THE GUNNING MACHINE ~ SANOGO SAWA, LAKINI...........

Yaya Sanogo
Kuna mtu anava jezi namba 6 ya Arsenal hivi sasa, na urefu wa futi 6.1. Kwa jina anaitwa Laurent Koscielny. Ana misuli ya kutosha tu na juzi juzi nimesikia Barcelona na Bayern Munich wanamtaka kutokana na kiwango kizuri alichokionesha mwishoni mwa msimu uliomalizika.
Koscielny hakutokea kwenye academy ya Arsenal. Alisajiliwa kutoka FC LORIENT ya Ufaransa mwaka 2010. Hii ni klabu ambayo mafanikio yake makubwa ni kushika nafasi ya 5 kwenye ligi kuu ya Ufaransa mwaka 2009, ingawa ilimaliza katika nafasi ya 7.

Koscielny
Leo Koscielny ni lulu Arsenal, Arsenal hawataki kumuuza japo walibezwa walipomnunua.
Kubezwa ni sahihi wakati mwingine. Mtu aliyekubeza wakati unamsajili Maroane Chamakh bure kutoka Bordeux yupo sahihi leo. Lakini aliyekubeza wakati unamsajili Koscielny hayupo sahihi hata kidogo.

Arsenal wamemsajili Yaya Sanogo kutoka AJ-AUXERRE ya Ufaransa. Ni mshambuliaji kijana mwenye umri wa miaka 20 na urefu wa futi 6.5.
Mimi sijawahi kumwona popote akicheza zaidi ya YouTube ambayo huwa inamfanya Diaby aonekane kama Zidane, lakini nimeangalia takwimu, nikaridhika kwa kiasi fulani.
Inaonekana alijiunga na timu ya vijana ya Auxerre akiwa na umri wa miaka 13 tu. Akasota huko mpaka mwaka 2010 alipopewa mkataba wa miaka mitatu baada ya kufunga magoli 25 katika michezo 14 na kutoa pasi 17 za magoli. Siyo kitu cha kawaida hiki.

Kinachoshtua ni thamani yake, Kwa klabu kuruhusu mchezaji mwenye miaka 20 kuondoka bure, inatia shaka kidogo. Lakini ukweli ni kwamba huyu kijana mkataba wake umekwisha juni 30 na Arsenal wakamsajili siku moja baadae ili kukwepa gharama. Huu ni ujanja wa kawaida  tu kwa Arsene Wenger.
Siutazami usajili wa Sanogo kama kitu muhimu kwa msimu ujao, wala siutazami kama tatizo kwa sasa. Nani anajua?
Huenda akaishia mahala kwa mkopo kama akina Ryo Miyaichi na Joel Campbell!

Au hata akibaki klabuni kama akina Serge Gnabry na Thomas Eisfield ili apate uzoefu, sina tatizo kabisa.

Taa nyekundu itawaka kichwani mwangu kama Arsene Wenger atamfanya kuwa striker pekee kuongezwa kwenye kikosi chake kwenye msimu huu wa usajili.
Hakuna muujiza anaoweza kuufanya Sanogo katika msimu wake wa kwanza, kama nia ya Arsenal siyo kuwa wasindikizaji msimu ujao.

Msimu uliomalizika, Arsenal walikuwa na Olivier Giroud kama mshambuliaji. Japo Wenger alikuwa na mpango wa kuwatumia mawinga wake hatari akina Walcott na Gervinho kama washambuliaji ndani ya mchezo mmoja kwa kupokezana ili kumchanganya adui lakini bahati mbaya walimwangusha na mpango huo haukufanikiwa.

Giroud akabaki mwenyewe, alipokuwa majeruhi au kuwa nje kwa adhabu, basi timu inakuwa na pengo kubwa. Pamoja na pengo hilo na Giroud kuonekana mchezaji muhimu kiasi hicho lakini bado umuhimu wake haukulingana na uwezo wake uwanjani.
Uwezo wa kucheza dakika 90 kwa kiwango kile kile. Nadhani hata yeye wakati anatua Arsenal, alitarajia kuwa msaidizi wa Robin Van Persie, yani atumike wakati RVP ni majeruhi au kwenye kombe la Capital One.

Hakuna jinsi ambavyo Arsenal watakwepa mahitaji ya mshambuliaji wa kiwango cha dunia, mshambuliaji wa kukufungia walau magoli 30 kwa msimu huku Giroud akifunga angalau 15 na walcott, Gervinho, Podolski na wachezaji wengine wakikupa jumla ya mabao walau 25 kwa msimu. Hapo huwezi kukosa kombe.

Pamoja na nafasi nyingine lakini Arsenal wanahitaji mshambuliaji. Siyo mshambuliaji tu, anatakiwa mtu atakayemfanya Giroud awe chaguo la pili kikosini.
Kwa timu inayotaka ubingwa, Giroud anapaswa kucheza kombe la Capital One au kuingia dakika ya 70 kwenye michezo migumu na siyo yeye kuwa ndiye mshambuliaji tegemeo.

Soko linao washambuliaji wa namna hiyo. Sitaki kuzungumzia majina makubwa yanayotajwa kuelekea Emirates, wala sitaki kutarajia chochote kwa sababu Arsene Wenger siyo mgeni kwangu.

Kama utamfufua shabiki wa Arsenal aliyekufa Agosti mwaka 2012, ukamwambia Yann M'vila hachezei Arsenal, shabiki huyo ataomba kufa tena. Hawezi kuamini.

Na kutokana na hilo sitaki kuamini chochote kuhusu Higuain mpaka athibitishwe rasmi.
Nani anamzungumzia Stefan Jovitec leo. Tulimzungumza sana wiki chache zilizopita, tukamchoka, tukamzungumza Rooney, tukamchoka. Sasa tunamzungumza Higuain.
Nasema Sanogo sawa, lakini siyo kwa msimu ujao.

>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>

Imeandikwa na Richard Leonce ChardBoy kutoka Wapendasoka (Kandanda)Group.
Nipate katika wapendasoka@gmail.com, chardboy74@gmail.com na @chardboy77 kwenye twitter. Au 0766399341.
Usisahau kulike page ya Wapenda Soka - Kandanda kwenye facebook.

4 comments:

  1. naskia mpaka suarez anatajwa kuelekea emirates na kuna watu wanaamini.

    ReplyDelete
  2. £23m ni hela nyingi kwa Arsenal. Sijui kwa nini Wenger hakumchukua Llorente bure.

    ReplyDelete

Powered by Blogger.