THE GUNNING MACHINE ~ FABREGAS HAPANA!! ARSENAL INAHITAJI NINI?
Kama nilivyowaambia wasomaji wangu wiki mbili zilizopita kwamba usajili wa Arsenal utatawaliwa na utata mara zote. Utata huo hutokana na vyombo vya habari pamoja na uhitaji wenyewe wa mashabiki wa Arsenal.
Waandishi wanajua kwamba mashabiki wa Arsenal wana hamu ya kusikia habari kuhusu usajili.
Arsenal imehusishwa na wachezaji wengi msimu huu wa usajili, kwa kila nafasi. Kuna ushabiki wa vyombo vya habari katika hili lakini leo nataka kwa upeo wangu niangalie Arsenal inahitaji nini hasa.
Nianzie mbele kwenye nafasi ya ushambuliaji ambako ndipo tunakotegemea ushindi utoke.
Theo Walcott ambaye kimsingi ni winga, ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji wa Arsenal wa msimu uliopita akifunga jumla ya mabao 21 na pasi za mwisho 14.
Olivier Giroud ambaye ndiye mshambuliaji namba moja akafunga magoli 17 na pasi za mwisho 11.
Cazorla alifunga mara 12 na pasi za mwisho 13. Kwa takwimu hizi utaona kwamba Cazorla, Podolski na Walcott walifanya kazi yao ipasavyo. Wamevuna mabao ya kutosha kwa nafasi zao, lakini bado Olivier Giroud hajaridhisha.
Pengine ni kutokana na kuwa peke yake kwa muda mrefu katika nafasi hiyo.
Robin Van Persie alifunga mabao 30 katika msimu wa 2011-12 lakini bado hakuipa Arsenal ubingwa. Unajua kwa nini?
Wachezaji wengine hawakufunga mabao ya kutosha, kazi ya ufungaji walimwachia RVP pekee ambaye pamoja na kufunga mabao mengi, bado hayakutosha kuipa Arsenal ubingwa wowote.
Lakini msimu uliopita mabao yamepatikana na kwa wachezaji wengi tofauti tofauti lakini tofauti yake ni kwamba mshambuliaji namba moja hakufunga mabao ya kutosha.
Nashangaa kwamba Arsenal wanaendelea kuwakosa washambuliaji wanaowanyatia ambao wangeweza kufuta tatizo hilo.
Sidhani kama Benik Afobe na Yaya Sanogo wataweza kuleta tofauti kwa msimu ujao. Iko wazi kabisa, Arsenal wanahitaji mshambuliaji.
Katika nafasi za viungo, hakuna matatizo sana.
Lucas Podolski na Gervinho kama wakiwa fit, wanaimudu nafasi ya kiungo cha kushoto.
Alex-Oxlade Chamberlain na Theo Walcott wanaimudu vizuri sana nafasi ya kiungo cha kulia.
Usimsahau pia kijana wa kijerumani Serge Gnabry anayekuja vizuri. Ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji na winga wa kulia. Lakini pia yupo Ryo Miyaichi.
Katika nafasi ya viungo wa katikati, Arsenal haina tatizo kubwa.
Tatizo ni mifupa ya Jack Wilshere. Lakini kama atakuwa fit kwa msimu mzima, ukiwaongeza Thomas Rosicky na Aron Ramsey, ukipenda utamwongeza Abou Diaby pia. Utakubaliana nami kwamba hakuna hitaji la Cesc Fabregas.
Kumbuka Gidion Zelalem na Thomas Eisfield wanawania nafasi hiyo na kwa macho yangu, mmoja wao atapata nafasi msimu ujao. Litakuwa ni jambo zuri sana kwa klabu.
Nafasi inayonipa shida ni kwenye kiungo wa ulinzi. Mikel Arteta aliimuda msimu uliopita na pengine atakabidhiwa tena msimu ujao lakini umri wake nao unakwenda. Lakini pia endapo atapata majeraha, Emmanuel Frimpong anaweza kuhitajika kuziba nafasi yake. Bado sina imani sana na kiungo huyu mwenye asili ya Ghana.
Nadhani nikiri kwamba mtu kama Lars Bender wa Bayern Liverkusen au Maroane Fellaini wa Everton wanaweza kuwa sahihi kwa nafasi hiyo japo sina uhakika kama tutampata yeyote kati yao.
Katika nafasi ya ulinzi, nadhani mabeki hawatoshi. Per Martesacke, Laurent Koscielny na Thomas Varmaelen ndiyo mabeki wa kati pekee wa kiwango cha kuchezea Arsenal. Msimu una mechi nyingi na kuna majeraha pia.
Mtu kama Ignasi Miquel huwezi kumtegemea sana japo anacheza vizuri lakini hana uzoefu, huwezi kumpa mechi ngumu. Kwa hali hiyo nakiri Arsenal wanamhitaji Ashley Williams wa Swansea.
Kwa mabeki wa pembeni sina uhakika sana na kiwango cha Bacary Sagna, lakini kama hatouzwa, basi uzoefu wake utaisaidia sana Arsenal akishirikiana na Carl Jenkinson.
Golikipa Vito Manone amejiunga na Sunderland, nakumbuka alijitahidi sana mwanzoni mwa msimu uliopita wakati Lucas Fabianski na Wojciech Szczesny ni majeruhi.
Najiuliza kama hali hiyo ikijitokeza tena, tutakuwa tayari kumkabidhi lango Damian Martinez kwa sasa?
Tukutane wiki ijayo wapendwa.
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka(kandanda) Group katika Facebook.
Nipate katika chardboy74@gmail.com au @chardboy77 kwenye twitter na 0766399341
No comments