IPO SIKU KILA MTU ATAISHANGILIA YANGA KUTIMIA LEO?
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, wenyeji timu ya Azam FC watawakaribisha Mabingwa wapya wa ligi hiyo msimu huu timu ya Young Africans maarufu kama Yanga.
Kitendawili kilichopo leo ni je Yanga wataibeba Simba? Na Je mashabiki wa Simba wataishangilia Yanga? Na hii inatokana na kuwa kama Yanga ikishinda leo itafufua matumaini ya Simba kuweza kupata nafasi ya pili ili kushiriki katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
Haijawahi kutokea kwa Timu hizo mbili ysni Yanga na Simba kila moja kumshangilia mwenzake au kushangilia kwa pamoja hivyo macho na masikio ya wapenda soka yatahitaji kuona tukio la leo kama Yanga wakishinda.
Simba ina pointi 44 katika nafasi ya tatu wakati Azam wao wana pointi 45 katika nafasi ya pili hivyo basi kama Azam ikishinda leo basi itakua imechukua nafasi ya pili na kufuta kabisa ndoto za Simba za kucheza michuano ya kimataifa lakini kama wakifungwa basi mshindi wa pili atapatikana katika mechi za mwisho ambapo Simba itacheza na JKT Ruvu wakati Azam watacheza na Mgambo.
Mechi hiyo ya leo ni no. 141 na itachezeshwa na mwamuzi wa kati Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika vibendera Frednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (Dsm), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hussein Kalindo (Dsm) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian Mabena kutoka Tanga.
Katika mchezo huo timu ya Young Africans itakabidhiwa Kombe lake la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr Fennela Mkangara.
Mchezo huo wa leo unatarajiwa kuanza majira ya saa 11 kamili jioni, kwa saa za Afrika Mashariki na kati ili kutoa fursa kwa wadau, wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kushudia mchezo huo pamoja na shamrashamra za kukabidhiwa kikombe.
Young Africans watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu na mgeni rasmi, huku wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wakimkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili Mrisho Ngasa na fedha taslimu sh. millioni moja
No comments