THE GUNNING MACHINE ~ ARSENAL TUMETIKISWA, UDHAIFU WETU UMEONEKANA.
Jioni ya tarehe 1/3/1995 katika hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikua hai. Alikua akiongea na klabu ya waandishi wa habari.
Katika mazungumzo yake, Mwalimu alisema, "Nchi yetu ni imara sana, lakini haijatikiswa. Haijapata misukosuko ya kuthibitisha ni imara kiasi gani.
Ili nyumba ionekane imara, inapaswa kupigwa na dhoruba na vimbunga, kama itabaki ikiwa wima basi tunasema nyumba hiyo ni imara."
Haya maneno ya Nyerere bado yanaishi mpaka leo hii, siyo kwenye nchi tu, hata kwenye soka.
Mpaka ninapoandika makala haya, Arsenal wamefungwa na timu sita katika msimu wa soka 2013/14. Timu hizo ni Aston Villa, Chelsea, Manchester United, Borussia Dortmund, Napoli na Manchester City.
Ukizitazama timu hizi zote, ni Aston Villa pekee ndiyo timu inayoweza kukushangaza kwa kuifunga Arsenal msimu huu. Huwezi kuiweka Aston Villa kwenye kundi la Manchester United na Chelsea au Napoli.
Kimahesabu, 83% ya timu zilizoifunga Arsenal msimu huu ni za daraja la juu katika soka.
Hii inamaanisha nini?
Katika timu bora, Arsenal bado ni timu ya katikati. Ina ugonjwa unaoipata Taifa Stars wa kukosa consistence kwenye michezo mikubwa.
Usiku wa Februari 15, 2012 Arsenal walipokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa AC Milan katika uwanja wa San Ciro.
Wiki mbili baadae, Arsenal hiyo hiyo ikampiga Milan 3-0 nyumbani Emirates. Hali kama hiyo imejitokeza mara kwa mara kwa timu nyingine. Kumbuka kilichotokea mapema mwaka huu tulipokutana na Bayern Munich.
Hali hiyo imetukuta pia tulipocheza na Borussia Dortmund msimu huu wa ligi ya mabingwa katika hatua ya makundi.
Unapata majibu ya ubora na uimara wa kitu baada ya kukitikisa. Arsenal imetikiswa na timu kubwa.
Inatia faraja kidogo kuangalia aina ya timu zilizotufunga msimu huu, lakini inashtua sana kugundua kwamba hatufurukuti sana mbele ya timu kubwa.
Hii ina maana kwamba hatuna uwezo wa kuhimili mitikisiko.
Napata shida sana kujua tatizo linatokea wapi kila nikiangalia aina ya wachezaji tulionao na aina ya soka tunalocheza.
Tuna wachezaji sahihi, lakini bado tunacheza soka la aina moja. Tunatengeneza magoli ya aina moja.
Tunakosa ubunifu mathalani mabeki wa timu pinzani wanapoamua kujaa langoni mwao, ni aghalabu sana kuona wachezaji wa Arsenal wakitengeneza daraja la kuvuka au kuihadaa defence ya timu pinzani, zaidi ya kurudisha mipira nyuma.
Tunataka kucheza soka lile lile bila kujali aina ya timu tunayopambana nayo na tupo katika mazingira yapi.
Tulifungwa na Napoli katika mchezo ambao tulikua tunatafuta sare tu ili tuongoze kundi, lakini bado timu ikawa inajilinda kwa mtindo ule ule ambao huwa tunautumia tunapoingia kwa ajili ya kushambulia.
Baada ya kutikiswa ndo unayagundua haya. Unagundua Olivier Giroud haitendei haki Arsenal. Nilisema hapa hapa kwenye The Gunning Machine kwamba Giroud ni mchezaji wa Capital One Cup kwa Arsenal ya sasa.
Kwa viungo wanaocheza nyuma yake, kuanzia kwa Flamini, Arteta, Ramsey, Wilshere, Cazorla, Özil, Rosicky, Walcott anapaswa kuwa juu ya Luis Suare'z. Kazi ya Giroud ni kufunga, siyo kutoa assist kama wengi wanavyodhani.
Rogerio Ceni wa Brazil, wakati wa enzi zake alifunga zaidi ya mabao 100. Huyu siyo mshambuliaji wala kiungo, ni goli kipa. Lakini bado magoli yake zaidi ya 100 hayakumfanya awe golikipa bora wa dunia. Unajua kwa nini?
Kufunga haikuwa kazi yake, ni kama ambavyo kuokoa mipira ya kona na kutoa assist zisivyo kazi za Giroud. Hizo ni sifa za ziada tu.
Tungemsifia zaidi ya wengine kama angekua anafanya hayo lakini anafunga zaidi kama jukumu lake namba moja.
Lakini tunayaona haya baada ya kutikiswa, ngoja tuone Profesa atafanya nini. Asingetikiswa asingefanya lolote lakini naamini atafanya jambo.
Haruna Niyonzima wa Yanga ameshuka kiwango siku hizi. Siyo yule aliyeitwa Fabregas, wanaoifuatilia Yanga wanajua. Lakini kwa kuwa Yanga inashinda, hakuna anaejali. Ni mpaka watikiswe. Arsenal imetikiswa, udhaifu wake umeonekana.
......>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>,<<<<<<<<<<<<<<
... Imeandaliwa na Richard Leonce Chardboy
chardboy74@gmail.com
0766399341
@chardboy77 kwenye twitter.



Iko poa sana!
ReplyDeletemacho yetu sie
ReplyDelete