LIGI YA MABINGWA ULAYA ~ HAKUNA KAMA REAL MADRID HATUA HII YASHINDA 6 UGENINI. HUKU CHELSEA IKIBANWA



Raundi ya kwanza ya Hatua ya 16 bora ya ligi ya Mabingwa Barani Ulaya imeendelea usiku wa kuamkia leo ikishuhudia Real Madrid wakitoa kipigo cha hatari cha bao 6-1 ugenini dhidi ya Schalke 04 inayoshiriki Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga.

Mchezaji bora kabisa wa dunia kwa sasa Cristiano Ronaldo alifunga goli 2 huku Karim Benzema naye akifunga bao 2 na Mchezaji ghali kabisa duniani Gareth Bale akifunga bao 2 pia.

Real Madrid ikiwa katika kiwango bora kabisa ndiyo timu pekee iliyoshinda magoli mengi katika hatua hii ikifatiwa na PSG ambao nao waliweza kushinda 4-1 wiki iliyopita wakiifunga Bayer Leverkusen ambayo nayo inashiriki ligi kuu Ujerumani.

Real Madrid walianza mchezo kwa kasi kubwa na kupata bao la kwanza dakika ya 13 likifungwa na Benzema kisha Gareth Bale akifunga bao safi akiwa katikati ya msitu wa mabeki wa Schalke dakika ya 21. Mpaka mapumziko Real Madrid wakiongoza kwa bao 2-0.

Kipindi cha pili ndicho kilileta dhahama baada ya Ronaldo kufunga goli la tatu dakika ya 52 kabla ya Benzema kurudi tena golini na kufunga goli la 4 dakika 5 baadae. Gareth Bale akafunga goli lake la pili dakika ya 69 likiwa ni goli la 5 kwa Madrid kabla ya Ronaldo hajamaliza karamu ya magoli kwa kufunga goli la 6 dakika ya 89.

Klas Huntelaar alifunga goli la kufutia machozi katika muda wa lala salama hivyo kufanya matokeo ya mwisho 6-1 na kuifanya Schalke 04 kutakiwa kufunga goli 7-0 katika mechi itakayopigwa Spain mwezi ujao kama itataka kusonga mbele.

CHELSEA YABANWA 1-1 NA GALATASARAY

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo ilishuhudiwa Chelsea wakitoka 1-1 ugenini dhidi ya Galatasaray licha ya kutangulia kufunga goli la Mapema kupitia kwa Fernando Torres dakika ya 9 tu kabla ya Aurelien Chedjou hajasawazisha dakika ya 65 katika mchezo uliopigwa huko Uturuki.


+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments

Powered by Blogger.