KOMBE LA DUNIA 2014 ~ VICENTE DEL BOSQUE ANAPOFELI SOMO LA HESABU..........
Kuna mwanafilosofia mmoja wa china anaitwa Confucius kutoka china aliwahi kusema katika vitabu na nukuu za maneno yake kuwa " Study the past if you would define the future". Alimaanisha inabidi usome yaliyopita kama unataka Kung'amua yajayo. Ulimwengu umeshuhudia moja ya maajabu ambaye hakuna,aliyeyatarajia, hakuna aliyeyafikiria na wala hakuna aliyeyawaza. Spain kafungwa goli tano, Ni ajabu kweli. Kwa haraka haraka Spain ndo timu ya taifa yenye kikosi ghali duniani. Kikosi kikubwa na kipana zaidi.
Hata aliekuwa ndotoni ilikuwa vigumu kuliota ili. Unawazaje timu yenye wachezaji watano kikosi cha kwanza wanaocheza ligi kuu Uholanzi kuifunga bingwa mtetezi na timu inayoongoza ubora duniani kwa goli tano. Kwa wajuzi wa mambo ilikuwa rahisi kutabiri ugumu wa mambo kwa Spain kwa wakati huu, Ila sio kwa kiasi hiki hapa.
Kwa haraka haraka kikosi hiki cha Spain kimecheza mashindano makubwa yote tangu Mwaka 2008 mpaka Leo, asilimia 60 ya kikosi kilichukua Euro chini ya marehemu Luis Aragones, asilimia 80 kilichukua ubingwa wa Dunia na Kutetea wa Ulaya. Hakina mabadiliko tena, style Ni ile ile wakati nguvu ikishuka, ukimuondoa Busquet kiungo cha Spain kina watu wa umri wa miaka 30, wanachoka, hawana pumzi ya Duma ya duma tena, hawana nguvu ya faru tena, Ni rahisi sana kuwashinda Spain kwa sasa.
Ukiwa na uwezo wa walau kumiliku asilimia 40 ya mpira fanya mambo makubwa mawili, Kaba Vyema Kisha kimbia vyema. Ukiweza hivi vitu umeshinda. Bahati mbaya Del Bosque anaathiriwa na kutokujua Philosophy za Confucius, hakusoma yaliyopita ili kung'amua yajayo, wakati Candreva na Christian Maggio wakitaka kuwatoa nyongo mabeki wake katika kombe la mabara dhidi ya Italy bado aliona Ni bahati mbaya, usingemlaumu sana, alikuwa hajashuhudia manyanyaso muda mrefu, lakini fainali ya Brazil ilikuwa ya kujifunzia.
Gustavo na Paulinho waliiteketeza kiungo yake, speed za Neymar, Oscar na Hulk ziliwanyonga mabeki zake, ulikuwa wakati wa kutizama katika mfuko Kuna chenji kiasi gani ya kukurudisha dukani, ulikuwa wakati wa kujua namna gani unamuandaa Martinez badala ya Pique, ulikuwa wakati wa kujua nani atakaa kwa Xavi kama Koke au Alcantara. Ulifika wakati wa kuiamini mikono ya David De Gea. Ulijiri wakati wa kujua aina engine za kumlinda Iniesta.
Nilikuwa natizama ubora wa Iniesta, Ni bora kweli kweli, hukosei ukisema ndo miguu bora iliyobaki katikati mwa uwanja katika kizazi hiki, lakini alikosa wapi apeleke mpira kwa ufasaha, wakati akikabwa kwa nguvu alikosa msaada, nikatizama mabadiliko anatoka Diego Costa anaingia Torres, nikajiuliza kwanini asingekuwa Negredo ama Lorrente? Katika benchi nikamwona Koke, Javi Martinez. Viungo bora kabisa.
Ya nini kuwang'ang'ania wakongwe wengi, hakuna anayeweza kupinga ubora wa Busquet haswa katika tik taka lakini ametumika sana, ametumika katika umri mdogo kumtegemea peke yake kuzuia viungo wakorofi Ni ngumu, alitakiwa awe na Martinez. Mwisho wa siku kila timu itajua sana kucheza na Spain, Hata ndugu zangu Uingereza nao wanaweza kuonekana bora sana, unaweka wakabaji na wakimbiaji Kisha unacheza na Spain.
Tatizo kubwa la Barcelona limehamishiwa Spain. Usishangae mechi ijayo Del Bosque ndo akagundua hili, usishangae ndo akawaanzisha hawa, ila atakuwa anawapa mzigo mkubwa wa kutengua matokeo Haya. Na kama akibaki vile vile watu wanakaba na kukimbia basi. Kwa sasa ukiwa unacheza na Spain unawahitaji zaidi Bale, Neymar, Walcot, Muller kuliko Wilshere, Gotze, Sneijder. Unahitaji mbio na nguvu kuliko ufundi.
Nilikuwa namtizama Nikola Rizzoli refa wa Italy alochezesha mechi, Hata yeye alionekana kumaliza mpira huku akiwa na mshangao, aliking'uta nywele zake kwa mshangao, Sura ya Del Bosque yenyewe ilikuwa na mshangao, Hata Van Gaal alishangilia kwa mshangao, wachezaji wa pande zote walifurahi na kuumia kwa mshangao kwa wakati mmoja. Kikubwa Hata mashabiki wote walibaki na mshangao.
Naamini kama Rais wa 32 wa Marekani Franklyn De Roosevelt angekuwapo Leo angemshauri Del Bosque kuwa " We may not be able to prepare the future for our children, but we can at least prepare our children for the future" maanake tunaweza kushindwa kuandaa yale yajayo kwa watoto wetu lakini walau tuandae watoto wetu kwa yajayo. Hii ndo dhambi inayomtafuna Bosque, anaogopa kumwanzisha Koke, anahofia kumweka Martinez, na ndo maana hakumwita Negredo. Kuna mwalimu wangu aliwahi,kusema ukiijua hesabu vyema basi Ni rahisi kutabiri ama kufanya maamuzi katika wakati sahihi. Pole Del Bosque inawezekana kweli somo la hesabu lipo kushoto kwako. Lakini muda bado unao.
AHSANTENI.
...... Imeandaliwa na Nicasius Coutinho Suso
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++



No comments