BAADA YA KUWAKOSA ETHIOPIA SASA TAIFA STARS KUCHEZA NA ZIMBABWE
Baada ya kukosa mchezo wa
kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ethiopia, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa
Stars’ imepata mwaliko wa kucheza na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa
kimataifa unaotarajiwa kufanyika jijini Harare, Novemba 13.
Kama ilivyotokea kwa Ethiopia
kuomba nafasi hiyo kwa Tanzania, pia Zimbabwe imefanya hivyo na mara moja
Tanzania imethibitisha kucheza mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa wenye kutoa
tathmini ubora ili kuingia kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa
la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kuikosa Ethiopia ambayo
ilitoa taarifa baadaye kuwa isingeweza kuihodhi Taifa Stars kwa sababu ya hali
mbaya ya hewa kwa kipindi cha Oktoba mwanzoni, kulisababisha Tanzania iliyokuwa
imejiandaa kucheza mechi hiyo kushushwa kwa kiwango kikubwa nafasi ya ubora wa
viwango vya FIFA kutoka ya 132 hadi zaidi ya 144. Zimbambwe kwa sasa ni ya 110
na Ethiopia ni ya 126.
Tayari Kocha Mkuu wa Taifa Stars,
Charles Boniface Mkwasa amepewa majukumu ya kuanza maandalizi na wakati wowote wiki
hii atatangaza kikosi ambacho kitawavaa vijana hao wa Mheshimiwa Rais Robert
Mugabe wa Zimbabwe.
“Ni kipimo kizuri, ni timu nzuri
kucheza nayo,” alisema Mkwasa alipozungumza na Mtandao wa TFF ambao ni www.tff.or.tz.
Taifa Stars ambayo kwa sasa haina
mashindano au kujiandaa na mashindano yoyote baada ya kutolewa nafasi ya
kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika, inajipanga huku ikisubiria ratiba mpya za
Baraza la Mpira wa Miguu Afrika Mashariki (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
No comments