KILA LA KHERI YANGA JUMAMOSI



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar  es salaam.

Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wa jumamosi, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.

Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).

Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel itasuburia kucheza  mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).

Wakati huo huo wapinzani wa Young Africans timu ya Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili  saa 9 usiku kuamkia ijumaa kwa usafiri wa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair   bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tunisia  (FTF), Bw. Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya Etoile du Sahel (ESS) Bw.Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10

Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.


++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments

Powered by Blogger.