INSIDE UNITED : MAMBO UNAYOPASWA KUYAJUA KUHUSU MANCHESTER DERBY
Katika INSIDE UNITED leo tunaangalia mchezo wa pili wa ligi kuu nchini England kati ya Mahasimu wa jiji moja la Manchester hapa naizungumzia timu yenye mafanikio kuliko timu zote katika soka la England Manchester United dhidi ya Mabingwa Watetezi Manchester City.
Timu hizi zinakutana muda mfupi ujao katika dimba la Old Trafford ikiwa ni mechi ya pili msimu huu kwa timu hizo ile ya kwanza ikiisha kwa United kukubali kichapo cha bao 1-0 katika dimba la Maine Road lililokua likitumiwa na Manchester City.
HISTORIA
Mechi ya kwanza baina ya timu hizo ilipigwa mwaka Novemba 12 mwaka 1881 ikiwa ni zaidi ya miaka 130 iliyopita katika uwanja wa Man City Wakati huo Manchester City ilijulikana kama WEST GORTON na Manchester United ikijulikana kama NEWTON HEARTH.Mechi hiyo ilimalizika kwa Newton Hearth (Man United) kuibuka na ushindi wa bao 3-0 . Wakati huo haikuonekana kama ni mchezo muhimu wenye upinzani mkali kama ilivyo hivi sasa kwani kulikua na timu nyingi katika jiji la Manchester ambazo zilikua zikishindana zenyewe bila kuwa na Ligi kama ilivyo hivi sasa.
Mechi ya kwanza katika ligi daraja la pili (Championship hivi sasa) baina ya timu hizo ilikua msimu wa mwaka 1894-1895 ambapo Man United iliitandika Man City bao 5-2 .
Mwaka 1906 Ilikua mwaka ambao timu hizi zilikutana kwa mara ya kwanza katika Ligi Daraja la Kwanza (Ligi kuu hivi sasa) ambapo Manchester City iliibuka na ushindi wa bao 3-0 mechi ambayo inasemekana ilikua na mvuto wa hali ya juu hata kuvunja rekodi ya mapato ya mlangoni zikipatikana zaidi ya paundi 1,000 (Zaidi ya milioni 2.5 za Kitanzania hivi sasa)
Pesa ambazo zilikua nyingi mno wakati huo.
Wachezaji wanne wa Man City waliojiunga na Man United (Jimmy Bannister,Herbert Burgess,Billy Meredith na Sandy Turnbull) waliisaidia Man United kupata ubingwa wa Kwanza katika historia ya klabu hiyo mwaka 1908 na msimu uliofata Sandy Turnbull alikua mchezaji wa kwanza kupewa kadi Nyekundu katika mechi hii.
Moja kati ya watu wanaoheshimika katika klabu ya Man United ni Dennis Law huyu jamaa George Best na Sir Bobby Chalton wanakumbukwa kwa kuifanyia makubwa Man United hali iliyopelekea kuweka sanamu zao nje ya uwanja wa Old Trafford lakini Huyu Dennis Law ndiye aliyeishusha Daraja Man United mwaka 1970 wakati huo akihama toka United kwenda Man City alifunga bao pekee lililoipeleka Man United kushuka daraja na baada ya kuona hilo Law alijistukia na kustaafu kucheza soka msimu uliofata.
Msimu wa mwaka 1986-87 wakati Man United wanabadilisha Kocha kwa Alex Ferguson kuchukua nafasi ya Ron Atkinson na hatimae kumaliza Ligi wakishika nafasi ya 11 majirani zao Man City walishuka daraja msimu huo.
Mechi ya kwanza kwa Alex Ferguson akiwa kama kocha wa Man United dhidi ya Man City ilikua ni katika kombe la FA Ambapo Man United ilishinda bao 1-0 huku mechi ya kwanza katika ligi kwa Ferguson dhidi ya Man City mwezi March mwaka 1987 bado United ilishinda bao 2-0.
REKODI MUHIMU
Mpaka leo imeshapigwa michezo 168 baina ya timu hizi katika mashindano yote huku Man United ikishinda mara 69, Man City ikishinda mara 49 huku timu hizi zikitoka sare mara 50.Ryan Giggs wa Man United ndo mchezaji anayeshikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi baina ya timu hizo akicheza mara 36 katika mara 168 walizokutana.
Wayne Rooney wa Man United anashikilia rekodi ya mchezaji aliyefunga magoli mengi kabisa baina ya timu hizo akifunga mabao 11 mpaka sasa.
Mechi ambayo iliingiza mashabiki wengi uwanjani baina ya timu hizo ilikua mechi iliyochezwa tarehe 20 Septemba 1947 ambapo mashabiki 78,000 waliingia katika uwanja wa Maine Road ambao ulikua ukitumiwa na timu zote hizo kufatia uwanja wa Old Trafford kuathiriwa na Vita kuu ya pili ya dunia.
Kocha aliyeipatia mafanikio makubwa Man United Sir Matt Busby aliwahi kuichezea Man City zaidi ya mechi 200.
MECHI YA LEO
Wakati Man United ikiwa katika kiwango bora hivi sasa ikiwa imeshinda mechi dhidi ya Tottenham,Liverpool na Aston Villa na kuipandisha mpaka nafasi ya 3 katika msimamo, Man City hali yao si nzuri sana kwani licha ya kutupwa nje dhidi ya Barcelona katika ligi ya mabingwa Man City wamepoteza nguvu yao ya ushindi na wataingia katika mchezo wa leo wakiwa katika nafasi ya 4.
Mchezo wa mwisho baina yao Man City walishinda bao 1-0 goli la Sergio Aguero



No comments