TUNAPOCHEZEA SOKA LETU HAPAFANANI NA SISI.
Na Richard Leonce
Ni watu wachache Tanzania wenye jinsia ya kiume ambao si walemavu na hawakuwahi kuicheza soka hata kidogo mitaani. Hadi leo pamoja na uhaba wa viwanja vya wazi kwenye mitaa yetu, bado watoto na vijana wanaupiga tu hata barabarani japo siyo kwa kiwango kile. Wengine wamehamia kwenye 'Play Stations' ambako nako wanaendeleza mapenzi yao kwenye mpira. Kwa ufupi, Soka ni mchezo pendwa hapa nchini.
Mungu hakunyimi vyote, pamoja na kwamba huwa hatufiki mbali kwenye soka la kimataifa, lakini kuna vitu tunavyo ambavyo hata kwenye mataifa jirani havipo.
Soka letu limejaaliwa Yusuph Manji, limejaaliwa Mohamed Dewji, Limejaaliwa Nassor Binslum, limejaaliwa Familia ya Bakhresa, limejaaliwa Azam Media, Limejaaliwa mchezo wa Simba Vs Yanga nk.
Leo napenda nijikite kwenye hiki kitu ambacho hatuna, kinaninyima raha sana mimi. Si kingine zaidi ya mahali pazuri pa kuchezea mpira wetu.
Viwanja vyetu vingi vinakatisha tamaa kwa kweli na havitoi maudhii hasa ya utamu wa soka letu.
Fikiria jinsi unavyotumia wiki nzima kuisubiri kwa hamu mechi kati ya Coastal na Yanga pale Mkwakwani Tanga. Siku inafika, umetulia kwenye sofa sebuleni kwako na glasi yako ya mvinyo, unaitazama Luninga yako ya kisasa yenye hadhi ya mwonekano Ang'avu (HD).
Unawaona wachambuzi mahiri wakiwa wamevalia suti za bei mbaya. Kisha unamaliza kwa kuwaona wachezaji mahiri, wa thamani wakihangaika kupambana na uwanja ambao hauruhusu hata mpira kuserereka. Kwa kweli inakatisha tamaa.
Wadhamini wa ligi zetu wanaweka pesa nyingi sana kwenye mpira, ni pesa nyingi ukilinganisha na pesa inayowekwa na wadhamini kwenye ligi za mataifa mengine ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Vilabu navyo vinalipa pesa nyingi kwa wachezaji na hata makocha kwa ajili ya kukonga nyoyo za mashabiki. Lakini mpira wenyewe unachezwa wapi?
Ni nani hatimizi wajibu wake hapa?
Viwanja vingi vya mikoani vinamilikiwa na chama cha mapinduzi. Sitaki nipoteze muda hapa kuidai haki ya viwanja hivi kurudishwa serikalini kwa sababu tuliwahi kuidai haki hiyo kwa bidii sana, tena wakati huo tukiwa na Rais mpenda michezo lakini ilikua kama tunampigia mbuzi gitaa. Basi tukubaliane kwamba viwanja ni mali ya CCM.
Lakini jamani ina maana CCM wameshindwa kutambua kwamba kwa umiliki wao wa viwanja tayari wao ni wadau wakubwa wa michezo? Hivi hawajui kama kupitia hivi viwanja wanaweza kuingiza pesa zaidi na viwanja vyenyewe vikawa katika hali nzuri?
Au hakuna hata mtu wa kuwaambia siri ya ule uwanja wa Arsenal kuitwa Emirates, Au ule wa Manchester City kuitwa Etihad?
Tusiseme kwa jeuri kwamba vilabu vijenge viwanja vyao. Suala la viwanja kutokua mali ya vilabu halifanyi iwe sahihi kwa wamiliki wa viwanja vilivyopo kuendelea kumiliki viwanja vibovu. Na haifanyi jukumu la kutunza viwanja lihamie kwa vilabu vya ligi kuu.
Huwa nashangaa sana. Siyo mara moja wala mara mbili nimewahi kushuhudia Kiwanda cha Kagera Sugar kikiingia gharama kuirekebisha 'pitch' ya uwanja wa Kaitaba, eti kwa sababu wanautumia kwenye ligi. Siyo vibaya, lakini je hawa wamiliki wana jukumu gani kama wamiliki? Au hawapati faida? na kama hawapati faidi inabidi tujiulize ni kwa nini.
Hapa ni lazima tuanze kubadilika. Tuwe na mawazo ya kujenga viwanja vipya vyenye miundombinu rafiki kwa mpira wa kisasa. Linaweza kuwa jukumu la vilabu lakini hata mashirika na taasisi binafsi zinaweza kujenga viwanja. Uwanja ni kitegauchumi kizuri tu.
Lakin wakati tunawaza hayo, hebu CCM nayo ituonee huruma basi. Natambua kwamba viwanja vingi vilijengwa zamani kwenye miaka ya 1970 hadi 1980 kwa hiyo miundombinu yake haikidhi na pengine kuvirekebisha unaweza kulazimika kuvifumua kabisa, Lakini jamani CCM hata ile sehemu ya kuchezea?
Vilabu na nyinyi sijui tutawaambia mpaka lini. Nyinyi hata viwanja vya mazoezi tu hamtaki kujenga. Yani Boko Veteran wanakua na uwanja, halafu timu ya ligi kuu haina. Muone aibu. Pesa ya kujengea uwanja siyo tatizo, kama hamna nendeni benki mkakope, deni halimfungi mtu. Mkikopa kwa ajili ya uwanja, uwanja wenyewe utalipa deni.
Inatia hasira kuona timu imejiandaa vizuri, imefanya mazoezi kwa mfumo fulani, lakini inashindwa kuutumia na kupelekea hata kupoteza mechi kutokana na ubovu wa uwanja. Hatuwezi kwenda mbele.
0766399341
Twitter: @RichardLeonce

No comments