SOKA LA BONGO : MACHO HAYAONGOPI, HUU NI MWISHO WA ENZI
Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara imesimama kwa muda kupisha
maandalizi na mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaoihusisha timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya timu ya taifa ya Benin.
Timu zote zimecheza michezo mitatu mitatu ambayo imeshuhudia Mtibwa
Sugar wakikaa kileleni baada ya kukusanya alama 9 kwa kushinda michezo
yao yote waliyocheza.
Wapenzi wa mpira wa miguu na hususani ligi ya nyumbani wanapata
burudani sana msimu huu, wanashuhudia ligi yenye ushindani na
isiyotabirika. Tena kwa macho yao tofauti na zamani ambapo tulizoea
kupata soka kwa mbwembwe za mtangazaji wa redio.
Wanashuhudia ligi yenye msisimko mkubwa ukilinganisha na ligi za misimu kadhaa iliyopita ambapo kuna baadhi ya timu zilikua zikikusanya
tu alama kirahisi licha ya kuwa na vikosi vya kawaida sana. Lakini msimu huu hali ni tofauti kabisa.
Timu zote zinaonesha kuwa na hamu ya kupata matokeo mazuri kutokana na maandalizi mazuri ambayo wameyafanya. Maandalizi ndiyo yanayochangia kazi nzuri inayoonekana viwanjani kwa sababu viwango vya wachezaji wengi wa ligi kuu ya Tanzania vipo sawa, kinachowatofautisha ni maandalizi na hamasa tu.
Hamasa ya udhamini ina mchango wake katika hili. Hakuna timu ambayo inatamani kushuka daraja kwa sababu kuna udhamini wa pesa zadi ya shilingi milioni mia moja kwa kila timu inayoshiriki ligi kuu kutoka kwa wadhamini ambao ni Vodacom na Azam Media.
Milioni mia moja siyo pesa ndogo kwa timu yoyote hapa nchini. Hali haiwezi kuwa sawa na wakati ule ambapo haikuwepo.
Kitu cha kutia moyo ni kwamba makampuni yameanza kujitokeza kudhamini timu nyingine tofauti na Simba na Yanga. Hizi siyo enzi zile ambapo Simba na Yanga walikua na uhakika wa kumnasa mdhamini yeyote yule ambaye angeamua kutangaza biashara yake kupitia soka.
Inapendeza sana kuona sasa jezi za timu nyingi zina nembo za wadhamini tofauti tofauti vifuani. Inaongeza hadhi ya ligi yetu lakini pia ni chamgamoto kwa timu nyingine kufanya vizuri ili wadhamini waendelee kujitokeza.
Hakuna uchawi, kama ubingwa utaenda kwa Mbeya City au Kagera Sugar, ni wazi kwamba udhamini mnono utakwenda kwao. Ule ufahari uliokithiri wa Simba na Yanga unafikia mwisho wa enzi kwa kasi sana na sasa vigogo hao wanalazimika kufanya kazi kubwa uwanjani kutafuuta matokeo kama timu nyingine.
Tumeshuhudia matokeo ya sare tatu mfululizo waliyoyapata Simba, tena katika uwanja wa Taifa ambao wameuzoea sana tofauti na timu walizokutana nazo. Unajiuliza itakuwaje wakienda Sokoine au Kaitaba?
Hawana jinsi, wanapaswa kujipanga vizuri zaidi ili wasiendelee kuumbuka. Yanga wao wanaonekana kufaya kazi kubwa baada ya kushtushwa na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar katika mpambano wa kwanza wa ligi. Wameshinda mechi zao mbili zilizofuata lakini siyo kirahisi sana kama ilivyozoeleka. Wameshinda baada ya kazi nzito sana uwanjani.
Azam FC nao wameoneshwa kwamba hii siyo ligi laini kama wanavyodhani, baada kushindwa kutikisa nyavu za Tanzania Prisons pale Sokoine. Hii yote inakuonesha kwamba hizi ni zama nyingine kabisa.
Mpira hauchezwi tena magazetini kama zamani. Hakuna atakayekupigia porojo kwa mbwembwe kwamba Jaja ni mkali kuliko washambuliaji wote wa ligi kuu, kila kitu kinaonekana moja kwa moja uwanjani na mtazamaji ataamua.
Mtazamo wa wachezaji juu ya soka lao umebadilika pia. Hawazitazami tena Azam, Simba na Yanga kama timu pekee za kucheza mpira kwa kiwango cha juu.
Haya ndio matunda ya udhamini mzuri kwenye vilabu.
Idi Mbaga hana tena sababu ya kubembeleza kubaki Yanga wakati JKT Ruvu wanamuhitaji na wana uwezo wa kumpa maslahi mazuri.
Nimefurahi sana kuwaona watu kama Reliant Lusajo, Edward Christopher, Rulanga Mapunda, Selemani Kassim na Danny Mrwanda wakizitumikia timu ambazo siyo tu zinawapa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu kila wiki, bali pia zinawaweka mbali na presha kubwa ya matusi kutoka kwa
kashabiki.
Wanachopaswa kufanya wachezaji hao ni kutuliza akili zao na kufanya kazi tu. Ingekua enzi zile tungeambiwa wamekwisha, lakini enzi hizi hakuna wa kutudanganya. Kama wamekwisha tutawaona na kuthibitisha kupitia uwezo wao uwanjani.
Hakuna asiyetamani lile bao la Jabir Aziz dhidi ya Yanga lingefungwa na mshambuliaji wa timu yake. Nilipolitazama nilitikisa kichwa nikimaanisha ndio ndio, anaejua anajua tu.
facebook :Richard Leonce Chardboy
twitter :@chardboy77
email :chardboy74@ gmail.com


No comments