ARSENE WENGER ~ MSEMINARI WA KALE ANAYEHUBIRI INJILI KWENYE SOKA
Katika maisha
yangu sijawahi ona watu wenye imani kali kama wahubiri wa dini, Mapadri
,masheikh na wachungaji hawa watu wana imani kali sana na dini zao. Imani zao
zimejengwa kwa kusoma na kusikia mafundisho ya vitabu vitakatifu.
Vitabu
Vitakatifu Vinatuambia “Imani huja kwa kusikia ,tena kwa kusikia neno la Mungu”
na Ili Shekh uitwe Shekh lazima uwe una Imani thabiti ya dini ya kiislamu
ilojengwa kwa misingi ya kurani. Na mchungaji vivyo hivyo,Lazima awe amejazwa
neno la Imani kupitia misingi thabiti ya biblia.
Lakini hakuna
shekh aliekua shekh bila kupitia Mafundisho thabiti ya Dini ya kiislam,na ili
uwe padre lazima upitie Seminari. Achana na Seminari magamaga za siku hizi Kila
mtu akijenga shule anaiita seminari. Matokeo yake wanatuzalishia
"magigisi" na "magobo"
Seminari
zilikua zamani bwana,Mtu akitoka seminari hata bila kukwambia utamjua tu. Tabia
hata hekima yake itaongea tu. Wachungaji na Mapadre waliosoma seminari za Kale
walifundwa wakafundika, walikanywa wakakanyika. Hawa watu ni ngumu
kuwatenganisha mbali na imani zao.
Hawa watu
huwezi kuwabadilisha kwenye kile wanachokiamini. Mchungaji na
padre walishafundishwa,wakasikia pia wakasoma kua Isaka ni mzaliwa wa kwanza
halali wa Ibrahim.Hasilani huwezi kumbadilisha na kumwambia Ismail ndie mzaliwa
wa kwanza halali wa Ibrahim.
Kesha
ukeshavyo, Huubiri uhubirivyo hawezi kubadili msimamo wa watu hao watu asilani.
Mpige mawe kama Stephano, muwekee kisu shingoni bado atachukua mbundugo na
kuendelea na Imani yake. Mchungaji anaamini akimuombea kiwete atatembea
tena,akimuombea kipofu ataona tena,kiziwi pia atasikia tena.Muda mwingine
kipofu huwa aamini kua siku moja akiombewa ataona,ila mchungaji ana imani
asilimia zote kua kipofu lazima atapokea uponyaji.
Hata akimuombea
mara ya kwanza kipofu asione ila bado atakua na imani ipo siku kipofu huyo
ataona tena kwakua alishawai ombea vipofu wengine wakaona tena. Huo ndo ujasiri
wa mchungaji,hiyo ndo imani ya mchungaji.
October 22, Mwaka 1949 mjini Strasbourg alizaliwa
muinjilisti wa soka, Mwenye imani kali kama Ibrahim.Huyu ni mtoto wa mzee
Alphonce,aliyekua mfanya biashara maarufu wa vipuri mjini Strasbourg.Alitumia
muda mwingi kuangalia mpira akiwa bar.Hakika soka ilikua ndani ya damu
yake.Alitumia mbinu alizoziona bar na kuziamishia kwenye timu yake ya kijiji.
Tangu kijana alipenda kazi ya ukocha kuliko kucheza
mpira.Mda mwingi alikua akipanga kikosi kwenye timu yake ya kijiji amayo baba
yake alikua akifundisha.Maisha yake ya soka kama mchezaji yalianzia kwenye timu
ya kijiji cha Duttlenheim,kijiji ambacho alikulia mseminari huyu.
Hakuna aliyemjua muinjilisti huyu kwenye maisha yake
ya uchezaji. Alitundika daruga akiwa na timu ya RC Strasbourg na kufungua
ukurasa mpya katika ngazi ya ukocha. Maisha yake kama kocha yalianza mwaka 1981
mara alipohitimu shahada yake ya biashara na kukabidhiwa mikoba kama kocha wa
timu ya vijana katika timu ya RC Strasbourg. Mwaka 1983 akateuliwa kua kocha wa
vijana wa timu ya cannes kabla ya kutimkia katika klabu ya Nancy Lorraine mwaka
mmoja baadae,mwaka 1987 klabu ya Nancy ikashuka daraja.
