MAENDELEO YA SOKA LETU: WATANZANIA NA MAISHA YA NGUVA



Katika Maisha mwanadamu hutegemea sana maamuzi. Hili ndilo jambo ambalo wengi linawashinda, wengi linawaponza na wengi linawarudisha nyuma. Maamuzi huenda sambamba na ndoto, mtu mwenye ndoto siku zote hufanya maamuzi yaliyo sahihi zaidi kulingana na ndoto zake.

Hapa ndipo Tatizo la sisi watanzania lilipo, hapa ndipo waafrika wengi wanafail. Hatuna maamuzi stahiki kwa ndoto sahihi. Tunaishi kwa sababu tunatakiwa kuishi na si kwa namna tunayopaswa kuishi. Tunamfanya Mengi aonekane ana akili kupita kiasi, tunayatizama Maisha ya Bakhresa kama bahati mwisho tunamuona Samata ni ngekewa. Hii ndio Tabia yetu, hapa ndipo hulka yetu imelala.

Si ajabu kumsikia Abdulhalim Humoud akikwambia Azam wamemkwamisha kwenda South Africa baadae akaingia Simba akatulia na asifanye lolote, kama Azam walikwamisha ndoto maamuzi yapi aliyachukua alipotua Simba. Hii ni akili ambayo sio yeye Tu hata Simon Msuva nadhani anayo, hata mtoto anayekuja huku chini anayo, maamuzi stahiki kwa ndoto sahihi. Hii akili ndio yetu watanzania, ya viongozi wetu na pia ya wazazi wetu. Akili ya Jonas Mkude inamuwaza zaidi Kwizera kuliko ndoto za kucheza Southampton kama Wanyama. Alimuwaza Mbiyavanga, akamuwaza Joseph Leo anamuwaza Kwizera wakati pengine Kwizera ataenda El Merreikh ataanza kumuwaza chipukizi mmoja wa Mwadui Fc atakayetakiwa Simba. Na hapa ndipo Tatizo lilipo, hata viongozi wanawaza hivi, wanawaza Simba kama jina na sio Taasisi, ndivyo ambavyo Yanga pia imedumu na ndoto ya Shabaan Nonda mpaka kesho. Maamuzi stahiki kwa ndoto Sahihi. Na mashabiki tupo hapa, watanzania tupo hapo, tunamlilia Emmanuel Okwi kuliko tunavyoweza kumwandaa Chanongo, Okwi akiwa mapumzikoni unasikia tunalalamika Burundi kutufunga. Unalia nini wakati akina Msuva unawaona wanastahiki nafasi katika benchi na sio uwanjani.?



Mwasisi wa Taifa hili hayati Mwalimu J.K. Nyerere alifariki mwaka 1999. Takribani miaka 19 tangu Tanzania ishiriki mashindano ya AFCON. Leo ni miaka takriban 34. Pengine Mwalimu amefariki na ndoto nzuri zaidi kuliko Watanzania wengi, amekiona kile ambacho wengi hawatakiona kwa sasa. Na hawana mpango wa kukiona pia. Viongozi hawana maamuzi, wachezaji hawana maamuzi na watanzania hawana maamuzi, sio maamuzi Tu Bali yale ya ndoto sahihi. Mwalimu haliliacha Taifa likiwa mbele Hatua kadhaa kisoka kuliko Ethiopia na Cape Verde, lakini bahati mbaya wajukuu zake watakuja kuliongoza Taifa hili likiwa Hatua kadhaa nyuma ya Tahiti kisoka. Ndio,  usishangae tumebadili Sanaa kuwa soka na soka kuwa Sanaa na Kisha tukaviunganisha na siasa. Ndio maana si ajabu mpaka Leo tunaamini nafasi ya okwi haizibiki Simba, tunaamini Taifa halimuwezi Uganda, na Ndemla hastahili kuwa mbele ya Kwizera. Tumeyafanya mafanikio ya soka kama pepo, hatujui ni lini ila ipo siku yatakuja.

