KWAHERI FRANK LAMPARD, KWAHERI SUPER FRANKIE. MIGUU YAKO NA MOYO TUTAIKUMBUKA DAIMA..
Kuna moja ya vitu vya ajabu sana ambavyo Ni ngumu kuvishuhudia, mojawapo Ni Mzaramo kudai kwao ni Kanda ya ziwa, ama Mngoni kusema Ni wa kaskazini mwa Tanzania. Ila kwa Frank Lampard Ni tofauti, Ni mmoja Kati ya bainadamu wachache waliopapenda ugenini kuliko nyumbani, moja Kati ya binadamu wachache waliopigana kwa damu na mateso kupajenga ugenini.
Familia ya Lampard imejaa West Ham, Baba yake Ni moja Kati ya wachezaji walioheshimiwa zaidi pale West Ham, baadae akawa kocha, mjomba wake Harry Redknap kaitumikia West Ham kwa zaidi ya miaka mitano, Lampard mwenyewe kalelewa pale tangu 1995 maana yake karne ya 20 mpaka 2001 karne ya 21, walimlea, wakamkuza wakamfanya bora, mpaka alipoenda Chelsea.
Achana na Ryan Giggs, Steven Gerrard, Xavi Hernandez, John Terry Huyu yupo tofauti, utiifu na kujitolea kwake ni tofauti, wakati hawa wakiwa wamekuzwa kwa maono na mienendo ya vilabu vyao, wakiwa wametumia muda mwingi kujifunza Tamaduni za timu zao, huyu Ni tofauti, huyu alikuja keshakuwa mtu mzima, alikuja akiwa keshapata mpenzi, kwa wachezaji wa kisasa angekuja kuchukua mshahara Tu, angefuata jina Chelsea.
Ulimuona Cesc Fabregas aliamini maisha yake hayakuwa kamili bila kurudi nyumbani, aliamini Emirates sio kwao, Ni vigumu sana, Ni ngumu kupafanya ugenini kwenu, Ni ngumu kuipigania nyumba ya jirani maisha yako yote ya nguvu. Unaweza kumtaja Didier Drogba ila bado hajafikia roho hii.
Bahati Nzuri naye alikuwa na bahati, bahati kubwa, wakati akiamua kuipenda Chelsea na mashabiki wakaamua kumpenda yeye, wakati akiamua kucheza mechi dhidi ya Liverpool akiwa anaomboleza Kifo cha mama yake mashabiki waliita jina la Super Frankie, walilitungia na nyimbo, Ni ngumu kumalizika nyimbo kumi pale Stamford Bridge bila ya nyimbo yenye jina lake kuimbwa, wao wanaamini Ni kiungo bora kabisa kuwahi kuikanyaga Ardhi, wanaamini Ni mchezaji bora kuwahi kuvaa jezi ya blue. Achana na Gianfranco Zola atakumbukwa kwa ubunifu wake, huyu Hata kaburi lake naamini litapakwa rangi ya blue. Mwanajeshi wa West Ham alieamua kuipigania Chelsea. Kafunga magoli zaidi ya 200, ndie anaongoza Chelsea, anawazidi mbali washambuliaji wengi, Ni mtu wa pili nyuma ya Ryan Giggs kwa assists ligi ya Uingereza. Ni kiungo pekee kuwahi kufunga zaidi ya magoli 150.
Moja ya makocha wanaoheshimika na wagumu kutoa sifa kwa wachezaji wa timu pinzani Ni Sir Alex Fergusson, huyu ndiye alieamini kuwa Gerrard hajawahi kuwa wa kiwango cha dunia lakini kwa Lampard alivua kofia. Namtizama Lampard nawatizama mashabiki wa Chelsea, hatutasikia nyimbo ya Super Frankie, hawatoimba moja ya nyimbo wanayoipenda zaidi, wamepunguza Kidole kimoja Kati ya vile kumi walivyonavyo Ni ngumu kupata mbadala.
Sio mashabiki wa Chelsea Tu, Hata wapenzi wa EPL pia, wakati Steven Gerrard akichoshwa na majeraha, wakati Wayne Rooney akiwa chini ya kiwango chake, makipa watapumua, tutapungukiwa na magoli ya Mita 40, tutakosa uhondo wa mashuti speed ya Jet, kidogo Rose Barkley wa Everton anaweza kutupa hiki. Kibaya Ni kwamba wakati Lampard anaondoka, ligi inabakiwa na Cleverley, Ligi inabakiwa na Diaby, mahali ambapo Lampard alipachezea atakavyo kuanzia August atacheza Mikel.
Usishangae jezi yake akavaa Matic. Wakati mwingine inakubidi kutunzwa kwa heshima, Hata kama Lampard huyu sio wa 2005 Mara nyingine mtu unapewa heshima ya uliyoyafanya, Mourinho angeamua hili, Mourinho angemhifadhia dakika 15 kila baada ya mechi tatu, baadae angestaafu kwa mbwembwe pale. Nimekosa sherehe za Lampard kustaafu, ngoja nijaribu kuona kama ntaziona za Wayne Rooney, usiulize kwanini sio Gerrard au Giggs. Nilitamani Hata jezi yake istaafishwe.
KWAHERI FRANK LAMPARD, KWAHERI SUPER FRANKIE. MIGUU YAKO NA MOYO TUTAIKUMBUKA DAIMA.
Ahsanteni. By Nicasius Coutinho Suso (WS)



No comments