ASANTE NONGA. SI DHAMBI KUKIOGOPA KIVULI CHAKO

Na: Ayoub Hinjo

Kila mtu ni shujaa wa maisha yake. Haijalishi ni ugumu au urahisi wa maisha lazima kuna kitu utakifanya kwa ushujaa na ikiwezekana hata watoto au wajukuu zako utawasimulia.


Paul Nonga ni shujaa wa maisha yake. Alichofanya Nonga ni ushujaa ambao wachezaji wengi wa bongo wanashindwa. Kiuhalisia hakuna mchezaji anayependa kukaa nje au kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika dunia hii ambayo kila mchezaji anatambua mpira ni kazi,sasa kwanini aingize pesa yake ikiwa hajaitolea jasho!?

Ushujaa wa kwanza wa Nonga ni pale alipojipiga moyo konde na kuamua kuivaa jezi ya Yanga huku akisisitiza hashindwi kugombania namba na wakina Ngoma,Tambwe,Busungu na Anthony wataalamu wa mambo wanasema utamu wa ngoma uingie ucheze. Inaonekana midundo ya ngoma inaenda kwa kasi ambayo Nonga haiwezi na hata kama anaiweza labda style za uchezaji zimemshinda kwa kubadilika badilika sana.

Nonga alikuwa shujaa wa Mbeya City kila mwisho wa wiki sio hapo tu aliupeleka ushujaa wake katika ardhi ya Shinyanga na kufanikiwa kuwa kipenzi cha Jamhuri Kiwelo. Katika safari yake ya kwenda Yanga alishindwa kuthibitisha hilo sababu kwanza alikutana na watu wengi ambao wanacheza nafasi moja na pili alikuta kuna watu walishaweka mizizi yao mipana katika nafasi hiyo. Labda Nonga alishindwa kuonyesha alichonacho kwa kuwa aliamini hata akiwa anafunga hatoweza kuwa katika kikosi cha kwanza na bahati mbaya zaidi kwake inawezekana presha ya kukabiliana na imani ya ushindi ya mashabiki ilikuwa kubwa kwake sababu hata sehemu alizotoka hakuna muhemko wa aina ile ya mashabiki.

Ushujaa wa kuamua kujitoa katika timu ndio ushujaa ambao ulimshinda Jerry Tegete. Sababu alikuwa na mapenzi binafsi na Yanga na kusahau uwezo wake ulikuwa unashuka na alisahau kuwa hata soko lake la mpira linaweza kuwa shida sababu hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara. Nonga anaamini katika kutafuta malisho mengine ambayo yatampa nafasi kurudisha uwezo wake na pia na nadhani katika vita ambayo alikuwa anapigana na kina Tambwe kuna vitu atakuwa amejifunza ili kuboresha ubora wake.

 Uzuri ni kwamba hakuna mchezaji asiyependa kucheza Yanga au Simba ni timu za historia katika maisha yao. Kuondoka kwa Nonga Yanga kunafungua milango kwa wakina Nonga wengine kuingia ndani ambao nao baadae wataaga na kuondoka na wengine kuingia tena. Najaribu kumwangalia Malimi Busungu kwa jicho la tatu jinsi maisha yanavyokuwa magumu kwake licha ya kuwa kiraka katika nafasi nyingi.

Wakati Paul Nonga anafunga magoli kila alivyotaka kipindi yupo Mbeya City au Mwadui magoli hayo hayo yalikuwa yanamkimbia wakati yupo Yanga. Ilimchukua nafasi nyingi kufunga goli moja au hasifunge kabisa nadhani hata kivuli chake mwenyewe kilikuwa kinamwogopesha Nonga na kuamua kuomba kuuzwa sababu alishaumwa na nyoka hata linapomgusa jani anashtuka.

No comments

Powered by Blogger.