Umepata kumsikia Paul J Meyer, alikuwa mfanyabiashara maarufu aliyefanikiwa na aliyejihusisha na mambo ya kijamii Marekani, aliwahi kusema "Productivity is never an accident. It is always the result of a commitment to excellence, intelligent planning, and focused effort". Alimaanisha Uzalishaji ama mafanikio hayaji kama ajali Bali ni kujitolea ipadavyo, mipango yenye akili na juhudi yakinifu. Angekuwa kiongozi wa soka angesema mafanikio hatuwezi kupata kwa kumleta Maximo amfundishe Maulid au Poulsen amfundishe Ngasa. Maximo alitakiwa amfundishe Ngasa kipindi hiko, Kisha Poulsen angekuja kumtumia Ngasa aliyeiva akiwachanganya na akina Msuva, bahati mbaya wakati Maulid anafundishwa namna ya kuendesha kasi yake na mpira Ngasa alikuwa anafundishwa kuwa mahala sahihi ni yanga au simba. Hata ndoto zake zikawa hapo, akachagua ndoto isiyo sahihi, akafanya maamuzi yasiyostahiki baadae alipoikataa El Merreikh tukamshangaa wakati tulimwandaa wenyewe awe hivi, aipende Yanga kuliko kitu chochote na aitumikie kwa Maisha. Tabia za wachezaji wengi wa sasa wenye vipaji hazina tofauti na zile za Haruna Moshi tulizokuwa tunazipinga bado tumezifumbia macho. Hata sie wapenzi wa mpira hatuna ndoto sahihi, ndoto zetu sahihi huja na kuondoka, bahati mbaya wala hazikai sana. Tunapata Ndoto CAF wakitoa ratiba ya kufuzu zinapotea tukifungwa na Msumbiji wala hatuwazi kama baada ya mwaka na nusu ratiba nyingine itatoka. Tunahamia kwa kulwa na doto ambao wakishatoka Klabu Bingwa tunalaumu Okwi hakuwepo.

Wakati nakua nilikuwa na ndoto ya kumuona nguva. Ndoto nzuri kweli. Ndoto ambayo hata tajiri wa Dunia naamini hatoifumbia macho ikitokea. Mwaka 2012 ilibidi nifute ndoto hiyo baada ya shirika la serikali ya Marekani la National Ocean Service kusema hakuna ushahidi wa kuwepo kwa nguva, nyingi zilizopo ni hisia. Wengi wanatamani hisia hizi ziwe kweli, nikagundua sio ndoto sahihi nikaachana nayo, ya nini kuishi na ndoto ya kuhisi wakati zenye uhalisia zipo. Watanzania tumeamua hili, tunazifanya hisia kuwa ndoto za kweli, hatuamini kama Paul J Meyer, tunaamini kuna shortcut(ufupisho), hatuamini katika juhudi, tunawaandaa Serengeti boys kucheza Azam, na Leo tunaiona Burundi haizuiliki. Tunaketi na kahawa tukisubiri mechi ya watani wa jadi kumuona Okwi, yeye anacheka tunavyompigia magoti na kumwahidi donge nono, Yanga hawana Academy ya maana, Simba Academy chali. Azam wanamfuata Kavumbagu. Ndio hapa tulipo, tunaishi Maisha ya Nguva, hayapo lakini tunahisi yatafanikiwa. Tunaendelea kumfundisha Kiemba soka ili Singano akikua tumshangae kwanini hana Stamina. Nasubiri maamuzi yetu ya sasa kutaka kuandaa AFCON wapi yatatupeleka. Kwa mwenendo huu soka la Tanzania litaendela siku ambayo nitatimiza ndoto yangu ya kupiga picha na Nguva. Namaanisha HAIWEZEKANI.

Ahsateni.
By Nicasius Coutinho Suso

0712203770
nnicasius@outlook.com

1 comment:

  1. Awesome stuff...!! Though it saddens me as Tanzanian that we depend entirely on shortcuts which cant bear fruits. Let's do comparative analysis from developed soccer countries and see how we can apply in our context!

    ReplyDelete

Powered by Blogger.