VPL ~ JE MASHABIKI YANGA KUISHANGILIA SIMBA LEO?
Katika dimba la Uwanja wa Taifa leo litapigwa pambano kali la ligi kuu Tanzania bara kati ya Azam FC timu ambayo inakamata nafasi ya kwanza kumenyana na Simba SC wanaokamata nafasi ya 4 katika msimao wa Ligi.
Kikubwa kinachosubiriwa katika pambano la leo kati ya Azam FC na Simba SC ni kuona kama Mashabiki wa Yanga wataishangilia Simba ili ishinde kwani kama Azam atafungwa na Yanga kushinda leo itawarahisishia Yanga kuongeza nguvu katika kuwania kombe kwani wako nyuma ya Azam kwa pointi 4 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Azam Inaingia uwanjani leo kupambana na Simba ikiwa haijapoteza mchezo wowote msimu huu kwani imecheza mechi 21 ikishinda mechi 13 imetoka sare mara 8 haijafungwa mchezo wowte mpaka sasa huku ikiwa imeshafunga magoli 41 ikiruhusu wavu wake kuguswa mara 13 ina pointi 47 katika nafasi ya kwanza.
Azam Fc watataka kuifikia rekodi ya Simba SC kwa kumaliza ligi bila kufungwa hivyo kuongeza ugumu katika mechi ya leo. Simba wao wanakamata nafasi ya 4 wakiwa wameshacheza mechi 22 msimu huu wakishinda 9 wametoka sare mara 9 na kufungwa mara 4 huku wakifunga mabao 38 na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara 22 ina pointi 36 huku ikiwa imepitwa pointi 11 na Azam Fc inayoongoza ligi hiyo.
Mechi nyingize za Ligi hiyo zitaishuhudia Yanga Sc ambao ni mabingwa watetezi wakisafiri kuikabili Mgambo JKT katika uwanja wa Mkwakwani mechi ambayo Yanga wanausaka ubingwa wakati Mgambo wao wanajinusuru kushuka daraja.
Mtibwa Sugar wako nyumbani wakiikabili Coastal Union wakati pale Chamazi JKT Ruvu wataialika Rhino ya Tabora. Kule Kagera wenyeji Kagera Sugar wataialika Ruvu shooting katika dimba la Kaitaba.
Mechi nyingine kubwa leo ni katika Jiji la Mbeya ambapo kutakua na Mbeya Dabi ambapo Mbeya City wataumana na Prisons katika mchezo utakaopigwa katika dimba la Sokoine.
Mbeya City inakamata nafasi ya 3 ikiwa na pointi 42 huku prisons wao wakiwa katika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 22.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments