MIWANI PANA YA EDO ~ ARSENAL vs SPURS: JE HUU UTAKUA MWISHO WA ARSENAL KUTAWALA JIJI LA LONDON?


Baada ya mechi ya Liverpool vs manchester United unafata mtanange huu wa watani wa jadi pale katika jiji la London baina ya Arsenal na Totenham Hotspurs.
Jiji la London limebarikiwa kuwa na timu nyingi ambazo hufanya mechi kati ya timu hizo kuwa na upinzani mkali na hapa ndo namwelewa mshkaji wangu Allen Kaijage anapoombea baadhi ya timu zishuke daraja katika jiji hilo ili kupunguza ugumu wa mechi zinazojulikana kama "Dabi"
Miwani yangu pana muda huu inajikita kuangazia mechi itakayoanza muda wa saa 12 Jioni kati ya Washindi wa nne na wale washindi wa Tano katika ligi msimu uliopita.

Totenham Hotspurs inaingia katika mchezo wa leo utakaopigwa katika uwanja wa Emirates huku ikiwa na sura mpya katika kikosi chake. Wachezaji wengi wameondoka na wengi wamesajiliwa na Spurs ambayo inaaminika kuwa timu ya kwanza msimu huu kutumia pesa nyingi katika usajili kwani imeshatumia zaidi ya paundi milioni 100 kusajili wachezaji mbali mbali.

Kwa upande wao Arsenal wataingia katika mchezo wa leo wakiwa wamesajili wachezaji wawili tu tena bure kabisa Yaya Sanogo na "mwana mpotevu" Mathew Flamin huku kikosi chake cha kwanza kikiwa salama baada ya kutompoteza mchezaji yeyote wa kikosi hicho kitu ambacho kocha wa Arsenal anajivunia na kuamini kama timu yake itafanya vizuri. Ikumbukwe imezoeleka Arsenal kupoteza mchezaji muhimu kila msimu unapoanza.

Laurent Koscielny anataraji kurudi katika pambano la leo baada ya kutumikia adhabu ya kukosa mechi moja baada ya kupata kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Aston Villa. Aaron Ramsey ambaye amekua moto kwa siku za hivi karibuni ataungana na Jack Wilshere pale kati huku mbele wakiwa Giroud, Walcott na Carzola.
Lucas Podoski, Chamberlain na Arteta wanaendelea kukosa mechi baada ya kuumia na hivyo wataungana na Diaby na Vermalean ambao nao ni wagonjwa.

Upande wao Spurs wanaweza kumkosa nyota wa Timu hiyo gareth Bale ambaye yuko bize kushughulikia dili lake la kujiunga na Real Madrid. Adebayor na Assou- Ekkoto nao wataikosa mechi hii kwakua hawana "match fitness".
Defoe,Mousa Dembele na Soldado wataanza huku wakisaidiwa na wageni katika ligi na klabu hiyo Etienne Capoue na Paulinho.

Katika historia ya Ligi kuu nchini England haijawahi kushuhudia mechi kubwa iliyojaa magoli kama mechi baina ya miamba hii kwani kwa miaka 15 sasa timu hizi hazijawahi kutoka  sare ya bila kufungana.

HISTORIA INASEMAJE?

  • Katika mechi 6 zilizopita baina ya timu hizo magoli 31 yamepatikana ikiwemo ushindi wa 5-2 walioupata Arsenal miaka miwili iliyopita.
  • Totenham Hotspurs imeshinda mara moja tu katika uwanja wa nyumbani wa Arsenal Tangu kuanzishwa kwa ligi msimu wa mwaka 1992/1993. Ikishinda 3-2 mwaka 2010 mwezi Novemba.
  • Katika mechi nne zilizopita za ligi katika uwanja wake wa nyumbani, Arsenal imeshinda mechi moja tu, Wakitoka sare mara 2 na kupoteza mara 1.
  • Magoli yote 13 katika Ligi ambayo mshambuliaji wa Arsenal, Olivier Giroud amefunga tangu ajiunge na Arsenal amefunga akiwa katika jiji la London huku 11 kati ya hayo akiyafunga katika uwanja wa Emirates.
  • Ushindi dhidi ya Fulham wiki iliyopita umeifanya Arsenal kushinda mechi ya 100 katika ligi baina ya timu za London (London Derbies).
  • Arsenal hawajawahi kufungwa katika mechi mbili za mwanzo wa ligi katika uwanja wake wa nyumbani tangu walipofungwa na Barnley na Chelsea katika uwanja wa Highbury msimu wa mwaka 1949/1950.
  • Roberto Soldado amefunga magoli 12 katika michezo 10 ya Ligi tangu akiwa Spain na kama akifunga leo basi atakua mchezaji wa kwanza katika kikosi cha Spurs kufunga michezo mitatu mfululizo akifata nyayo za Jermain Defoe.

  • Spurs wametengeneza nafasi 39 za kufunga msimu huu lakini hakuna hata nafasi moja iliyozaa bao mpaka sasa kwani magoli yao mawili katika mechi mbili zilizopita yalitokana na mikwaju ya penati.
  • Spurs imeanza na ushindi mfululizo katika ligi kwa mara ya kwanza tangu msimu wa mwaka 2006/2006 waliposhinda mechi 3 mfululizo za ligi.
  • Mechi ya mwisho baina ya timu hizo, Spurs walishinda 2-1 magoli ya Gareth Bale na Aron Lennon huku Arsenal wakifunga kupitia kwa Per Mertesacker.

Hii ni vita ambayo haitumii risasi za moto bali ni dakika 90 uwanjani.

..... Kwa maoni na ushauri nicheki Facbook: Edo Daniel Chibo au Email. wapendasoka@gmail.com au hewani katika 0715 12 7272

No comments

Powered by Blogger.