THE GUNNING MACHINE: KWA NINI LEO TUSIFUTE KABISA JINA LA EMMANUEL ADEBAYOR?
Na Richard Leonce
Imebidi nipate muda wa kurudi tena kwenye TGM masaa machache tu kabla ya kipute cha aina yake kupigwa katika uwanja wa Old Traford. Arsenal wakienda pale kutafuta ushindi wa kwanza wa ligi kuu tangu mwaka 2006. Yaani huu ni mwaka wa 10 kila wakienda wanaambulia kipigo ikiwemo kile cha 8-2 mwaka 2011 au sare.
Siyo mashabiki wengi wa Arsenal tunampenda Emmanuel Adebayor, hii inatokana na namna alivyoondoka katika kikosi cha Arsenal, maneno yake, ule ushangiliaji wake wa kuudhi baada ya kutufunga akiwa na Man City nk.
Lakini ni ngumu sana kumwondoa Adebayor katika mambo muhimu ya Arsenal kwa sababu yeye ndiye aliyetupa ushindi wa mwisho wa ligi kuu pale Old Traford September 2006. Walijaribu akina Carlos Vela, Samir Nasri, Cesc Fabregas, Gervinho, Chamackh na wengine lukuki lakini wameshindwa kuuvunja mfupa aliovunja Adebayor.
Leo tunakwenda tena pale katika mchezo muhimu. Ukiachana na maneno maneno ya ugomvi wa Arsene Wenger na Jose Maurinho, umuhimu wa mchezo wa leo unatokana na maana ya ushindi kwa timu zote.
Huu ni aina ya michezo ambayo tunasema ni ya 'pointi 6' kwa sababu zinakutana timu ambazo zote zinawania ubingwa. Unapomfunga mwenzako unakua umepata pointi 6 kwa maana ya zile tatu za ushindi lakini pia unakua umemnyima yeye pointi tatu za kukusogelea au kukuacha zaidi.
Arsenal wana faida kubwa sana katika mchezo wa leo kwa sababu wapo mbele kwa pointi 6 dhidi ya Man UTD na wana nafasi ya kufungua zaidi ombwe hilo kwa ushindi ambao utawaweka mbele zaidi kwa pointi 9.
Hizi ni nafasi ambazo hutokea mara nyingi kwenye ligi na makocha wajanja huzitumia. Bahati mbaya Arsenal wamekua hawazitumii mara kwa mara na ni moja kati ya sababu zinazowanyima ubingwa mara nyingi. Utakumbuka Arsenal walipoteza mchezo dhidi ya Liverpool, lakini hivi karibuni walipoteza nafasi ya aina hiyo mbele ya Tottenham wakikubali sare ya 1-1 katika mchezo ambao iwapo wangeshinda wangepanua pengo la pointi baina yao na Tottenham kuwa 6.
Nafasi nyingine ni leo. Katika uwanja mgumu siyo kwa Arsenala pekee bali timu nyingi. Siyo jambo rahisi kupata ushindi Old Traford. Hata timu ndogo zinaposhinda pale huwa hazishindi kirahisi. Ni kazi inayohitaji umakini, jasho na mara nyingine damu.
Mimi ukinipa sare katika mchezo wa leo nitachukua bila hata kujilaumu japo ushindi ni muhimu zaidi. Sare itamaanisha tumecheza na Man UTD na bado tupo mbele yao kwa point 6. Hapa nina maana ya kwamba ningependa zaidi kuona Arsene Wenger anahakikisha kwanza umadhubuti kwenye ukuta.
Tutakua bila Hector Bellerin leo na nafasi yake bila shaka itachukuliwa na Carl Jenkinson. Huwa napenda kitu kimoja kwake, kasi ya Jenkinson haiwiani na kimo chake, ni mrefu lakini ana kasi ya kumtosha kabisa.
Kuna watu wana wasiwasi na yeye kwenye mchezo wa leo, na hii inatokana na yeye mwenyewe kutojiamini. Ukimtazama Jenkinson huwa anacheza kama vile anatafuta kukubalika. Martin Keown amewahi kusema anacheza huku akiwaomba radhi mashabiki kwa kuwepo pale. Hii si nzuri hasa kwa mchezo mkubwa kama huu ambao macho mengi yatakua kwake.
Anapaswa kukumbuka kwamba alisajiliwa kwenye dirisha moja na Bellerin, tena yeye alianza kupata nafasi ya kucheza kikosini kabla yake. Zaidi ya yote ana umri wa miaka 24 sasa hivi. Kama ana ndoto za kuwa mchezaji mkubwa basi anapaswa kuipokea nafasi ya leo kwa mikono yake yote na amwoneshe mdogo wake (Bellerin) kwamba yeye ni kaka yake na mikononi mwake upande wa kulia wa Arsenal upo salama.
Bila Santi Cazorla ushindi huwa ni ngumu kidogo na ninalitarajia hilo leo. Japo Arsenal haina uhaba wa viungo lakini eneo hilo ndilo litakaloamua Arsenal icheze vipi.
Kwa vyovyote vile mashambulizi ya kushtukiza ni muhimu leo, hivyo unahitaji pasi ndefu zenye macho ambazo Granit Xhaka anaweza sana kuzipiga, lakini yupo pia Mohamed Elneny ambaye anaweza kuituliza timu na kupiga pasi katika maeneo salama.
Niliona Alexis Sanchez akifanya mazoezi na wenzake na bila shaka atatumika leo japo siyo kwa kiwango cha 100%. Sanchez anapocheza inakua ni faida kwa aina ya mchezo wa Arsenal kwa sababu hawahitaji sana akina Mesut Özil nyuma yake.
Sanchez hahitaji sana zile pasi za mwisho, badala yake anaweza kukimbia na mpira yeye mwenyewe na hata kugeuka nao, hali ambayo hutoa fursa kwa walishaji wake kutafuta kingine cha kufanya na tumeshuhudia akina Theo Walcott, Özil na hata Iwobi wakifunga kutokana na mijongeo ya uhakika ya Sanchez.
Hii ni tofauti sana na Olivier Giroud ambaye ni mtu wa kukaa kwenye nafasi, ikibidi kupiga 'one, two' lakini anahitaji sana pasi ili afunge hivyo ni ngumu kwa walishaji wake kutafuta kingine cha kufanya.
Lakini leo ambapo Man UTD hawana Erick Baily wala Chris Smalling kwenye safu ya Ulinzi inaweza kuwa rafiki kwa mifumo yote ambayo Arsenal wataamua kuitumia.
Kwenye safu ya ulinzi, Laurent Koscielny na Shkodran Mustafi hawajapoteza mchezo wowote tangu walipoanza kucheza pamoja. Leo kijana anaevutia sana Marcus Rashford atakua akijaribu kupita katikati yao, lakini watakua na kazi ya kumsaidia Jenkinson kukabiliana na akina Antony Martial na Juan Matta.
Siyo kubwa, lakini naiona sababu ya kufuta jina la Emmanuel Adebayor leo na kuandika jina la Sanchez, Özil, Walcott au Xhaka leo. Tukutane wakati mwingine.
twitter; @chardboy77
No comments