THE GUNNING MACHINE ~ SIR. ALEX FERGUSON vs ARSENAL

                

                      NI VITA YA MIONGO MITATU.
Vieira na Seaman
 
"Sijawahi kushuhudia mtu yeyote akiwa katika kilele cha mafanikio ya soka kwa kipindi kirefu kiasi hiki. Kwa upande fulani inatia shaka ukijiuliza pindi mtu huyu atakapoondoka klabuni, haijalishi ubora wa atakayekuja badala yake lakini ni lazima ataacha shimo kubwa.



Klabu itahitaji mageuzi kwa sababu alama yoyote na maisha yoyote pale Old Traford yanamzunguka Alex Ferguson"
Hayo ni maneno ambayo yalitamkwa na Arsene Wenger miaka miwili iliyopita wakati akimzungumzia hasimu wake huyo mkubwa kwenye soka.
Mtu huyo aliyeutendea makubwa mpira ametangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu. Hakuna jinsi ambavyo THE GUNNING MACHINE inaweza kukwepa kumuenzi mzee huyo.
Kwa miaka yote 27 akiwaongoza Manchester United kuwa wapinzani wakubwa wa Arsenal kuliko hata Tottenham Hotspurs ambao upinzani wao si wa kutisha sana.
Basi leo kwa heshima kubwa, THE GUNNING MACHINE inakuletea baadhi ya matukio makubwa yaliyotokea kipindi cha Man UTD chini ya Ferguson dhidi ya Arsenal ambayo siyo ya kusahau.

VITA YA KWANZA YA OLD TRAFORD-1990.

 
Oktoba 1990, Ulipigwa mpambano kati ya Man Utd na Arsenal ambao unatajwa kuwa na vurugu kuliko mapambano yote yaliyozikutanisha timu hizo.
Ilikuwa ni katika mfumo wa zamani wa uendeshaji wa soka nchini England na soka kwa kipindi hicho lilikua ni mchezo wa kibabe, hawa akina Isco, Gervinho na Neymar wangekaa nje kuokota mipira.
Basi tatizo lilianza wakati mpira ukimilikiwa na Denis Irwin wa Man United wakati huo timu zilikua hazijafungana.
Akatokea beki mmoja mgumu sana wa Arsenal wakati huo, anaitwa Nigel Winterburn akamwekea Irwin "munda" au wengine wanaita "kumpa mwili" kwa nguvu hadi akaenda chini kisha Winterburn akaondoka na mpira.
 
 
 
Unadhani Irwin alikubali?
 
Kilichotokea ni Nigel Winterburn kupokea mabuti kutoka kwa wachezaji wote wa Man United kisha vita ikasambaa na kuwahusisha wachezaji wa timu zote mbili. Wote wakaanza kushushiana makonde kasoro golikipa wa Arsenal David Seaman pekee aliyeamua kujiweka kando.
 
Arsenal walishinda mchezo huo kwa bao 0-1 lililofungwa na Anders Limpar ingawa kutokana na vurugu zilizofanywa na wachezaji, timu zote zilipokonywa pointi.
Arsenal chini ya kocha George Graham walipokonywa pointi 2 na Man Utd chini ya Fergie wakapokonywa pointi 1.
Kwa jinsi mchezo ulivyokuwa, ukapachikwa jina na kuitwa Vita Ya Kwanza Ya Old Traford.

                ARSENAL 3-2 MAN UNITED :1997.

 
Hii inaweza kuwa ni moja kati ya mechi zilizomo ndani ya kumbukumbu za Sir Alex Ferguson. Siyo mechi ya kukutoka kirahisi rahisi tu.
Ilikuwa ni katika msimu wa kwanza kwa kocha Arsene Wenger kuiongoza Arsenal kwa msimu kamili.
 
Nakumbuka dakika ya 7 tu ya mchezo huu wa ligi kuu, Nicolas Anelka aliuwahi mpira uliokuwa unaambaa ambaa baada ya shuti kali la Marc Overmas kupanguliwa na mabeki wa Man United. Akamwangalia Peter Schmeichel amekaaje, akauweka kambani.
Kiungo mgumu, mweusi, Patrick Vieira akamtesa tena Schmeichel kwa shuti kali dakika ya 20 na kufanya mabao kuwa 2-0. Arsenal wakaonekana kama wamewalaza mapema Man United. Wakaanza kutandaza lile soka lao kama ulivyo utamaduni.
 
Lakini ndani ya dakika 10 za mwisho, Tedy Sheringham akasawazisha magoli yote mawili kiajabu ajabu tu.
Basi kipindi cha pili kikawa cha piga nikupige. Likapigwa soka ambalo unaona kabisa kwamba hapa hakuna sare, lakini hujui nani anafungwa. Kipindi hicho kuna watu wa nguvu kama akina Ray Parlour, Ian Wright na Steve Bould. Denis Bergkamp hakucheza mchezo huo kutokana na majeruhi.
Zikisalia dakika 7 tu mpira kumalizika. Arsenal wakapata kona iliyopigwa kutoka magharibi ya uwanja. Ilipigwa kona ya shuti kali, ikakutana na kiungo David Platt nae bila ajizi akautandika bila huruma na kuutia kimiani.
 
Wachezaji wa Arsenal walitumia zaidi ya dakika nzima kushangilia bao hilo.
Dakika zilizosalia zilishuhudia mpira wa kasi na nguvu kwa timu zote, lakini ni Arsenal ndio walionekana kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.
Basi hadi mwisho wa mchezo huo, Fergie na Man United yake wakawa wamelala kwa mabao 3-2 katika mchezo mkali sana. Na labda kwa kumalizia tu sehemu hii ya kwanza, nikumegee siri yangu mimi Chardboy kwamba tangu mechi hii ilipochezwa, ndipo nilipoanza kulilia kuangalia mechi za ligi kuu ya England na hasa Arsenal, japo sikua shabiki wake moja kwa moja.
 
Mtu wangu, huu ni mwanzo tu, unataka kujua Vita ya Pili ya Old Traford Ilikuwaje?
Hivi unajua Fergie ametibua rekodi ngapi za Arsenal?
Ilikuwaje Sir akatupiwa Pizza nyumbani kwake Old Traford?
Wenger aliwahi kumfananisha Van Nistelrooy na mke wa mtu, unataka kujua ilikuwa vipi?
Pale Fergie alipoambiwa amzungumzie Wenger mwaka 2002, unajua alisema nini.
Wiki ijayo hapa hapa...
Imeandaliwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka (Kandanda) group.
 
Napatikana sasa katika wapendasoka@gmail.com, chardboy77@yahoo.com na @chardboy77 kwenye twitter. Au 0766399341.

No comments

Powered by Blogger.