TAIFA STARS NOMA YAIPIGA BENIN BAO 4-1 MBELE YA PINDA
Mfumo wa 3-5-2 uliotumiwa na kocha wa Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars Martin Noij uliweza kuwapa maelfu ya mashabiki wakiongozwa na Waziri Mkuu mh. Mizengo Pinda ambao waliohudhuria pambano la kimataifa la Kirafiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania dhidi ya Benin furaha kwa kuibuka na ushindi wa bao 4-1.
Silaha kubwa ya ushindi leo ilikua ni kujaza viungo wengi katikati ambao waliharibu kabisa mipango ya Benin na kufanya Washindwe kupita kwenda katika goli la Stars ambalo leo alianza Mwadin Ally badala ya Deo Munishi ambaye amekua akianza katika mechi nyingi.
Alikua ni nahodha Nadir Haroub Cannavaro aliyewainua Watanzania baada ya kupiga goli la kwanza dakika ya 16 ya mchezo akiunganisha mpira wa adhabu ndogo ya Erasto Nyoni.
Bao la Pili la Stars lilifungwa na Amri Kiemba baada ya kuuwahi mpira uliokosewa na beki mmoja wa Benin hivyo kufunga kwa urahisi.
Mpaka mapumziko Stars walikua mbele kwa magoli hayo Mawili.
Kipindi cha pili Stars walikuja na nguvu zaidi na kuweza kupata bao la 3 dakika nne tu baada ya mchezo kuanza kipindi cha pili lakini safari hii alikua ni Thomas Ulimwengu akiunganisha krosi ya Mrisho Ngasa.
Juma Luizio aliipatia Stars bao la 4 dakika chache baada ya kuingia kufuatia kazi nzuri ya Thomas Ulimwengu ambaye alionekana kuwasumbua vilivyo Benin.
Goli la kufutia machozi la Benin lilipatikana dakika za lala salama kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na nahodha wao anayekipiga Katika klabu ya Wes Brom ya Nchini England Stephen Sessignon na kumpasia mfungaji Suanon Fadel ambaye alifunga kiurahisi.
TATHMINI YA MCHEZO
● Mfumo alioutumia kocha Wa Stars wa kujaza viungo wengi katikati ya Uwanja na kuwaacha Thomas Ulimwengu na Amri Kiemba uliwapa mwanya washambuliaji hawa kuisumbua ngome ya Benin huku mipira mingi ikizuiwa na viungo wa Stars pale katikati na hii pia ilisaidia kutosumbuliwa kipa Mwadini.
● Kuna kitu ambacho mwalimu anapaswa kukifanya wakati huu nadhani anapaswa sasa kuingiza vijana zaidi katika kikosi hiki ili kuiandaa timu kwa mechi za kufuzu kucheza kombe la Dunia za mwaka 2018.
Inapaswa sasa kuachana kidogo kidogo na baadhi ya wachezaji ambao wana umri mkubwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana ambao wanapaswa kuingia taratibu katika timu ili kupata uzoefu.
● Taifa Stars iliweza kupata mashuti 7 yaliyolenga lango la Benin na manne kati ya hayo yalizaa goli huku ikipiga mashuti matano yaliyotoka nje ya goli hii inaonyesha kabisa mfumo huo wa kujaza viungo wengi unaweza kufanikiwa na kuwapa nafasi washambuliaji kufanya yao pale mbele.
Tulifanikiwa kumiliki mpira kwa zaidi ya 55% hii ilionyesha pia viungo wa kumiliki mpira na kukaba tunao ila tatizo hapa linaweza kuwa ni umri wa viungo hao ambao wengi wanaelekea ukingoni.
ASANTENI
Imeandaliwa na Edo Daniel Chibo
Nicheki kama una lolote kupitia
0715 127272(Whatsapp)
wapendasoka@gmail.com (email)
Edo Daniel Chibo (Facebook)
Wapenda Soka - Kandanda (like page katika facebook)
No comments