THE GUNNING MACHINE ~ MASIKINI NAHODHA WETU KIPENZI FABRIGAS!!


UKWELI UNAOTIA HURUMA KUHUSU NAHODHA WETU.

Huwezi kuwa shabiki wa Arsenal usimjue Francesc Fabregas. Huyu alikua nahodha kipenzi wa Arsenal kabla ya kutimkia Barcelona ya Spain, timu ambayo mwenyewe anadai ni asili yake.
Ni kweli, Cesc aliipenda Barcelona akiwa na umri wa miaka 9, wakati huo akiichezea klabu ya watoto ya CE MATARO.

Mwaka mmoja baada ya kuanza kuipenda Barcelona, akiwa na umri wa miaka 10 tu
akapata bahati ya kusajiliwa na shule ya soka ya La Masia hiyo Ilikua mwaka 1997.
Alikua akicheza kama kiungo mkabaji, lakini akawa anafunga mpaka magoli 30 kwa msimu akiwa na akina Gerald Pique na Lionel Messi.
Moyo wake ukaandaliwa kwamba anapaswa kuichezea Barcelona siku moja kama ilivyo ndoto ya kila mwana La Masia.
 

Ili akomae zaidi, ikabidi Cesc atafutiwe timu. Hapo ndipo Arsene Wenger alipoitumia nafasi hiyo kumnyakua kijana huyo wa kihispaniola akiwa na umri wa miaka 16 mwaka 2003.
Kumbuka alikuja akiwa na ndoto yake ya kuichezea Barcelona siku moja. Hakuwa na mpango na unahodha wa Arsenal, kama ni unahodha angeutamani zaidi wa Barcelona.
Akavunja rekodi nyingi ikiwemo ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kucheza kikosi cha kwanza cha Arsenal kwenye mchezo wa kombe la Carling akiwa na umri wa miaka 16 na siku 177.


Akatokea kuwa mchezaji muhimu sana Arsenal, akapewa unahodha, kampuni ya vifaa vya michezo "Nike" wakampa kiatu maalumu cha kupigia pasi, akapendwa na kila mtu anayeipenda Arsenal.
Kuna mashabiki wengi waliwapa watoto wao jina lake. Hakuna alichokosa Fabregas akiwa na Arsenal zaidi ya vikombe.

Kukosa vikombe akiwa na Arsenal, huku kila siku akiwatazama aliocheza nao zamani wakifurahia ushindi na kila mwaka wanaleta ofa ya kumtaka. Uwezo anao wa kucheza Barcelona. Angefanyaje na anakiri timu hiyo ndiyo asili yake.?
Arsene Wenger akataka £35. Inasemekana Cesc mwenyewe alizama mfukoni kuongeza kiasi fulani cha pesa ili ada itimie aondoke akatimize ndoto yake.

Hatimaye tarehe 15 Agosti 2011, akasaini kuichezea Barcelona. Mashabiki wa Arsenal wakaumia sana, lakini  hakuna watu wajeuri kama hawa. Nakumbuka mtu mmoja aliniambia, "hata Yesu Kristo angeichezea Arsenal, kuna siku angeondoka tu, Fabregas kitu gani bwana?"

UKWELI UNAOUMA.

Nahisi Arsene Wenger aliukamua utamu wote wa Cesc kama Sir Alex Ferguson alivyoukamua utamu wa Wayne Rooney.
Akiwa Arsenal, Cesc alitengeneza jumla ya nafasi 541 za kufunga, yeye mwenyewe akafunga mara 30. Hiyo ikamfanya kuwa juu ya viungo wote duniani kwa kipindi chake. Hata Xavi na Iniesta hawakumfikia.
Fabregas alichelewa kujiunga na Barcelona. Ofa ya kwanza ilienda Arsenal mwaka 2006 lakini Arsenal wakaikataa.

