya Marcelo hasa hasa anavyobadirika kwa wakati. Mfano timu inapojilinda kuna taswira ya beki kisiki hujitokeza, na timu inaposhambulia kuna taswira ya kiungo wa pembeni na hiki ndicho kitu ambacho kilimfanya Isco acheze zaidi katika eneo huru kwa sababu eneo la kushoto ambalo huwa anacheza Bale ambalo ndiyo eneo alilotakiwa kuwepo Isco lilikuwa linamilikiwa na Marcelo hivo  kumpa uhuru Isco kucheza katika eneo huru.

2: RONALDO

Kuna vitu vingi vinapotea kwa Ronaldo  kasi yake imepungua sana huwezi ƙ|inganisha na kasi yake kipindi yuko kijana na siyo mchezaji wa kubadirika mara kwa mara katika mchezo ila kuna ambacho hakijapungua kwa Ronaldo nacho ni uwezo mkubwa wa kufunga. Haonekani kama muda wake wa kupungua kufunga unaelekea kuisha na magoli yake matatu ndiyo yaliyosababisa Real Madrid kuwa na uhakika wa 60% kwenda Cardiff.


1: DANI ALVES.

Mwisho wake ulionekana umeshafika baada ya yeye kutoka Barcelona kwenda Juventus lakini amedhihirisha tofauti na mafikirio yetu mpaka sasa akitoa pasi za mwisho nne za magoli zikiwemo za jana ambazo zilikuwa muhimu kuelekea Cardiff.

Wengi wetu tulishtuka kutomuona Juan Cuadrado, lakini uwepo wa Dani Alves uliondoa mshituko wetu kwani alifanikiwa kufanya mlinganyo wakati wa kushambulia ambapo alishirikiana vizuri na Gonzalo hata wakati wa kuzuia alishirikiana vizuri na Andrea Barzagli.


Martin Kiyumbi.

Tufuatane kwenye mitandao ya kijamii.

Facebook na Instagram ni Martin Kiyumbi.

No comments

Powered by Blogger.