THE GUNNING MACHINE

HURUMA YANGU KWA ANDREY ARSHAVIN.
 
Thomas Rosicky alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Jamhuri Ya Czech sawa na Andrey Arshavin wa Urusi katika michuano ya Euro 2012.
Wiki iliyopita baada ya Rosicky kupiga bao mbili katika ushindi mgumu wa Arsenal dhidi ya W.B.A, blogers wengi waliandika kuhusu ufundi wa Rosicky midfield ya Arsenal. Lakini tofauti na wao, mimi nilimkumbuka Andrey Arshavin kisha nikasikitika sana.
Nikakumbuka siku chache zilizopita nilikua nimesoma gazeti moja la kimataifa likiripoti kwamba Arshavin atastaafu soka mwishoni mwa msimu.
Sijui kama ni kweli ama ni uzushi,lakini hata kama ni uzushi, kinachonisikitisha ni ukweli kwamba tendo hilo (la kustaafu kwa Ashavin) halipo mbali na sasa. Litatokea miaka michache ijayo.
Mchezaji aliyekuja kwa ada ya uhamisho ya £13M. Tena nakumbuka ilikua ni siku ya mwisho ya usajili. Tuliuchukulia usajili wake kama ushindi, kwa sababu Arsene Wenger alimuwania kwa kipindi kirefu.
 
Leo thamani, kiwango na umuhimu wa Arshavin umeyeyuka kama theruji juani. Ameanza katika michezo miwili tu msimu huu.
Nakumbuka msimu uliopita wakati Arsenal wanatafuta tiketi ya kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya, tena wakiwa nyuma Tottenham HotSpurs (hakuna kitu Arsenal wa ukweli wanachukia kama kuwa nyuma ya Spurs) Benchi la ufundi la Arsenal bado lilikubali kumtoa Arshavin kwa mkopo kwenda Zenit St Petersbrough na kampeni ya kupata tiketi ya Ligi ya Mabingwa ikafanikiwa.
Kwa maneno mengine ni kwamba Arshavin hakuwa muhimu kwa kampeni ile.
Msimu huu mechi yake ya mwisho ni ya mwezi Januari dhidi ya Chelsea akiingia zikiwa zimesalia dakika 15 mchezo kumalizika. Na wakati anaingia, kwenye benchi aliwaacha Emmanuel Frimpong, Golikipa na mabeki wanne.
Pengine angekuwepo mchezaji wa nafasi yake, Arshavin asingecheza.
Kuna wakati namwona kwenye picha za mazoezi pale London Colney akicheka kwa furaha na wenzake ingawa sidhani kama nafsini mwake ana furaha na hali halisi ya kiwango chake.
Niliwahi kumwona Francis Coquelin akisema kwamba Arshavin ndiye mchezaji mwenye juhudi sana mazoezini na hajawahi kumwona akikosea au kumpa shida mwalimu.
Kulikua na nafasi kwake ya kwenda Reading kwa mkopo mwezi Januari mwaka huu lakini alikataa kwa madai kuwa bado anadhani ana nafasi ya kuichezea Arsenal.
Kuna lawama kwa Arsene Wenger kwamba ndiye aliyemharibu Arshavin. Mimi huwa napinga kabisa suala hilo.
Nakumbuka kipindi fulani Wenger aliwahi kumtumia kama mshambuliaji wa mwisho, lakini ilikua ni kwa kipindi kifupi tu ambacho Eduardo na Bendtner walikuwa majeruhi. Sisemi alikuwa wapi Robin Van Persie kwa sababu najua wajua.
Tofauti na hapo, Wenger amekuwa akimtumia kama mshambuliaji anayetokea kushoto (winga)
kumbuka tangu Arsenal waanze kutumia mfumo wa 4:3:3 mawinga wote wamegeuka washambuliaji na Arshavin alisajiliwa ili kukamilisha mfumo huo.
Kumbuka timu aliyotoka ya Zenit ilikua ikitumia mfumo huo kabla ya Arsenal.
Lakini ukisema Wenger amemharibu Arshavin, utasema nini kwa Mikel Arteta?
Utasema nini kwa Aaron Ramsey ambaye mashabiki huwa wanajua kumlaumu tu, wanajisahaulisha kwamba kwa msimu huu pekee, Ramsey ameishatumika winga wa kulia,
kushoto, kiungo mkabaji (wakati Arteta ni majeruhi),kiungo mshambuliaji (ambayo ndiyo hasa nafasi yake) na beki wa kulia (wakati Sagna ni majeruhi na Jenkinson anatumikia kadi nyekundu).
Mashabiki hawaoni hilo.
 
Wanasema Arshavin hakuzoea kufanya kazi ngumu ya kupanda na kushuka kufuata mipira na kushambulia. Lakini mimi nakumbuka mechi moja misimu kadhaa iliyopita dhidi ya Middlesbrough nafikiri, Arshavin alicheza mbele ya Kieran Gibbs. Wakati huo Gibbs alikua kama Jernade Meade wa Arsenal U19 hivyo Arshavin akawa analazimika kumfanyia back up ya kutosha. Lakini Arshavin alionekana kuifurahia sana kazi hiyo na alikua akicheka muda wote.
Ni nini kimemsibu Arshavin?
 
Unajua sasa hivi akina Dan Chibo na Bebeng Sterling hawamwogopi tena?
Ni kweli kwa sababu hana tena uwezo wa kuwafunga magoli manne nyumbani kwao Anfield kama alivyofanya wakati anawasili Arsenal.
 
 
Hisia zangu ambazo sina uhakika kama zipo sahihi ni kwamba kinachommaliza Arshavin ni kule kuujua mpira sana.
Unaweza kubisha, lakini ukweli ni kwamba baadhi ya wachezaji waliochezea sana mpira tangu utotoni huwa wanaudharau na kudhani wanaweza kuufanya lolote.
Mkumbuke Carlos Vela kwa mfano. Ni aina ya wachezaji ambao wameudharau mpira, nao ukawatupa kama Arshavin ingawa wanaujua.
Ni tatizo ambalo linaelekea kuwakuta akina Daniel Sturidge, Ashley Young na Joe Cole.
Unamkumbuka Ray Parlour?
 
Sidhani kama anajua kupiga danadana, lakini aliweza kucheza katikati ya akina Bergkamp, Overmas, Pires, Henry na Vieira na kuwafanya wammiss asipokuwepo. Unajua kwa nini?
Alijua kwamba yeye hana kipaji cha kuchezea mpira kama Arshavin, hivyo akawa anatimiza kile tu anachotaka mwalimu, basi.
Kwa maoni yangu, hilo ndilo tatizo la Arshavin. Anaamini anaujua sana mpira na kweli anaujua lakini ameshindwa kuutendea haki. Kuujua mpira na kuutendea haki ni vitu viwili tofauti.



................Richard Leonce Chardboy (Wapenda Soka (kandanda) group on Facebook)

2 comments:

Powered by Blogger.