THE GUNNING MACHINE ~ MCHAWI WA WILSHERE HUYU HAPA.

 
Wilshere
Kama nilivyoahidi kwamba nitaongea baada ya Arsenal kutegua kitendawili cha kucheza au kutocheza ligi ya mabingwa msimu huu.
Kitendawili kimeteguliwa na Arsenal wamefuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ambayo yamekwishapangwa tayari.
Carzola
Sitazungumzia ugumu wa kundi letu leo, bado tuna muda wa kutosha. Nataka nijaribu kuiangalia timu yetu kiufundi kidogo kwa jicho langu.


Kila timu ina mtu ambaye kwa lugha ya kimchezo tunasema "ana free role". Ana uwezo wa kurandaranda na mpira, kupita katikati au pembeni ya kiwanja (mara nyingi upande wa kushoto).
Msimu uliopita, Arsenal walimsajili Santi Cazorla kutoka Malaga na moja kwa moja akakabidhiwa jukumu hilo. Cazorla akawa anapita popote penye nafasi bila kuathiri mfumo wa timu.
Ghafla, kiwango cha Jack Wilshere ambaye alikua majeruhi kwa kipindi kirefu kikaonekana kupanda kwa kasi sana. Ni kipindi ambacho Mikel Arteta alikua imara kwenye safu ya kiungo (mkabaji).
Ni kipindi ambacho Theo Walcott alikua kwenye mazungumzo marefu ya kusaini mkataba, hivyo akawa hana msaada mkubwa kwa timu.
Basi ni wakati huo ambapo Wenger aliamua kuiunda timu yake kwa kupitia Jack Wilshere. Arteta alikuwepo nyuma yake na Cazorla alikuwepo mbele yake. Hii ilimpa Wilshere "free role".
 
Umuhimu wa Jack Wilshere ulianza kupungua baada ya Walcott kurudisha makali yake kwenye wing ya kulia. Pasi nyingi zikawa zinaelekea kwake, na sasa Wilshere akawa anatakiwa kuanzisha yeye shughuli ya ukabaji pale mipira inapopotea. Kazi ambayo hakuwahi kuifanya hapo kabla.
Kutokana na aina ya mchezo wa Jack Wilshere, akaanza kujikuta kwamba anapata kadi mara kwa mara ambazo zilikua zinamtoa mchezoni kwa kuona anaonewa.
Hapo ndipo Aaron Ramsey alipoonekana muhimu.
Kwanza hana hasira, pili anakimbia umbali mrefu bila kuchoka, tatu siyo mpenzi wa kukaa sana na mpira kama wilshere.
Lakini uwepo wa Ramsey uwanjani unakupa faida ya ziada kwa sababu ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi.
Msimu huu mambo yanaonekana kumnyookea Ramsey kwa sababu mbili. Kwanza kiwango chake binafsi kimepanda, pili Mikel Arteta hayupo.
Anachokifanya Wenger ni kuzihadaa timu pinzani kwamba Ramsey anacheza kama kiungo mkabaji, kitu ambacho siyo kweli. Ramsey anatumika kama mtumwa tu wa viungo wengine katika timu.
Ndiyo maana utaona pindi timu inaposhambuliwa anakuwepo pamoja na kiungo mwingine (Wilshere au Rosicky) na pindi timu inaposhambulia anakuwepo pamoja na kiungo mwingine (Rosicky, Wilshere au Cazorla).
 
Ukitazama hiyo chati ya mchezo wa kwanza dhidi ya Fernerbahce utashindwa kugundua ni nani mwenye jukumu la ulinzi kati Ramsey na Wilshere.
Wanaonekana kama mtu mmoja.
Angalia vizuri utagundua kwamba hakuna hasara kama unamwondoa mmoja kati yao (kulingana na ugumu wa mechi) ili umpange Podolski kushoto (kama ilivyokua dhidi ya fulham).
Na kutokana na faida za Ramsey nilizozitaja hapo juu, ndipo Wenger anapoamua kumpanga badala ya Wilshere kwa sasa.
Kwa jinsi chati inavyoonesha katika mchezo huo, hakukua na winga wa kushoto, bali Cazorla na Rosicky ndiyo waliokua wakivizia upande huo kwa zamu na kwa kushirikiana na Gibbs, walifanikiwa kuwahadaa mabeki wa Fenerbahce.
Lakini faida ya kumwondoa mmoja kati ya Ramsey na Wilshere ni umuhimu wa kumpanga Lucas Podolski kwenye wing ya kushoto kwa sababu ana sifa za mshambuliaji (siyo winga teleza), hivyo atakupatia magoli pia au hata mashuti kadhaa.
Lakini pia kwa kuwa winga anakuwepo, basi inawapa Rosicky na Cazorla uhuru (free role) wa kufanya ufundi mbele ya 18 ya adui na hivyo kifanya Arsenal ionekane maridadi machoni kama ilivyokua dhidi ya Fulham.
Kwa sasa Podolski ni majeruhi, sijajua nani ataziba pengo lake.
Mfumo huu siyo mzuri kwa ulinzi lakini kwa sasa Arsenal wanacheza hivyo ndiyo maana Jack Wilshere anaonekana kupotea, lakini kama Arteta atarudi, au kama Flamini atakuja na jipya, basi tegemea kumwona Jack10 akiibuka kwa mara nyingine.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy.

Nipate katika chardboy74@gmail.com au @chardboy77 kwenye twitter na 0766399341.

No comments

Powered by Blogger.