SAKATA LA MALIPO YA HASSAN KESSY KUJULIKANA KESHO ALHAMISI.
Msuluhishi wa kisheria wa sakata la madai ya Simba dhidi ya Young Africans na Mchezaji Hassan Hamisi Ramadhani maarufu kama Hassan Kessy, Mzee Said El-Maamry anatarajiwa kukutana na pande zinazopingana Alhamisi Novemba 3, mwaka huu ili kufikia mwafaka wa madai hayo.
Taarifa kutoka TFF imesema kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliagiza pande za Simba na Young Africans kumaliza suala hilo mapema mwezi uliopita, lakini kwa sababu zilizo nje ya TFF na Kamati yake walishindwa kufanya hivyo hali iliyopelekea kupewa barua ya wito kuitwa kikaoni Oktoba 29, mwaka huu.
Hata hivyo, msuluhishi huyo alishindwa kuendelea na kikao hicho baada ya taarifa kutoka Young Africans kusema kwamba mmoja wa Wawakilishi wake, Wakili Alex Mgongolwa yupo safarini Iringa alikokwenda kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.
Kutokana na hali hiyo, E-Maamry amepanga sasa kukutana na wawakilishi wa pande zote mbili Alhamisi saa 11.00 jioni kwenye ofisi za TFF ili kuangalia namna ya kumaliza madai ya Simba iliyowasilisha mashauri mawili ambako moja ni dhidi ya Young Africans ilihali jingine ni dhidi ya mchezaji Hassan Kessy.
Mzee El-Maamry amesema: “Ili kutenda haki, lazima tutoe nafasi kwa pande zote kusikiliszwa. Ni vema Mwanasheria wa Young Africans akasubiriwa.”
Kamati ya TFF inasuburi makubaliano hayo, na ikitokea imeshindikana, suala hilo litarudi kwenye Kamati hiyo kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria zinazoongoza mpira wa miguu.
No comments