OKWI NI HALALI HARAMU YANGA



Sakata la Mshambuliaji machachari wa klabu ya Yanga ya Tanzania, Emmanuel Okwi raia wa Uganda linazidi kuteka vinywa na masikio ya wapenzi wa soka hapa nchini hasa kwa siku za hivi karibun.

Kimsingi sakata hili lilipaswa kuanza siku nyingi, lakini limeshika kasi zaidi baada ya mwanandingga huyo kutia saini kandarasi ya miaka miwili na nusu na Mabingwa wa Tanzania bara, Dar es Salaam Young Africans maarufu kama Yanga.

Okwi anakumbukwa kwamba aling'ara sana akiwa na klabu ya Simba ya Tanzania ambao ni wapinzani wa jadi wa Yanga.

CHIMBUKO LA UTATA.
Utata juu ya Okwi ulianza tangu mwaka 2012 alipokwenda nchini Austria kwa majaribio. Hakuna aliyeamini kwamba Okwi anaweza kushindwa majaribio katika nchi kama Austria.

Lakini mwisho wa siku alirudi Simba kwa sababu ambazo mpaka leo hazijulikani.Wapo waliosema hakufuzu vipimo vya afya vya timu timu hiyo, lakini wapo waliofika mbali kwa kusema Okwi hakuwenda Austria wala nchi yoyote kwa majaribio, bali alikuwa nchini kwao Uganda.

UTATA MPYA
Januari 2013, klabu ya Simba ilifanikiwa kumuuza Okwi kwa dau la zaidiya milioni 400 za kitanzania kwenda klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Okwi akaenda huko lakini mpaka ninapoandika makala haya, klabu hiyo haijailipa Simba hata shilingi moja kama malipo ya manunuzi ya mshambuliaji huyo.

Pamoja na hilo, viongozi wa Simba kwa imani waliyokuwa nayo kwa Etoile Du Sahel, wakakubali kusaini TMS na kumruhusu Okwi kuitumikia klabu yake mpya.

UGOMVI WA OKWI NA ETOILE DU SAHEL.
Mambo hayakwend vizuri kwa Okwi katika klabu yake mpya. Kwa madai yake ni kwamba alikuwa halipwi mshahara na klabu hiyo na alikuwa akibaguliwa kutokana na kutokuwa mzawa katika taifa la Tunisia.

Hatimaye Okwi akatumia fursa ya ruhusa aliyoipata ya kwenda Uganda kuitumikia timu yake ya Taifa, kuikacha timu hiyo ya Tunisia na hajarudi mpaka leo hii.

Kwa kumtumia meneja na mwanasheria wake Edger Agaba, Okwi akaandika barua FIFA kuishitaki Etoile kwa kutomlipa mshahara wake.

Agaba kwa taaluma ya sheria aliyonayo, akashirikiana na viongozi wa juu wa shirikisho la mpira wa miguu la Uganda, FUFA wakampigania Okwi ili apate kibali cha kujiunga na klabu nyingine ili asiue kiwango chake na dhumuni kubwa lilikuwa ni kumtumia katika michuano ya kombe
la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, CHAN.

FIFA wkamruhusu Okwi kujiunga na timu nyingine wakati suala lake na Etoile likishughulikiwa.

Kwa kuwa meneja wa Okwi ni mmoja kati ya watu wa karibu wa Villa, Okwi akajiunga na timu hiyo ya jijini Kampala.

JINA LAKE LAKATALIWA CHAN.
FUFA walipopeleka jina la Okwi kwa Shirikisho la mpira la Africa, CAF kwa ajili ya michuano ya CHAN, CAF wakalizuia kushiriki michuano hiyo kwa madai ya kwamba Okwi ni mchezaji wa Etoile ya Tunisia na yupo Villa kwa mkopo tu hivyo hakidhi vigezo vya kushiriki michuano hiyo.

OKWI ATUA YANGA.
Desemba 2013, Yanga wakatangaza kumsajili Okwi kutoka Sports Club Villa ya Uganda. Usajili huo ukazua utata uliopelekea TFF kusitisha usajili wake na kuomba ufafanuzi FIFA kuhusu uhalali wa usajili wa mchezaji huyo.

MAJIBU YA FIFA UTATA MTUPU.
Majibu ya FIFA ni kwamba, wao wanatambua madai ya Simba kwa Etoile, na wanatambua pia madai ya Okwi kwa Etoile na wao ndio waliomuidhinisha Okwi kucheza timu nyingine wakati suala lake likishughulukiwa. Madai
yote yatabaki kama yalivyo mpaka wao watakapotoa ufafanuzi, lakini hayo hayamzuii mchezaji kucheza timu yoyote itakayofuata taratibu za usajili wake.

MASWALI TATA.
Okwi anamilikiwa na nani?

Yanga wamefuata taratibu za usajili kwa kutoihusisha Etoile kwenye usajili wa Okwi?

Etoile wanadai Okwi ni mchezaji wao. Kwa sheria za mikataba ya wachezaji kuhusu malipo zinasema usipomlipa mchezaji mshahara unakuwa umevunja mkataba.


Je inawezakana mkataba wa Okwi na Etoile ulivunjika baada ya Etoile kushindwa kumlipa?

Kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini CAF walimzuia Okwi kushiriki michuano ya Chan?

Unawawekaje Etoile katika nafasi ya kummiliki Okwi kama ni kweli hawajalipa chochote kwa Simba wala hawajamlipa wala kumtumia Okwi?

Hayo ni baadhi ya maswali ambayo hata Okwi mwenyewe hana majibu yake kwa sababu hata yeye anakiri kwamba suala hilo bado lipo FIFA na halijatolewa maamuzi.

Ugumu wa suala hili ni kwamba inahitajika subira. Subira ni ngumu sana katika hili ukizingatia kwamba FIFA hawajalitolea maamuzi kwa mwezi wa nane sasa na haionekani kama watalitolea maamuzi hivi karibuni.

Kwa hali hiyo ni kama kuiweka Yanga na Okwi mwenyewe mtegoni kwani tayari wameingia mkataba na bila shaka Okwi analipwa kwa kazi ambayo haifanyi.

Endapo yanga wataamua kumtumia Okwi, kisha maamuzi ya FIFA yakaja
kwenda tofauti, itakuwa ni hasara kubwa kwa klabu.

Lakini pia watakapoacha kumtumia kisha FIFA wakasema hakukuwa na tatizo, Yanga watakuwa na hasara pia kwa kushindwa kuitumia silaha yao halali.

Najua kuwa Yanga watamtumia Okwi na hii imeongezwa nguvu zaidi na taarifa zilizotoka hivi karibuni  kama CAF wamemruhusu Okwi kuichezea Yanga kuanzia mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mabingwa wa Afrika Al-Ahly.
Je ni kweli kwamba swala la Okwi limeisha na hata kama Yanga watashinda kesho hakuna atakayekata Rufaa ili Yanga ipokwe pointi?
Sisi Mashabiki wajibu wetu ni kuishangilia Yanga haijalishi nani atacheza kesho kwakua Okwi ameruhusiwa na CAF hakuna haja ya kutopangwa.

...... Imeandaliwa na Richard Leonce (Chadboy) toka Wapenda Soka group katika Facebook na Whatsapp.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments

Powered by Blogger.