USTADHI BENZEMA NASUBIRI JAPO UVITAMANI KILE KITI NA KOFIA.


Historia inaniambia Kuwa kale palikuwepo na tawala nyingi ambazo zilikuwa kubwa kupita kiasi na wafalme wao walionekana kama kuutawala ulimwengu kwa ujumla kiutendaji kazi mojawapo ikiwa Tawala ya warumi.
Lakini hii haikuondoa ukweli Kuwa kulibaki tawala ambazo zilikuwa ndogo na zikabaki Kuwa bora na Kuwa na viongozi wao waliowaheshimu na kuwalinda kisha kuwazika kwa utukufu wa hali ya juu.    Hata soka lipo huku kwa sasa,  kumekuwa na Dunia mbili kwa sasa, moja anaitawala Messi, nyingine anaitawala Ronaldo Cristiano. Wametengeneza matabaka Yao wenyewe. Ufalme wao wenyewe. Tupo katika upofu ambao umetuzuia kuona japo vidogo anavyovifanya Hazard katika uwezo wake,  ama Neymar na ustadhi Kareem Benzema na wengine wenye uwezo huu.  Walikuwepo wawili tu ambao walijaribu kulinganishwa nao, Suarez wa Liverpool maana huyu wa Sasa kaenda kumtumikia mfalme na Ibrahimovic Zlatan. Hawa waliweza kutengeneza Ufalme wao mdogo mdogo huku chini,  wakaweza kupigana Walau wapate magoli 30 kwa msimu na hapa wakapata mashabiki na nchi walizokuemo zikawa na watu wa kujivunia, maisha Yao mbele ya Camera yakawavuta Zaidi wakawa kivutio Zaidi. Ndio hawa waliamua kutengeneza Ufalme wao wenyewe na wakaabudiwa na kuimbwa kwa kiasi chake.

Kuna njia kuu tatu katika maisha ya soka kwa wale wenye mvuto wa Kuwa World beaters (wakuiteka Dunia) hasa washambuliaji. Moja ni kuanza kwa kupigana, ukaipa timu magoli yako murua,  ukafunga unavyojisikia na kuipa timu ubora kupitia wewe hata kama sio ubingwa. Hapa wewe utakuwa mfalme wa kutupwa, utapendwa na kuimbwa maradufu, kisha unachagua kama hukupata mafanikio uliyotaka unaenda kuungana na mfalme mkubwa ambaye una uhakika muunganiko wenu utakupa unachotaka au kama umeshinda baadhi ya vitu unachagua sehemu moja yenye malisho bora unapishana na mfalme ambaye kachoka unaenda kuendeleza maisha yako. Hii ndio njia ambayo Luis Suarez, Neymar, Bale na Ronaldo wameipitia ingawa Bale na Neymar wanaweza wakawa na Muda wa kuirudia kwenda kutafuta Ufalme wao wenyewe.  Kuna hii nyingine ya Akina Messi, unakuzwa kuja Kuwa mfalme, unasubiri Ronaldinho achoke utumie nafasi basi, na kuna hii ya mwisho ambayo unakuja kwa mfalme unamsaidia kwa kila kitu, kwa nguvu zako zote na anakusaidia kushinda kila kitu kisha unaenda sehemu nyingine kutafuta ufalme wako mwenyewe. Hapa ndipo Benzema alipo. Hapa ndipo ambapo ameamua kuozea. Benzema yupo katika umri sahihi wa ukomavu kwa washambuliaji, lakini bahati nzuri kwake ukomavu umekuja akiwa kapata kila kitu muhimu katika ngazi ya klabu upande wa mataji.  Katika ulimwengu huu wa upungufu wa washambuliaji wa kati hana sababu ya kuendelea kuishi nyuma ya Ronaldo,  Bale na sasa James Rodriguez pengine pia nyuma ya Sergio Ramos. Anatakiwa awe mahala ambapo analiliwa, jezi zake zinapiganiwa na jina lake limetungiwa nyimbo kadhaa za kumsifu. Kama Sturridge amefikia hatua ya kuabudiwa ndani ya misimu miwili kwanini sio yeye aliyekuwa bora tena nyuma ya vivuli vya watu kwa zaidi ya misimu minne.

Mwanasaikolojia mmoja na mtu aliyehusika sana na kusoma tabia za watu Abraham Maslow aliwahi kusema mshindani wako wa kwanza maishani ni uwezo wako mwenyewe,  na kushindwa kwako ni pale utakaposhindwa kutumia nafasi zako mwenyewe. Kwake kwa kauli hii kila mtu angeweza kuwa mfalme. Hata Benzema yupo hapa, mshindani wake wa kwanza ni uwezo wake mwenyewe, hajaamua kuuweka mbele ya kina Lewandowski au Aguero. Na sisi hatuwezi kuamini kama anawashinda kwa sababu hajaamua kutoka kwenye kivuli, lakini inauma wakati mwingine ambapo mtu unayemweka benchi Olivier Giroud jina lake linapazwa kwenda angani kuliko wewe. Na yule Kane ambaye kaibuka msimu huu ghafla atakuwa na thamani kuliko wewe, hata Bas Dost wa Wolfsburg atatafutwa kuliko wewe. Lakini ukweli haupo hivyo, Benzema bado anafanya mengi makubwa kuliko hawa. Wakati Arsenal wanaye Giroud, Liverpool Sturridge, Manchester wanahangaika na Falcao aliyetoka majeruhi na Rooney anayehitaji msaada huku Van Persie akiwa anajichokea,  kule Dortmund hakuna wakumtaja kati ya wale Ramos na Cirro Immobile. Hizi zilikuwa sehemu sahihi kwa Benzema kuweka kiti chake cha enzi. Zilikuwa sehemu ambazo angeabudiwa na kutukuzwa. Hawa wote wanamis watu sahihi wa kuwaimbia nyimbo, watu sahihi wakujichora tattoo zao, hata dunia imemis watu wa kuweza kufunga goli 25 na kusaidia mengine 10 katika hizi ligi. Benzema anaiweza kazi hii, anahitajiwa kwa kazi hii,  bahati mbaya moja tu, hajahitaji kuifanya kazi hii. Kile kiti cha dhahabu na kofia ya kipekee kwake haijawa kitu bado, natamani avifikirie hivi vitu na atakuwa kafanya uamuzi sahihi. Nani asiyetamani kufanya uhuni wa Suarez na bado unatetewa,  unaamua kukanyaga kama Costa na bado unaonekana malaika, au unaamua tu kugomea mkataba kama Sterling ambaye hajafika hata huko na unaliliwa. Siku akiziota kofia na kiti cha utukufu atakuwa katika njia sahihi. Ufalme ndio kitu pekee alichobakisha kushinda lakini anaamua kujichelewesha na kutuchelewesha. Ahsanteni
By Nicasius Coutinho Suso

No comments

Powered by Blogger.