LIGI YA MABINGWA ULAYA ~ HAKUNA JIPYA KWA MAN CITY WAUNGANA NA ARSENAL KUSUBIRI MSIMU UJAO


Hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa ulaya iliendelea usiku wa kuamkia leo kwa mechi mbili kupigwa katika miji ya Barcelona Hispania na Paris Ufaransa.
Manchester City wakisafiri kuifata Barcelona walijikuta wakiambulia kichapo cha bao 2-1 hivyo kutolewa kwa jumla ya goli 4-1 baada ya mechi ya awali kulambishwa 2-0 katika uwanja wa Etihad jijini Manchester mwezi uliopita.

Man City waliokua uwanjani bila kocha wao Manuel Pellegrin ambaye alikua jukwaani kama mtazamaji baada ya kufungiwa mechi mbili kulalamika kama mwamuzi aliwaonea walikua wakihitaji ushindi wa 3-0 kuvuka hatua hii.

Lionell Messi alitangulia kufunga dakika ya 67 baada ya makosa ya beki wa City Jeon Lescot kushindwa kuokoa mpira katika eneo la hatari.
City walirudisha kupitia kwa nahodha wake Vicent Kompany dakika ya 87 kabla ya Dani Alves kupigilia msumari wa mwisho kwa kufunga goli la pili dakika za lala salama kama alivyofanya katika mechi ya Awali pale Etihad.

Kwa matokeo hayo Barcelona imetinga hatua ya Robo Fainali kwa jumla ya goli 4-1.
Katika mechi nyingine iliyopigwa katika jiji la Paris Ufaransa, Bayer Leverkusen waliopaswa kushinda bao 5-0 dhidi ya PSG walijikuta wakilambishwa mchanga baada ya kukubali kichapo cha bao 2-1 na kujikuta ikiaga mashindano hayo kwa kichapo cha jumla cha goli 6-1 baada ya mechi ya awali kupoteza nyumbani kwa kufungwa 4-0.

Bayer walitangulia kufunga kupitia kwa Sidney Sam dakika ya 6 kabla ya Maquinous kusawazisha kwa upande wa PSG.
Ezequel Lavezzi alifunga goli la ushindi kwa PSG dakika ya 53.
Ligi hiyo itaendelea tena wiki ijayo kupata timu zingine nne zitakazoungana na Atletico Madrid,Barcelona,PSG na Bayern Munich katika hatua ya Robo Fainali.

+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments

Powered by Blogger.