THE GUNNING MACHINE ~ UKIWA SHABIKI WA ARSENAL UNAPASWA KUVUMILIA
Arsenal |
Alikataa kwa sababu nilishindwa kumpa sababu za kueleweka za kufanya hivyo. Siyo kwamba sikuwa nazo ila nilijua hata ningempa asingenielewa kwa sababu yeye siyo mpenzi wa Arsenal. Hajui inakuwaje kuwa shabiki na mwandishi wa makala za klabu hii.
Wiki iliyopita niliwapa wasomaji wangu angalizo kwamba wasiamini katika tetesi za usajili, nikawashauri watulie angalau wasubiri taarifa rasmi.
Nilisema hivo kwa sababu mimi mzoefu sana wa sera za usajili za Arsenal. Zaidi ya 70% ya wachezaji wazuri duniani hivi sasa, waliwahi kuhusishwa kujiunga na Arsenal.
Christiano Ronaldo, Didier Drogba, Fernando Tores, Carlos Tevez, Juan Mata, David Luiz, Alexis Sanchez, Demba Ba, Luis SuareZz, Rafael & Fabio Da Silva, Yaya Toure, David Villa n.k. Ni wengi sana, lakini hakuna aliyesajiliwa zaidi ya tetesi kufifia.
Wito wangu ukapuuzwa na wapenzi wenzangu wa Arsenal, japo siyo kwa kupenda ila kwa mapenzi yao ya dhati kwa klabu hii.
Wakaendelea kujisumbua kuniuliza mimi masikini ambaye sina uhusiano wowote ule na maafisa habari wa Arsenal kuhusu Higuain nikawaambia sina taarifa zozote.
Wakaniuliza vipi kuhusu Luis Suarez nikawajibu sijui.
Labda niwakumbushe ndugu zangu hawa kitu kimoja. Mwaka 2002, timu moja nchini Uingereza ilimsajili beki anaitwa Rio Ferdinand kwa ada ya £30m.
Wakati timu hiyo inamsajili Rio kwa fedha hiyo, Arsenal wao wakamsajili Pascal Cygan kutoka Lille kwa £2m eti aje kuziba pengo la Ian Wright aliyestaafu msimu mmoja kabla.
Arsenal walikuwa katika wakati mzuri kipindi hicho lakini ukweli unabaki pale pale kwamba huwezi kupata mbadala wa Ian Wright kwa £2m. Na hata ukimpata utahitaji muda kumtengeneza.
Bahati mbaya sana, miaka 11 baadaye, Arsenal hawajaacha tabia hii. Wenzao walishaacha. Huwezi kumpata mbadala wa Robin Van Persie kwa £11m, labda umwongezee miaka minne mbele na uwe tayari kusubiri.
Arsenal wamekwenda barani Asia kujiandaa na msimu mpya bila nahodha wao Thomas Varmaelen ambaye tunaambiwa ni majeruhi kama walivyomwacha Cesc Fabregas kwa sababu hiyo kisha wakamuuza.
Mabeki waliopo fit ni Per Martesacker na Laurent Koscielny.
Kuna mechi muhimu ya msimu inakuja. Ni mechi ya awali ya mtoano ya ligi ya mabingwa Ulaya.
Kama kumbukumbu zangu zipo sahihi na jama taratibu zipo kama ninavyofikiri, ni kwamba Koscielny na Cazorla hawatacheza mchezo huo kutokana na kadi za njano walizozipata msimu uliopita.
Kumbe hata ukuta wetu unapaswa kuongezewa nguvu. Ukiyafikiria sana haya, unapata mvurugiko wa mawazo. Na hiyo ndiyo sababu ilinifanya nitamani kuisitisha The Gunning Machine. Nilitaka nisubiri angalau ligi ianze ili nijue Arsene Wenger ana mipango gani.
Kwa sasa sijui, bado nachekeshwa tu na taarifa za magazeti kuhusu Gonzalo Higuain ambaye kumbe hakuna hata ofa iliyokwenda Real Madrid kwa ajili yake, japo najua kwamba Arsenal wanamvizia.
Naamini Arsenal wanamvizia Higuain na siyo Suarez kama inavyoandikwa. Magazeti ya Uingereza yanaipenda Arsenal kuliko Real Madrid.
Naamini kwamba taarifa za Suarez kwenda Arsenal ni kwa ajili ya kuwashitua Real ili wamchukue haraka na iwe rahisi kwao kumtoa Higuain. Ndivyo fikra zangu zinavyoniambia.
Kwa zaidi ya nusu ya umri wangu nimekuwa nikiifuatilia Arsenal na kwa bahati nzuri ni kwamba ipo na kocha mmoja kwa kipindi chote hicho,hivyo ni mara chache sana mimi kuwa mbali na ukweli kuhusu Arsenal.
Kwa leo tuishie hapa, lakini nataka nimalize na taarifa ambayo wapenzi wengi wa Arsenal wanaweza wasiijue kutokana na kuwa bize na usajili wa Higuain ni kwamba Arsene Wenger yu mbioni kusaini mkataba mpya na Arsenal.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka Group.
Nipate katika chardboy74@gmail.com, @chardboy77 kwenye twitter na 0766399341
usisahau pia kulike page ya Wapenda Soka-Kandanda kwenye Facebook
No comments