Wengi walifikiri huo ndo utakua mwisho wa mseminari
huyu katika maisha yake kama kocha La hasha huo ndo ulikua mwanzo wa nyota yake
kuangaza. Mnamo mwaka 1987 klabu ya Monaco ikampa ajira ya kua kocha wa timu
hiyo,uteuzi huo ulileta maswali mengi sana,hakuna aliyeamini klabu kubwa kama
Monaco itamteua kocha alioyeishusha timu daraja.”Hakika huyu ni mwana wa
Mungu”,ni mmoja wa watu wenye bahati katika sayari yetu. Msimu wake wa kwanza
akiwa na Monaco akaiwezesha klabu hiyo kuwa bingwa wa ligi kuu ya ufaransa,pia
mwaka 1991 aliiwezesha Monaco kua bingwa wa kombe la ufaransa.
Katika kipindi chake kama kocha wa Monaco alipata
kuwasajili wachezaji kama Glenn Hoddle na George Weah ambae baadhi ya watu
walikejeli usajili wake lakini mwamba huyo wa Afrika miaka kadhaa mbele
ukaibuka kua mchezaji pekee bora duniani kuwahi kutokea kwenye Dunia yetu ya
tatu.
Huo ndo ujasiri wa mseminari huyu ulipoanzia. Mwaka
1994 alishindwa kukubaliana na uongozi kuhusu mkataba wake na klabu ya Monaco.
Kumbuka klabu ya Monaco ilimzuia kwenda kufundisha katika klabu ya Bayern
Munich mwaka huo huo. Huo ndo ulikua mwisho wake wa huduma kama kocha kwa klabu
ya Monaco na Ufaransa kwa ujumla. Ailitimkia kwenye klabu ya Nagoya Grampus
kabla ya kupigiwa pande na rafiki yake David Dein kuinoa klabu ya Arsenal mwaka
1996. Timu zote alizofundisha awali zilikua shule hapa ndipo alipoanza rasmi
kazi yake ya uinjilisti.
Utamwambia nini huyu mtu akuelewe wakati washabiki wa
Arsenal hawakumuelewa alipotumia pesa kumnunua Dennis Bergkamp. Wengi
walilalamika pesa zilizotumiwa kumnunua mdachi huyo. Ni yeye pekee aliyeamini
Begkamp ana thamani hiyo. Baadae kidogo Bergkamp akawaonesha mashabiki kuwa
Wenger alikua sahihi kuliko wao.
Unamkumbuka Nikolas Anelka? Wakati anasajiliwa kinda
huyu kila mtu alimnyooshea kidole. Magazeti yote yakamuadaa na kuona kama
amefanya kituko cha usajili, Ila mzee huyu na imani kama ya Abrahamu akamuamini
Anelka vivyo hivyo Anelka nae akampa kocha wake kile alichokiona kutoka kwake.
Mashabiki na wadau wakabaki midomo wazi,huku vyombo vya habari vikiwa vimepigwa
bao la pili na mfaransa huyu.
Robbin van Persie aliandamwa na majeruhi,mashabiki
wengi sana walipendekeza auzwe hasa pale Juventus walipotuma ofa. Lakini
muinjilisti huyu akamkumbatia kilema wake huku akiamini ipo siku kilema wake
atatembea tena. Aliamini ipo siku RVP atakua gumzo katika ligi ya uingereza na
ndivyo ilivyotokea ,washabiki walotaka auzwe wakasahau wakaanza kumshangilia.
Aaron ramsey,huyu mpiganaji wa kiingereza, wenyewe
humuita Rambow, ni mchezaji bora wa arsenal mwaka 2013,licha ya kupata majeruhi
bado anatarajiwa kua mchezaji bora wa arsenal mwaka 2014. Huyu ni muingereza
haswa,hujitoa asilimia mia ndani ya uwanja,hutoa kila kitu kwa ajili ya timu
yake. Kila mshabiki wa arsenal anampenda Rambow,ila bila imani ya kocha wake
huyu Ramsey asingekuwa mchezaji wa arsenal kwa sasa.
