KUMBE TATIZO LA MPIRA WETU HALIKUWA PESA ( SEHEMU YA 2)
Wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo pesa siyo tatizo la mpira wetu wa Tanzania. Nawashukuru sana wasomaji wangu ambao walinipigia simu au kunitumia ujumbe, wengi wakiniuliza nafikiri tatizo ni nini kama siyo pesa.
Ndugu zangu, mpira wa nchi kama hii ya kwetu unakabiliwa na matatizo katika nyanja karibu zote zinazouhusu. Ukuanza kuzungumzia hayo matatizo utagusa nyanja ya elimu, afya, ardhi, ustawi wa jamaa, na nyingine lukuki.
Vitu vingi vya msingi vinavyohitajika ili kuwa na ustawi katika soka vimetupita mbali sana. Unahitaji kuwa na shule za soka walau kila mkoa ili upate wachezaji wengi wazuri tena wakiwa katika umri sahihi.
Unahitaji ligi za vijana zenye mfumo wa ligi kuu. Yaani hizi timu za ligi kuu ziwe na timu za vijana wa umri mbalimbali ambao watakuwa wakishindana kwa mtindo wa ligi nchi nzima.
Lakini pia unahitaji madaraja yasiyopungua manne ya ligi za kitaifa ambapo timu zitakua zikiwania kupanda katika daraja la juu.
Ukiyafanya hayo yote lazima ulimwengu uitambue soka yako. Utakua na wachezaji wengi sana ambao watawafanya akina Mcha Khamisi kuhangaikia nafasi ya kucheza Ulaya ili wasiumbuke hapa kwenye ligi ya nyumbani.
Mfano mzuri ni yule winga wa zamani wa Taifa Stars, Said Maulid 'SMG'. Mwenyewe anakiri kwamba kilichomfanya azidishe juhudi za kwenda kucheza soka nje ya nchi ni ujio wa Mrisho Ngassa.
Kinachoikwaza soka yetu ni kukosa wanasoka walioiva kiushindani. Tuna wachezaji wa kawaida ambao hawana uwezo wa kutosha kulibeba Taifa hivi sasa hata kama tutawalipa shilingi ngapi.
Natambua kwamba hatuwezi kutengeneza mfumo huo kwa muda fupi. Huo ni mfumo ambao unatumiwa na mataifa makubwa ya Ulaya na wametumia miaka mingi kuutengeneza. Lakini hata kwa mfumo wetu huu tulio nao hatupaswi kusumbuliwa na nchi ndogo kama Burundi.
Mara nyingine ni bora kuwa kichwa cha mbwa kama umeshindwa walau kuwa
mkia wa Simba. Hizi nchi za ukanda wetu wa Afrika Mashariki hazikupaswa kutusumbua kama kweli tungekua tunajipanga vema kwa sababu mazingira yetu yapo sawa sawa na pengine tumewazidi baadhi ya vitu.
Umewahi kujiuliza ni kwa nini wachezaji wa Kitanzania hawaendi kwa wingi kucheza soka katika nchi hizi za Afrika Mashariki kama wao wanavyokuja kwetu kwa wingi?
Moja ya sababu ni kwamba hapa kuna pesa nyingi zaidi ya huko kwao, hivyo wachezaji wa Kitanzania hawavutiki sana kwenda huko na badala yake wachezaji wa Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi ndio tunaowaona hapa.
Naogopa sana ninapoona tuna pesa lakini bado tupo pale pale kama si kurudi nyuma zaidi. Hii inaashiria kwamba tunapaswa kujisahihisha haraka katika namna tunavyouongoza mpira wetu.
Nadhani hatujapata viongozi wenye nia za dhati na uchungu kwa soka la nchi yetu. Viongozi tulionao ni aidha hawana nia za kulipeleka mbele soka letu ama nia zao zimeambatana na mambo haramu katika mpira.
Siasa za Simba na Yanga bado zinaongoza soka letu hadi leo. Tunafika hatua tunasogeza mbele muda wa usajili kwa sababu tu vilabu havijakamilisha mambo kwa wakati. Huu ni udhaifu wa uongozi.
Soka lina misingi yake. Hata kama una pesa kiasi gani, laki ni kama unashindwa kuwadhibiti wachezaji wako wasicheze mechi za mchangani 'ndondo' hufai kua kiongozi wa mpira wa nchi hii kwa sababu tumekwishathibitisha tatizo la mpira wetu siyo pesa.
Unajivunia nini kuwa kiongozi wa soka la nchi ambayo wachezaji wanacheza mechi 26 tu za ushindani kwa msimu? Msumbiji wana sababu gani ya kufungwa na wachezaji wanaocheza mechi 26 kwa msimu? Kwa sababu unawalipa Tsh 50,000?Bahati mbaya mpira hauchezwi hivyo.
Anahitajika kiongozi atakayeisisimua ligi daraja la kwanza kabla hajafikiria kuirejesha ligi daraja la pili. Kiongozi atakayezipa dakika 90 nafasi ziamue na siyoa atakayekaa mezani kuamua timu ipi ipande daraja kati ya Stand UTD na Mwadui.
Hatuhitaji kiongozi mwenye pesa tu, tunahitaji kiongozi atakayetumia pesa zilizopo kwa mambo shihi huku akitumia rasilimali zilizopo kupata pesa nyingine kwa ajili ya klabu, ba hata akiondoka klabu isiyumbe kiuchumi.
Ni aibu na ujinga kujiita timu ya soka kama hata uwanja wa kuchezea soka huna na bado unajulikana kama timu kubwa Afrika.
{ Richard Leonce Chardboy}
Email: chardboy74@gmail.com
facebook; Richard Leonce Chardboy
Twitter: @chardboy77
Simu: 0766399341
No comments