KUMEKUCHA: SIMBA YAANZA LIGI RASMI
Klabu ya Simba hatimae imeanza ligi rasmi baada ya kupata ushindi wake wa kwanza katika ligi ikiwafunga Ruvu Shooting bao 1-0.
Iliwachukua Simba Dakika 77 kupata bao pekee katika mchezo huo baada ya juhudi binafsi za Emmanuel Okwi baada ya kutengeneza na kufunga bao akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Ruvu Shooting baada ya shuti la Elias Maguli.
Ikicheza mchezo wa kawaida kabisa Simba ilionekana kupoteza nafasi nyingi za Wazi huku Emmanuel Okwi akiwa ndiye mchezaji bora wa mchezo huo.
Simba walifanikiwa kulishambulia vilivyo lango la Ruvu Shooting wakipiga mashuti 14 ikiwa 8 kati ya hayo yakilenga goli na 6 yakitoka nje ya lango wakati Ruvu Shooting wao wakipiga mashuti matano tu kati ya hayo mawili yakilenga lango na matatu takitoka nje ya lango la Simba.
Ni mchezo ambao ulishuhudiwa Simba wakipata kona 9 huku Ruvu Shooting wakitoka bila kupata kona yoyote.
Kwa matokeo hayo sasa Simba imefikisha pointi 9 baada ya kucheza mechi 7 ikiwa ni timu ya pili baada ya Mtibwa Sugar kutofungwa mchezo wowote katika ligi mpaka sasa wakati Ligi hiyo ikisimama mpaka Disemba 26 kupisha michezo ya Timu ya Taifa hasa mashindano ya Challenge yanayoandaliwa na Shirikisho la soka Afrika mashariki na kati CECAFA.
Katika mchezo mwingine jioni hii JKT Ruvu ilibamiza Ndanda FC ya Mtwara bao 2-0 katika mchezo uliopigwa katika dimba la Chamazi.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++


No comments