NINACHOAMINI MAESTRO :SOMO LA FABREGASS NA OZIL BADO HALIJAELEWEKA KWA AKINA MSUVA.

Ndugu msomaji,
Mpira wa miguu ni mchezo unaoshirikisha watu 11 hili kutimiza idadi ya timu moja. Kwa maana hiyo mpira wa miguu ni mchezo wa ushirikiano wa watu 11 dhidi ya wengine 11. Ufanisi bora wa kazi kama kikundi cha watu 11 unatokea pale timu inapoibuka na ushindi na kishinda zawadi ambazo watakuwa wanashindania. Hiyo ndio kazi ya timu.



Muunganiko wa timu hutegemea utendaji kazi wa kila mshiriki hili kutimiza lengo lao. Pamoja na hayo yote naomba tuangalie utendaji kazi wa wachezaji wetu wa Tanzania ambao nao hutumia muda kuangalia mipira ya nje ya hapa nyumbani. Nahisi kuna kitu hawajakielewa kutoka sehemu wanayojifunza kupata ufundi wao. Nadhani ni vitu vingi ambavyo wachezaji wetu wanajifunza kutoka nje ya mipaka ya nchi lakini sidhani kama kuna uzingatiaji wa moja kwa moja kwa walichojifunza kutoka huko. Kuanzia nidhamu na hata ufanisi wa kazi wa kwenye mchezo husika hatuoni kile kinachowafanya wakeshe waangalie mipira ya Africa au Ulaya.

Kwa bahati nzuri wachezaji wetu wanaweza kujifunza kwa Thabani Kamusoko,Justice Majabvi,Niyonzima,Ngoma,Tambwe na hata wachezaji wengine ambao wana ufanisi bora wa kazi kuliko wachezaji wetu. Uwepo wa Kamusoko hapa Tanzania uwe chachu ya kujifunza kwa wachezaji wetu,huyu jamaa anafanya mchezo wa mpira uonekane ni rahisi sababu anafanya kile kinachostahili sio kama watu hawa hatuna kwenye nchini yetu,wapo wengi sana lakini tatizo ni ubinafsi wa umimi ndio umewajaa. Inawezekana wengi hawapati nafasi ya kumuona Kamusoko na hao niliowataja hapo juu. Mfano mzuri kwa viungo bora wa dunia Fabregas na Ozil hawa ni wachezaji wa timu tofauti wenye ufundi na ujuzi wa mpira.


Inawezekana kupitia Fabregas,Ozil na wengine tutajifunza somo bora hasa timu zetu zinaposogelea goli la wapinzani na hapo ndipo maana ya ushirikiano kama timu unaonekana. Inaonekana kama kituko kuwalinganisha wakina Ozil na wachezaji wa hapa nyumbani,nawafananisha sababu hapa Tanzania wapo wachezaji kama wakina Ozil lakini hawajitambui na kujifunza. Ufahari wakina Ozil ni kupiga pasi zenye macho na pasi za magoli kwa washambuliaji au mtu aliye kwenye nafasi hilo ni jipu kwetu,lazima litumbuliwe. Labda ni nafasi ngapi ambazo Msuva anajaribu kufunga lakini kwa sehemu ambayo yupo inashindikana!!? Ni nyingi sana na inapelekea hata yeye mwenyewe kufanya mashabiki wa timu yake kumzomea. Kama unataka kuwa Mamba lazima ujifunze kupitia Mamba la hasha itakuwa sivyo. Nikiwa namaana wachezaji wetu wengi wanataka kucheza soka nje ya mipaka ya hapa nyumbani lakini kuna mambo yanayowarudisha kwa kushindwa kukidhi mahitaji ya timu wanazoenda kwa hali kama hiyo lazima wakae chini na kujifunza tena kupitia huko wanakojifunza kisha walielewe vyema hilo somo sidhani kama kuna atakayerudi tena kutoka huko nje ya Tanzania.


Ufahari wa Ozil au Fabregas kutoa pasi ya goli ni mkubwa kwao kuliko kufunga goli lenyewe na hapo ndipo wakina Msuva na wenzake walitakiwa kujifunza kuwa kutoa pasi ya goli ni kufunga pia. Sio kama wakina Msuva hawapigi pasi za magoli,wanapiga pasi pale ambapo wanaona wao washindwa kufanya hivyo na mara nyingi kama wakiona wamechangia magoli mengi,ubinafsi wa uchoyo unaanza hapo ni kama kupunguza ushirikiano wengine na maana ya timu inakuwa haipo. Ya kujifunza kutoka kwa wenzetu ni mengi lakini tukiweza kukariri au kuelewa kile tulichojifunza tutafika mbali na kuona ladha kamili ya mpira ulio bora. Usione wakina Fabregas,Ozil na wenzake wanafanya vile sababu wanajua nini maana ya timu na ushirikiano wa kila mmoja kwenye ushindi. Wakati mwingine watu wetu wa karibu au mashabiki na wale wadau wakubwa wa mpira huthamini zaidi anayefunga magoli kuliko yule anayemfanya yule afunge na hio ndio husababisha ubinafsi na kukosa ladha kamili ya mpira. Utasikia atakaye funga goli anapata milioni moja,kwanini mtu akupe pasi wakati hata yeye anataka milioni. Mchango wa mtoa pasi hauonekani kwanini aliyetoa pasi asipate hata laki tano kwa pongezi ya msaada wake kwa mfungaji!!?

Wakina Msuva tukikaa chini na kujifunza kwa kina Ozil tutaelewa zaidi na kuona ufahari wa kazi unayofanya bila kujali timu timu unayocheza ina ukubwa gani na nafasi gani. Kumbuka tunajifunza kupitia makosa.

Imeandaliwa na : 
Ayoub Hinjo
E-mail: hinjo38@gmail.com
Simu: 0787624009/0719772772
@member: Manchester United Supporters in Tanzania 

No comments

Powered by Blogger.