WADAU WAOMBWA KUISAIDIA PAMBA FC IBAKI DARAJA LA KWANZA.

Naibu waziri wa Ardhi,Nyumba na maendleo ya makazi Angelina mabula amewaomba wadau wa soka wa mkoani Mwanza kujitokeza  kuisaidia timu ya soka ya Pamba fc inayoshiriki Ligi daraja la kwanza.

Akizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano maalumu,Mabula amesema Pamba fc ni moja kati ya timu kongwe sana hapa nchini na ina historia kubwa.

Mabula amewaomba wadau wajitokeze kwa wingi kuhakikisha wanaisaidia timu ya soka ya Pamba fc kwa msaada wa fedha na hata kimawazo.

Licha ya kuendelea kutoa misaada yake katika timu za Mbao fc na Toto Afrika ambazo zipo ligi kuu, Mabula alisema viongozi  na wadau wa soka wanatakiwa kuhakikisha timu ya Pamba fc inabaki Ligi daraja kwanza(FDL).

Katika msimamo wa Ligi daraja la kwanza kundi A, timu hiyo ipo mkiani baada ya kucheza michezo nane na kuambulia alama sita tu huku ikishinda mchezo mmoja dhidi ya Polisi Dar-es-salaam.

Pamba fc ilishindwa kufanya usajili na kukaa kambini kutokana na ukata wa pesa unaoikumba klabu hiyo.

Tangu ilipopoteza udhamini wa bodi ya Pamba(TCB) katika miaka ya tisini imekuwa ikiyumba katika kuendesha klabu hiyo ambayo imekuwa ikisota katika Ligi daraja la kwanza kwa kupanda na kushuka.

No comments

Powered by Blogger.