THE GUNNING MACHINE

MECHI ZILIZOBAKI NI KUFA AU KUPONA KWA ARSENAL ILA SILAHA ZIKO TAYARI
 
SILAHA ZA MAANGAMIZI
 
Ligi kuu ya England kwa Arsenal hivi sasa imefikia hatua ambayo siyo tu inawapa shida wachezaji na benchi la ufundi la Arsenal. Bali inawapa wakati mgumu sana mashabiki wa Arsenal kote ulimwenguni.
Poleni sana mashabiki wenzangu wa Arsenal. Hata mimi kama kama shabiki na mpenzi wa kweli wa Arsenal sina raha kabisa, ukizingatia kuwa kwa kazi yangu kila siku nalazimika kufungua mitandao mbalimbali ili kujua kinachoendelea kwenye Ulimwengu wa Michezo.
Tunalazimika kupiga hesabu ngumu za angalau kubaki kwenye Timu nne Bora (Top 4) ambazo hufanikiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya michuano yenye heshima na pesa nyingi ikiwa imesalia michezo mitano.
 
Ukitaka kujua hesabu zetu ni ngumu kiasi gani, ikumbuke mechi dhidi ya Norwich wiki iliyopita. Tulishinda tu kwa kutumia utu uzima lakini jahazi lilikua linakaribia kuzama na hapo ndipo tunapoamini kama Ligi ya England ni bora na ni ngumu hasa katika mechi za mwisho wa msimu.
Mchezo dhidi ya Everton katikati ya wiki ulikua mgumu lakini muhimu kupata pointi tatu. Shukrani hata kwa pointi moja tuliyoambulia lakini bado naamini mechi ile kwa upande wetu ilikosa mtu wa kuamua kushinda baada ya kukosa nafasi za wazi na hapo ndipo nawakumbuka sana Thierry Henry na Robin Van Perse.
 
 
Sitaki kuumulika mwezi Mei sasa hivi lakini nashawishika kuamini kua michezo dhidi ya Wigan pamoja na ule wa dhidi ya QPR itakua migumu sana kutokana na ukweli kwamba hao wote wanawania nafasi ya kubaki katika ligi kuu, labda tuombe wawe wamekwisha jihakikishia kushuka daraja tutakapokutana nao.
Tunacheza na Fulham Jumamosi hii, Timu ambayo ilikubali kichapo kutoka kwa Chelsea katika mchezo wa katikati ya wiki. Vipi kama wakiamua kuibishia Arsenal ili wapate angalau pointi moja? Kumbuka hawana cha kupoteza kwenye msimu kwa sasa.
Mchezo dhidi ya Manchester United tutauzungumzia wiki ijayo kwa kirefu, lakini nikukumbushe kuwa kwa siku za hivi karibuni Mashetani Wekundu wamekua kama ndoto ya kutisha kwa Arsenal.
Kinachotia doa maombi yetu ni kuwa kama matokeo yakienda kama tunavyotaka,basi ni lazima tuhakikishe tunamfunga Man UTD tarehe 28, vinginevyo wanaweza kutangaza ubingwa nyumbani kwetu tena wakiwa na Robin Van Persie hii itakua Aibu sana kwa kikosi cha Arsenal na mashabiki wake wote hapa duniani.
 
Ni kweli, sisi tutapenda kuona Man City anampiga Spurs jumapili ili tupate nafasi ya kumpita. Hali ikiwa hivyo na Manchester UTD akampiga Aston Villa, basi Man UTD watataka kushinda mchezo dhidi yetu ili watangaze ubingwa. Watakua wametupaka haja kubwa mitaani.
Hapa ndipo ninaposhindwa kumlaumu ndugu yangu Tuga Arsenal (Mnazi mkubwa wa ganazi) anapochafua hali ya hewa kwenye group la wapenda soka katika mtandao wa facebook.
 
Huu ni wakati ambapo sisi kama mashabiki, hatuna la kufanya, tuwaachie wachezaji, kocha na Mungu ili wafanye linalowezekana. Kushinda michezo yote iliyosalia ili tupate nafasa ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini pia kuwazuia Manchester United kujisaidia haja kubwa nyumbani kwetu.
 
 
               TUANGALIE KIKOSI CHETU.
Jack Wilshere alirejea katika michezo dhidi ya Norwich na Everton, kiwango chake bado sioni kama kinatusaidia kwa sasa ambapo timu ni muhimu kuliko mchezaji.
Muungano wake na Santiago Cazorla ilikuwa ngumu sana katika michezo hiyo, lakini naamini itakuwa ni kwa muda tu hali itarejea lakini swali ni kwamba tuna huo muda kwa sasa?
Nafarijika na kupenda mchango wa Aaron Ramsey wakati huu ambapo Wilshere na Rosicky hawapo fit kwa asilimia 100.
Ramsey ametumika kama kiraka kwa muda mrefu na tunapaswa kumpa hongera zake, lakini hatimaye sasa anaonekana kutulia zaidi kwenye nafasi yake akicheza kama kiungo mshambuliaji.
Kwa mbali napata picha ya Gilberto nikimtazama Mikel Arteta kwenye kiungo cha ulinzi. Anakaa vyema  na kufanya kazi yake kama bosi mbele ya mabeki wanne.
Kuhusu Oliver Giroud, nadhani huu ndiyo ungekua wakati wake wa kukaa benchi ili aanze kupigania nafasi yake. Lakini kwa bahati mbaya, hakuna mshambuliaji mbadala wa kumwachia nafasi.
Kwa macho yangu, huwa naona Podolski ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji, lakini ni kwa macho yangu mimi Rich na siyo macho ya Wenger.
THE GUNNING MACHINE kwa wiki hii haina mengi, tukutane tena wiki ijayo ambapo tutauzungumzia mchezo dhidi ya Manchester United lakini pia tutafunga mwezi Aprili na kuumulika mwezi Mei kama kawaida.
>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>.
 
Imeandaliwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka Kandanda group katika ukurasa wa facebook
 
Nipate katika chardboy77@yahoo.com na @chardboy77 kwenye twitter au 0766399341

3 comments:

Powered by Blogger.