Huyu mtoto wa mzee Aliphonce ana imani kama ya David
Oyedepo,aliamin ipo siku Ramsey atakua nyota.Lakini mashabiki wa arsenal
waliona ramsey ni kama mgonjwa wa ukimwi,hawakuamini kama atapona siku moja.Ni
yeye tu aliyemuamini
Lakini Huyu mzee wetu kuna mambo matatu ameamua
kuyafumbia macho.Hayo ndo yalioifanya arsenal ikose ubingwa kwa miaka nane na
huu unaenda mwaka wa tisa bado anafanya makosa yale yale yatakayomfanya atoke
kappa tena.
Kosa la kwanza ni kufumbia macho nguvu ya pesa ya
Chelsea na Manchester City. Bado anaiishi jana yake leo,Anaamini soka la karne
ya 20 ni sawa na soka la karne hii. Katika utawala wake alikua akishindana na
Manchester U nited pekee.Manchester United ikiteleza Arsenal ilikua haifanyi
makosa.
Tangu utawala wa Chelsea na Man City uanze Arsenal
wametwaa taji moja tu. Arsenal ya sasa inahitaji kutumia mabavu ya pesa ili
kushindana na Chelsea na Manchester City. Huwezi kuchukua kombe wakati
unawategemea Sanogo na Giroud na huku mwenzako ana Dzeko na Jovetic katika
benchi la wachezaji wa akiba.
Pili ni Kuendelea kukumbatia wachezaji wasiompa
matokeo.Tunajua kama wewe ni baba wa imani kwenye soka ila kwanini usijifunze
kwa yaliyokupata awali. Richard Wright, Denilson,Andre Santos,Francis
Jeffers,Igors Stepanovs,Sebastian Squillaci hawa ni miongoni wa wachezaji
mizigo aliowaamini na kuwapa nafasi. Licha ya kuwaamini na kuwang'ang'ania bado
hawakumpa matokeo,mwisho wa siku wachezaji hao wakaitia hasara klabu.Ila bado
hajakoma tu,bado anaamini kwa Giroud. Akimuangalia Giroud anamuona Henry ndani
yake,imani yake ndio inamuongoza hivo.
Kosa lake kubwa na la mwisho kushindwa kufanya
mabadiliko na marekebisho kwa kila sekta katika timu kwa msimu.Kuna msimu
Arsenal inakua na beki nzuri na viungo wazuri lakini inakosa mmaliziaji
mzuri(mfano msimu huu),kuna msimu inakua na beki mbovu ila wanapata viungo
wazuri na washambuliaji wazuri,pia kuna msimu wanakua na beki imara na
washambuliaji maridadi lakini viungo wanarega.Wakati akiendelea kumsubiri RVP
Cesc Fabregas alikua akiibeba timu licha ya kuongozwa na safu nyepesi ya
ushambuliaji iliyokua ikiongozwa na Adebayor.Mungu si Athuman Robbin van Persie
akarejea lakini msimu unaofuata tangu Rvp arejee akamuuza Cesc Fabregas.
Kiungo cha Arsenal kikalega,Akaanza kumuamini Ramsey
huku Thomas Rocisky akirejea taratibu kuziba pengo la Fabregas kipindi hicho
Rvp anaibeba timu, Lakini msimu unaofuata akamuuza RVP ambaye alikua mmoja wa
washambuliaji hatari Duniani na kumnunua Olivier Giroud kama mbadala wake,mpaka
wa leo Giroud viatu vya RVP havimtoshi.
Pata picha Arsenal ya leo ingekua na RVP na Samir
Nasri,ungekua unahitaji nini kwenye Dunia ya soka.Arsenal ilikua inahitaji mtu
kama suarez ili avae viatu vya RVP, keshokutwa atatafuta mshambuliaji mkali
huku akisahau Rocisky na Cazorla umri unawatupa mkono. Huyu kila msimu anakomaa
kuimarisha sekta moja au mbili tu.Kwake siku zinaganda,miaka haiendi.Huyu ndie
Baba wa imani,mimi napenda kumuita muinjilisti,Huyu ndie ARSENE WENGER,mwenye
roho ya kiseminari,imani ya kichungaji, hua akubali kupingwa kutoka kwenye kile
anachokiamini, hua apangi kushindwa, ila anashindwa kupanga.
By Kaijage jr
Middle ya juu




No comments