NILICHOKIONA KWENYE MECHI YA SIMBA NA YANGA.
Kuna kitu kimoja ambacho eneo la kiungo cha Simba walikuwa wanakikosa zamani ila kwa sasa kimepatikana Kupitia Kotei.
Kipindi ambacho Mkunde anacheza eneo la kiungo cha kuzuia alikuwa anashindwa kuleta ugumu eneo la kiungo cha Simba.
Lakini kwa mechi hii kuna mfupa umejengeka eneo la kiungo cha Simba kwa sababu ya Kotei.
Kwenye mechi hii, Kotei na Mkude kwa asilimia kubwa hasa hasa kipindi cha kwanza walipewa jukumu la kufanya ugumu zaidi eneo la katikati mwa uwanja. Jukumu la kujilinda kwao lilikuwa kubwa zaidi kuliko jukumu la kushambulia.
Na hii ndiyo ilikuwa approach kubwa ya timu zote mbili. Timu zote kipindi cha kwanza ziliingia zikiwa na tahadhari zaidi ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza.
Hatukuona nafasi nyingi zikitengenezwa pande zote mbili kwa kipindi cha kwanza.
Kitu pekee ambacho Simba walikitegemea ni wao kutaka kupitia pembeni ndiyo maana wakamweka Mzamiru na Kichuya pembeni huku Mohamed Ibrahim akicheza kama false 10.
Hii ilikuwa na maana kubwa sana kwa Simba kwa sababu Mohamed Ibrahim kwa kiasi kikubwa anaweza kutoa huduma zifuatazo .
Kwanza huduma ya kusambaza mipira pembeni mwa uwanja na kwa mshambuliaji wa kati.
Pili Mohamed Ibrahim anauwezo wa kufunga hasa hasa anapocheza eneo ambalo yuko nyuma ya mshambuliaji.
Sasa kitu ambacho kilikuja kuharibu mpango huu ni hiki hapa.
Yanga wakimweka Said Juma pamoja na Kamusoko na wote wakapewa jukumu moja na kuzuia zaidi.
Kwa kipindi cha Kwanza Kamusoko hakujihusisha kwa asilimia kubwa kwenye jukumu la kushambulia ingawa anauwezo mkubwa kwenye jukumu hilo.
Muda mwingi mwa kipindi cha Kwanza Walikaa nyuma, na hii ikamnyima Uhuru mkubwa Mohamed Ibrahim wa kutimiza majukumu yake.
Ndiyo maana kwa kiasi kikubwa Kichuya na Mzamiru ambao Walikuwa wanatokea pembeni wakipata mipira michache sana.
Kuna kitu kimoja kwa Mzamiru, kwenye mchezo huu kitu pekee kilichomkaba ni nafasi ambayo alikuwa jana.
Mzamiru siku zote huwa anaonekana bora zaidi pindi anapocheza kama Box to box Midfielder. Nafasi hii inampa uhuru sana wa kutokuwepo eneo moja. Mzamiru ni aina ya wachezaji ambao hucheza kwa furaha na kujiachia kama wakicheza eneo ambalo watakuwa uhuru kutembea eneo lolote la uwanja.
Yanga kwa kiasi kikubwa waliingia kwa ajili ya kujilinda na kucheza direct football ( yani mpira wa moja kwa moja).
Na hii inatokana na matokeo ya mechi iliyopita ambapo walicheza sana open football ( mchezo wa wazi).
Hawakuingia na mpango huo tena, walichokifanya ni kucheza mipira mirefu.
Kitu pekee ambacho kilisababisha mbinu hii kutofanikiwa ni kwa sababu, ili Yanga iweze kuwa hai kwenye eneo la kushambulia lazima eneo la pembeni liwe hai.
Bukungu na Mohamed Hussein kwa kiasi kikubwa walifanikiwa kuwafanya Kaseke na Msuva wasipate uhuru wa kucheza.
Mfano, kwa kiasi kikubwa Bukungu hakuwa akipanda zaidi mbele kushambulia , hii ilimpa uhuru mdogo Msuva kulazimisha mashambulizi.
Kitu kingine, Timu ya Yanga inapocheza mipira ya juu na mipira mirefu ya moja kwa moja tegemea huduma ya mtu kama Niyonzima kutokuwa nzuri ukilinganisha na kama Yanga ikiweka mpira chini.
Unapokosa huduma ya Niyonzima moja kwa moja unakuwa umekosa ubunifu wa pasi za mwisho kwa mshambuliaji wa mwisho.
Ndiyo maana kwa kiasi kikubwa mipira ambayo alikuwa akiipata Tambwe ilikuwa inakuja katika eneo ambalo ni ngumu kwake kufanya maamuzi ( alikuwa akipata mipira isiyokuwa na madhara).
Kuna kitu ambacho mabeki wa Yanga wanatakiwa wawe makini nacho kwa kiasi kikubwa.
Nacho ni wao kujipanga wakati timu inashambuliwa kwa kushtukizwa.
Nakupa mfano, kuna shambulizi moja la kushtukiza ambalo lilitokea eneo la kulia mwa Yanga. Juma Abdul alikuwa amepanda kushambulia.
Yondani alikimbia kucover eneo lake, lakini Juma aliporudi alikimbia kwenda eneo alipo Yondani badala ya kwenda eneo aliloacha wazi Yondani.
Kuna kitu kikubwa sana kwa Said Juma anatakiwa kujifunza kutoka kwa Mkude.
Yeye ndiye anayetengeza ni njia ipi ya kupitishia mipira kwenye timu. Au ni aina gani ya mchezo muda huu timu inatakiwa icheze.
Ili uweze kufanya hivyo unatakiwa uwe na uwezo mkubwa wa kupiga pasi ili kusukuma timu yako. Lakini hiki Said Juma anakosa ingawa ni Mzuri sana kwa kukaba.
Martin Kiyumbi

No comments