MIWANI PANA YA EDO ~ SABABU NNE KUU ZA KUAMINI YANGA INASHINDA LEO
Ni muda mchache sana umebaki kabla ya timu kongwe Tanzania Simba na Yanga ambao ni wapinzani wa Jadi hawajaingia katika uwanja wa Taifa kumaliza ubishi wa nani mbabe baina ya timu hizo kwa msimu huu.
Simba inaingia katika mchezo wa leo ikiwa na point 18 katika nafasi ya 3 huku Yanga wao wakiwa na pointi 15 katika nafasi ya 5.
Huku Yanga wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tangu ligi ianze upande wao Simba hawajapoteza mchezo wowote mpaka sasa timu zote zikiwa zimecheza mechi 8.
Lakini tarehe kama ya leo mwaka 1990 timu hizi zilikutana na Yanga kushinda 3-1
Miwani pana yangu leo inaangaza kutazama kwa makini vikosi vyote vya timu hizi na hapa ndipo napata sababu nyingi zinazoipa Yanga Ushindi siku ya leo na hizi ni baadhi ya sababu hizo:-
UIMARA WA KIKOSI
Yanga wanaweza kuwa wameshafungwa dhidi ya Azam FC lakini bado naamini wana kikosi imara kuweza kushinda leo kwani wana kikosi ambacho kimekaa muda mrefu pamoja huku kikiongezewa nguvu na ujio na wachezaji wapya kama Mrisho Ngassa ambaye msimu uliopita alikua Simba.
Ikumbukwe Yanga waliwatambia Simba msimu uliopita wakishinda 2-0 katika mechi ya mwisho wa msimu.
Simba wao wameweza kutopoteza mchezo wowote mpaka sasa na ndo timu pekee pamoja na Mbeya City na Azam ambazo hazijafungwa mpaka sasa lakini wamekua na kikosi kilichojaa chipukizi wengi na hii ni baada ya kuacha zaidi ya 80% ya wachezaji wake waliokua nao msimu uliopita.
Timu hii inaweza kua nzuri sana hapo baadaye lakini wanapaswa kuaminiwa na kupewa muda zaidi. Japokua hawapaswi kubezwa kwani wameongoza kwa kipindi kirefu katika ligi hii inaweza kuwapa morali ya ushindi ya kuamini kama wanaweza na vijana wengi pia watataka kukuza majina yao kupitia mechi hii.
BENCHI LA UFUNDI
Sababu nyingine ya kuamini Yanga atashinda mechi hii ni kwakua na benchi la Ufundi lilelile ambalo liliwapa ubingwa mwaka jana huku Simba wao pamoja na kuacha wachezaji wengi pia ilimtema kocha wake Patrick Lewig kutoka Ufaransa na sasa wako na kocha Mzawa Abdallah Kibaden ambaye alikua Kagera Sugar msimu uliopita. Japokua kwa jicho lingine Kibadeni anaweza akataka kuwadhihirishia Yanga hakubahatisha alipofunga katika ushindi wa kihistoria ambao Simba waliupata dhidi ya Yanga wa 6-0 ambapo Kibadeni alipiga goli 3 mwenyewe.
AIBU YA KUFUNGWA 5-0 MWAKA JANA
Yanga wataingia katika mchezo wa leo na michezo mengine yote watakayokumbana na watani zao Simba kutaka kulipiza kisasi cha kufungwa 5-0 hivyo kuwa na nguvu zote ari na kasi ya kutaka kuwafurahisha mashabiki zao,wapenzi na wanachama na kurudisha heshima ambayo watani zao wamekua wakijidaia.
BAADHI YA WACHEZAJI KUTAKA KUIKOMOA SIMBA
Mrisho Ngassa wiki hii alinukuliwa akisema kama asipofunga au kutoa pasi ya goli atachoma mojawapo ya nyumba zake 5 hii inaonyesha kabisa alivyo na usongo wa kuiangamiza Simba hasa baada ya kulipishwa milioni 45 juzi juzi na kufungiwa kwaajili ya kusaini kuchezea Simba.
Athumani Idd Chuji naye ni kati ya wachezaji walio na chuki na Simba hasa baada ya yote yaliyotokea siku za nyuma, pia wamo Mbuyi Twite, Kelvin Yondani n.k
Hizo ni baadhi tu ya sababu ambazo miwani yangu pana inanipa kiburi cha kuamini kuwa Yanga wanaweza kushinda mechi hii ya leo lakini hii sio formula ya kuamini kama matokeo lazima yawe hivyo kwani mpira ni dakika 90 na makosa ndo hupelekea timu flani kupoteza mchezo.
Mechi hii inaruka live kupitia TBC1
....... kwa ushauri na maoni niandikie kupitia facebook Edo Daniel Chibo au email: mfalme.edo@gmail.com
No comments