THE GUNNING MACHINE ~ UPANDE WA PILI WA SARAFU NI MCHUNGU KULIKO UTAMU WA UPANDE WA KWANZA.

 
Arsenal wana kitu kipya msimu huu ambacho walikikosa kwa muda mrefu kitu hicho ni Ari ya ushindi.
Ligi kuu ya England ni ligi ngumu sana. Ina timu zinazocheza soka safi kama Swansea, ina timu zinazocheza soka la mahesabu kama Chelsea, ina timu zinazotumia ubabe kama Stoke City, Zipo timu zinazocheza soka la ushindani kama Manchester UTD, timu ngumu kama Everton n.k.
 
 
Kuchukua pointi kutoka kwa aina hizo za timu inahitaji zaidi ya umahiri wa kucheza soka.
Miaka michache iliyopita, Arsenal walikuwa wakipoteza mechi nyingi za kawaida kutokana na kukosa morali. Mimi naamini Arsenal ni moja kati ya timu nzuri, zenye wachezaji mahiri sana katika dunia hii lakini huwa wanakosa morali ya kuwafanya wajitume.
Morali ndiyo inayokufanya ushinde mechi ngumu kama ile ya September 14 dhidi ya Sunderland ugenini. Ni mechi ambazo Arsenal huwa wanapoteza mara kwa mara na ninahisi wanaweza kuendelea kupoteza kama morali waliyo nayo itapotea.
 
 
Mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Olympiq Marseille, Arsenal walishinda lakini ilikuwa ngumu sana. Marseille waliishambulia sana Arsenal.
Huwa naogopa sana Arsenal inaposhambuliwa kwa sababu huwa inakosa mbinu mbadala (plan B).
Arsenal ni timu ya soka safi na la kuvutia. Siyo timu ya kutafuta penati au kutegemea kufunga kwa faulo (free kicks). Hata idadi ya mabao yanayofungwa kwa mipira ya kona ni ndogo sana.
 
 
Sikumbuki ni lini Arsenal walifunga goli kwa shuti kali la mita 35. Siyo kawaida yao. Huwa wana aina moja tu ya uchezaji ili washinde.
Wanapaswa kushambulia ili uwapende lakini soka lina pande mbili za sarafu. Kuna kushambulia na kushambuliwa.
Huwezi kucheza na Man UTD halafu ukategemea usishambuliwe, haiwezekani. Unachoweza kufanya ni kuzuia mashambulizi yasilete madhara. Na hapo ndipo ninapokosa imani.
Arsenal wanajitahidi sana lakini wanatia shaka wanaposhambuliwa. Wanampa wakati mgumu sana golikipa Wojchiech Szczesny.
Unajua kwa nini Arsenal wamepigiwa penati nyingi zaidi mpaka sasa kwenye ligi kuu?
Ni kwa sababu wana mfumo dhaifu wa ukabaji na kwa sababu morali ipo juu, wanajikuta wakicheza rafu nyingi kwenye kumi na nane yao. Japo kuna lawama kwa waamuzi katika hili.
 
 
Upande wa pili wa sarafu ya soka kwa Arsenal (kushambuliwa) ni mchungu kuliko utamu wa upande wa kwanza (kushambulia).
Arsenal wakishambuliwa huwezi kumwona Mesut Özil akipiga zile pasi zake. Sana sana utaona Jack Wilshere anaumia, kisha Koscielny anapata kadi nyekundu wakati Flamini ana njano tayari.
Sasa ili kushinda mechi ya aina hii unahitaji morali ya hali ya juu na ndiyo maana ukiacha mechi za 'pre season' Arsenal wamefungwa na Aston Villa pekee tangu Machi 3 mwaka huu mpaka sasa ninapoandika makala haya.
 
 
Morali inawawezesha walau kulazimisha sare pale wanaposhambuliwa. Na hata kushinda kwenye mazingira magumu kama walivyofanya pale Stade Velodrome Ufaransa usiku wa Septemba 18.
Hii ndiyo faida ya ari ya ushindi. Kwa sasa Arsenal wakikushambulia watakufunga tu. Olivier Giroud amefunga mabao matano kati ya mashuti sita aliyopiga langoni.
Siyo rahisi kuendelea na form hiyo lakini inaonesha jinsi anavyozitumia nafasi adimu anazozipata.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy.

Nipate katika
Email:chardboy74@gmail.com
facebook:Richard Leonce Chardboy
twitter:@chardboy77
simu:0766399341

2 comments:

Powered by Blogger.