THE GUNNING MACHINE ~ UMUHIMU WA MESUT ÖZIL UNAHITAJI JICHO LA TATU

Mesut Ozil
 
"Ninatazama mbele kwa kweli, kwa sababu ya imani kubwa aliyonayo mwalimu kwangu. Tumeongea mengi kwa simu na ameniambia mipango yake, ananiamini sana. Kitu ambacho ninakihitaji kama mchezaji.
Niligundua kwamba sitaweza kupata imani ya namna hiyo kwa sasa (kutoka Real Madrid) na nina hisi nitaipata imani hiyo nikiwa Arsenal, ndiyo maana nimesaini na klabu hii."
Ni maneno ya mfalme mpya na mshika bunduki wa kijerumani aliyetua Arsenal katika siku ya mwisho kabisa ya usajili wa majira ya kiangazi mwaka 2013, Mesut Özil.
Ni furaha katika moyo wa kila shabiki wa Arsenal. Furaha inatokana na umahiri wa mchezaji husika pamoja na mvuto alionao kwa mashabiki.
Furaha ya kumsajili Özil ni kubwa kuliko furaha unayoweza kuipata ukimsajili Xabi Alonso katika dunia ya sasa.
Yamezungumzwa mengi kuhusu usajili wake, wengi wakisema hakuwa hasa suluhu ya matatizo ya Arsenal. Lakini nataka tufumbue jicho la tatu tuone Özil analeta nini katika kikosi cha Arsenal. Ndani na nje ya uwanja.
                
                      NJE YA UWANJA.
 
Kuna jinsi ambavyo Özil analirudisha jina la Arsenal kwenye chati ya timu kubwa duniani. Ni mchezaji mkubwa kutoka timu kubwa na ye hadhi ya juu.
Unapokuwa na watu kama Jack Wilshere, Theo Walcott na Lucas Podolski jina la timu yako linatajwa kwa uzito fulani.
  
Lakini unapomwongeza Mesut Özil ukubwa wa jina lako unaongezeka mara mbili. Unamfanya Yaya Sanogo na Carl Jenkinson wajione wenye bahati kuchezea timu hiyo.
Lakini pia unaongeza thamani yako. Unaweka tofauti kati ya Arsenal na Wolves au Newcastle. Timu kubwa ni lazima iwe na watu kama Özil. Watu wanaolipwa pesa nyingi lakini pia wenye uwezo wa kujilipa kwa mauzo ya jezi tu peke yake.

 
                     NDANI YA UWANJA.
 
Hapa ndipo wengi wanapopatatilia shaka. Wanajiuliza Santi Cazorla, Aaron Ramsey, Thomas Rosicky, Jack Wilshere. Unamwongeza Özil wa kazi gani?
Fumbua jicho la tatu utabaini yafuatayo-;
Mpaka sasa, ikiwa na Lucas Podolski nje kwa majeraha, Arsenal inacheza bila ya winga wa kushoto. Usisahau kwamba hakuna Gervinho.
Lakini kumbuka niliwahi kusema hapa kwamba Santi Cazorla anakua hatari zaidi akitokea pembeni na siyo katikati.
Ni wazi sasa kua ndicho kinacho kwenda kutokea. Özil anaenda kucheza kama kiungo mshambuliaji. Nyuma ya mshambuliaji wa mwisho ili Cazorla asogee pembeni kushoto kama alivyokua Malaga.
Hili halina madhara makubwa kama watu wanavyodhani kwamba Arsenal itafunguka sana ikiwatumia Cazorla na Özil kwa pamoja. Haina maana hiyo.
 
Wala haina maana kwamba kwa vile Özil alitengeneza nafasi 91 msimu uliopita huku Cazorla akitengeneza 95 basi wanakwenda kutengeneza nafasi 186 wakiwa Arsenal. Haina maana hiyo hata kidogo.
Kama kufunguka na kuvuja, nadhani Arsenal ingevuja katika mchezo dhidi ya Tottenham ambapo Wilshere, Rosicky na Cazorla walicheza kwa pamoja tena bila ya winga wa kweli wa kushoto.
Natambua upungufu wa washambuliaji unaozungumzwa na ninasikitika kwa sababu tumewakosa washambuliaji wote tuliowavizia, kuanzia kwa Wayne Rooney mpaka kwa Demba Ba.
Lakini tusubiri tuone urejeo wa Nicklas Bendtner, Watu hawamzungumzi kabisa. Wanamkumbuka Bendtner aliyecheza mbele ya Cesc Fabregas, Nasri na Rosicky na akashindwa kuwashawishi. Lakini Bendtner wa sasa ana miaka 25, unaweza kutegemea chochote kutoka kwake.
Lakini nana anajua, huenda Lucas Podlski akatumika kama mshambuliaji. Kwa uzoefu alionao, sidhani kama anaweza kukuangusha akiwa na safu ya kiungo hatari kama aliyoisajili Arsene Wenger.
Morali ya timu ni kitu kingine ambacho Özil anaenda kukirudisha. Ukosefu wa hamu ya kushinda na kutokujiamini vimekua vikiiangusha sana Arsenal.
Timu imekua ikipata matokeo ya kushangaza. Huwezi kufungwa na AC Milan mabao 4-0 kisha ukashinda 3-0 kwenye mchezo wa marudiano.
Au unafungwa 0-3 nyumbani na Bayern Munich kisha unamfunga 0-2 ugenini. Hapo lazima kuna tatizo ambalo linahitaji wachezaji wazoefu na wenye thamani kubwa kama Özil.
Kwa jicho langu la tatu, naamini Arsenal wamempata mtu sahihi ndani na nje ya uwanja.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy.
Nipate katika chardboy74@gmail.com na @chardboy77 kwenye twitter au 0766399341.

 

No comments

Powered by Blogger.