Nadhani huo ndiyo ulikua wakati wake muafaka wa kujiunga na Barca. Angeweza kuyafanya yote aliyoyafanya Arsenal kama angepewa nafasi huko Catalunya lakini haikuwa hivyo.
Lakini siyo kosa lake, alipaswa afanye uamuzi mgumu wa kupambana na akina Xavi na pengine angeozea benchi. Hivyo alikuwa sahihi kubaki Arsenal.
Akaja kufanya maamuzi hayo miaka mitano baadae. Alichelewa sana. Bahati mbaya kwake ilikuwa ni kutimka kwa kocha Pep Guadiola aliyemsajili. Kocha aliyebaki Tito Vilanova hakujua amtumieje Fabrigas.

Wadadisi wa mambo wanaiona Barcelona ya sasa kama timu isiyokuwa muafaka kwa watu kama Fabregas, Rafinha na kaka yake Thiago aliyetimkia Bayern Munich.
Thiago amekubali kwa sababu moyo wake siyo kama moyo wa Cesc. Cesc ana moyo tofauti. Amewahi kutamka kwamba yeye anaweza kuchezea klabu mbili tu duniani, Arsenal na Barcelona.

Inachekesha kwamba Man UTD wanamhitaji Fabregas. Mwenyewe amesema anataka kubaki Barcelona. Japo anajua kwamba yeye siyo muhimu sana Barca, lakini anaona aibu kuondoka.
Amezoea kuongoza, amezoea kushinda na hataki kukubali kwamba ameshindwa kuyafanya aliyoyafanya akiwa Arsenal.
Ameshatwaa mataji sasa, lakini hana uhakika wa namba. Hata Thiago tu alikua ni tishio kwake na japo ameondoka lakini bado Cesc hayupo salama.

Binafsi nahisi hakuna mahali pazuri kwa Fabregas kucheza, akaheshimiwa na kupendwa kama Arsenal. Lakini ukweli mwingine unaouma ni kwamba Arsene Wenger hamuhitaji kwa sasa.
Wenger anatamani kuona Cesc anauzwa kwingine kwa sababu nusu ya Ada yake ya uhamisho itakwenda Arsenal.
Mashabiki wanamtamani nahodha wao arudi na ni rahisi Arsenal kumpata hata kwa £15 wakimtaka. Hiyo inatokana na mkataba wake wa mauzo kwenda Barcelona ambao unaipa Arsenal haki nyingi kumhusu Fabregas.

Lakini ukweli unaouma zaidi ni kwamba hakuna tena pengo lake. Arsenal walihangaika sana kuliziba kupitia Mikel Arteta lakini sasa hivi yupo Jack Wilshere na Aron Ramsey.
Kuanza kukomaa kwa kijana mjerumani Thomas Eisfeld ambaye amefanana na Cesc kwa kila kitu, kunawapa wajeuri wa Arsenal kiburi zaidi.
Kama Cesc anataka kutawala safu ya kiungo ya dunia kama zamani anahitaji timu nyingine. Timu itakayoundwa kupitia yeye na siyo Messi wala Neymar.
Lakini ukweli unaouma zaidi ni kwamba Barcelona hawaoni faida kumuuza. Waliishasaini mkataba mbovu na Arsenal ambao unaipa Arsenal haki nyingi iwapo Cesc atauzwa Popote.

Kingine Kinachouma ni kwamba Fabregas siyo tu hapendi kuondoka Hispania bali haipendi Man UTD. Siyo timu atakayofurahia kuichezea.
Je nini mwisho wake? Nasubiri kuona lakini namwombea nahodha wangu huyu mwisho mzuri.

Imeandikwa na Richard Leonce ChardBoy kutoka WapendaSoka Group.
Nipate katika chardboy74@gmail.com, wapendasoka@gmail.com, @chardboy77 kwenye twitter na0766399341.
Usisahau kulike page ya Wapendasoka-Kandanda kwenye Facebook.

No comments

Powered by Blogger.