HUSSEN SHARIF NA ERICK KYARUZI WATUMBULIWA KAGERA SUGAR, WANATUHUMIWA KUIHUJUMU TIMU.

Magoli sita ambayo Kagera Sugar walifungwa na Yanga nyumbani Kaitaba mwishoni mwa juma yamezua jambo ndani ya kambi ya klabu hiyo iliyoko Misenyi mkoani Kagera.

Zilianza kama tetesi kwamba kuna dalili za hujuma katika kikosi hicho ambazo zimepelekea kikosi hicho chenye wachezaji wengi wazoefu kupokea kipigo hicho.
Habari kutoka ndani ya kambi ya Kagera Sugar ni kwamba golikipa Hussen Shariff na mlinzi Erick Kyaruzi 'Mopa' wamesimamishwa kutokana na tuhuma hizo.
"Ni kweli, tumewasimamisha hao wachezaji na wana tuhuma ambazo kwa sasa siwezi kuziweka wazi kwa sababu bado ni tuhuma."
Alisema mpasha habari wetu ambaye hakuwa tayari kuwekwa wazi kwa sababu si msemaji wa klabu hiyo lakini akaongeza kwamba habari inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wachezaji hao ndiyo yenye ukweli kwa kiasi kikubwa.
"Wewe mwenyewe si umeona viwango vilivyooneshwa na hao wachezaji? Na hata ukiangalia vyombo vingi vya habari vimeinasa hiyo habari ingawa sisi hatujatoa sababu ya kuwasimamisha lakini ipo hivyo hivyo. Hao wachezaji mpaka sasa hawapo kambini"
Katika mchezo huo dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, golikipa Hussen Shariff ilibidi atolewe kipindi cha kwanza baada baada ya kukubali mabao matatu ambayo yote yalitokana na makosa yake kiufundi. Nafasi yake ilichukuliwa na David Burhan ambaye hata hiyo naye alipokea magoli matatu.
Kagera Sugar watakua na kibarua kingine kesho Ijumaa watakapowakaribisha Azam FC kwenye uwanja wa Kaitaba.
"Maandalizi yote yamekamilika, juzi na jana tulifanya mazoezi Kaitaba, leo ni zamu ya wageni (Azam FC), sisi leo tunajifua huku huku kambini kwetu, ukiacha Casilas na Mopa, tutawakosa pia Paul Ngwai na Juma Jabu ambao ni majeruhi"

No comments

Powered by Blogger.