BAADA YA MAUAJI YA YANGA JANA HUKU MBEYA CITY WAKILIA SASA LEO NI ZAMU YA SIMBA NA AZAM FC



Kipigo kikubwa kuwahi kutokea katika Ligi kuu Tangu Vodacom waanze kudhamini ligi hii kilishuhudiwa jana ambapo bingwa mtetezi Yanga waliifumua Ruvu Shooting "wiki" yani goli 7-0. Lakini bahati mbaya ikawa kwa Mbeya City ambao wamepanda ligi kuu msimu huu na kuleta upinzani mkali katika ligi kwani walikubali kipigo cha bao 2-0 toka kwa wagosi wa Kaya Coastal Union katika mchezo uliopigwa katika jiji la Tanga uwanja wa Mkwakwani.

Kagera Sugar wakiwa Nyumbani Kaitaba waliilambisha Rhino bao 1-0 wakati Mtibwa Sugar wao waliwafunga Ashanti ya Ilala 2-1 katika mchezo uliopigwa Manungu.
Mgambo JKT wakisafiri mpaka Arusha waliwafunga wenyeji JKT OLjoro 2-1

Leo ligi hiyo itaendelea ambapo timu zilizoanza vyema mzunguko huu wa Pili zitakapokutana katika uwanja wa Chamazi ulioko Mbagala Jijini Dar Es Salaam hapo tutashuhudia Azam FC ambao hawajafungwa msimu huu wakiikaribisha Tanzania Prisons ambayo nayo haijafungwa tangu kuanza kwa mzunguko wa pili.

Prisons inaingia katika mchezo wa leo ikiwa imetoka kuwafunga Ruvu JKT bao 6-0 katika mchezo uliopigwa katikati ya wiki huko Mbeya Magharibi wa Tanzania wakati Azam FC wao watakua na machungu ya kutolewa katika hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Feraviario ya Beirra Msumbiji huku ikiwa na matokeo ya bao 4-0 katika mchezo wao wa mwisho katika Ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Azam Fc Inakamata nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza michezo 16 ikishinda 10 na kutoa sare michezo 6 huku ikiwa haijafungwa mpaka sasa wakati Prisons wao wameshacheza mechi 16 wakishinda mechi 3 tu, wakitoka sare mechi 7 na kufungwa mechi 6 na wanakamata nafasi ya 11 katika msimamo baada ya kupata pointi 16 mpaka sasa.

Mchezo mwingine leo utakua kati ya Simba SC watakaoialika JKT Ruvu katika uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam.
Timu zote hizo zilikua Mbeya katika mechi zao zilizopita Ambapo Simba ililazimishwa Sare ya 1-1 na Mbeya City wakati JKT Ruvu walibamizwa bao 6-0 na Prisons.

Simba inaingia katika mchezo wa leo Ikiwa katika nafasi ya 4 katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 18 Ikishinda 8 ikitoka sare mara 8 na kufungwa mechi 2 mpaka sasa ikiwa na pointi 32 pointi 3 nyuma ya Mbeya City wanaokamata nafasi ya 3.

Jkt Ruvu wao wako katika nafasi ya 9 wakiwa wameshacheza mechi 17 wakishinda 6 na kutoka sare mara 1 lakini wamefungwa mara 10  na wana pointi 19.



By Edo Daniel Chibo
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

No comments

Powered by Blogger.