THE GUNNING MACHINE ~ MUHIMU NI USHINDI, 'GUARD OF HONOUR' NI YA MAN UNITED.


Arsenal
 
Kuna historia itaandikwa katika mchezo dhidi ya Manchester United siku ya  jumapili kwenye uwanja wa Emirates nyumbani kwa Arsenal.
Meneja wetu Arsene Wenger amethibitisha kwamba Arsenal watatoa gwaride la  heshima maarufu kama  "Guard Of Honour" kwa mabingwa wapya wa ligi kuu ya England kama ilivyo utamaduni wa Ligi kuu na ligi mbalimbali barani Ulaya ikiwemo La Liga.
 

 
 
Rasmi sasa kutoka THE GUNNING MACHINE, tunawapongeza mashabiki wote wa Man UNITED kwa ubingwa ambao wameupata kwa kustahili kabisa. Ndivyo soka ilivyo ukubali ukatae.
Mara nyingine ni kama mchezo wa kupokezana vijiti na ni uungwana kumpongeza mwenzio na kumpa heshima anayostahili.
Najua itauma mioyo ya wana Arsenal wote ulimwenguni watakaposhuhudia wachezaji wa Man United wakifanywa wafalme nyumbani kwetu, lakini kama shabiki mkomavu wa soka, hivyo ni vitu vya kawaida kabisa na hata sisi tuliwahi kupitia nyakati nzuri kama hizo.
Kitu muhimu kwetu ni pointi katika mchezo huo, siyo Gwaride la heshima (Guard of Honour) kama wenzetu Man UTD.
Tunahitaji pointi 3 kuliko Man United wanavyozihitaji na hii inatokana na ushindani ulioko katika kuwania nafasi nne za juu. Suala la kumzomea Robin Van Persie ambaye kimsingi ni bingwa, ni sawa na kupoteza muda.
UGUMU WA MCHEZO DHIDI YA MAN UNITED.
 



Man United wameshinda michezo 12 ya ugenini msimu huu, hakuna timu iliyofanya hivyo na hii Inawapa Nafasi nzuri ya kuamini  kuwa wana nafasi nzuri ya kushinda mchezo huo kwa rekodi hiyo.
Lakini kuna mtu anajiita Messi Msangi Chicharito (shabiki mkubwa wa Man United kwenye group la wapenda soka (kandanda)) aliwahi kusema  "Records are for books".
 
Kwa Upande wa Arsenal pia wapo vizuri hivi sasa, wamefungwa mchezo mmoja tu katika michezo 14 iliyopita. Hii inatoa picha halisi jinsi gani mchezo huu utakua mgumu.
Safu ya ulinzi ya Arsenal ambayo kama unakumbuka vizuri ndiyo iliyovuja na kuwapa Man United ushindi katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Old Traford katika mzunguko wa kwanza, imekomaa hivi sasa.
Haina Andre Santos, na hata nahodha Thomas Varmaelen anasubiri kwenye benchi. Laurent Koscienly na Per Martesacker wanaonekana kufanya vizuri kwenye ulinzi wakiwa nyuma ya Mikel Arteta wakati Nacho Monreal na Kieran Gibbs wanachuana kuwania nafasi katika beki ya kushoto.



Kikosi kipo vizuri, lakini napata wasiwasi kila Arsenal wanapokutana na Man United kwa siku za karibuni huwa wanafungwa kabla ya kuanza mchezo.
Wachezaji wa Arsenal huwa wanaonekana wanyonge sana mbele ya Man United hili linanipa tabu kufahamu ni kwa nini.
Mashabiki wa Arsenal wamekumbwa na jinamizi la kutopenda kuambiwa ukweli kuhusu timu yao, hivyo nachelea kusema wanaiogopa Man United. Lakini huo ndiyo ukweli  Arsenal siyo tena wapinzani wanaotisha kwa Man United.
Hakuna timu ambayo imeinyanyasa Arsenal kama United kwa miaka ya hivi karibuni na hilo ndilo huwafanya hata wachezaji kupatwa na ganzi kila wakutanapo na mashetani wekundu kutoka jiji la Manchester.

HALI ILIVYO KIKOSINI ARSENAL.

Stori kubwa ni nafasi ya Olivier Giroud ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu na rufaa yake imegonga mwamba.
 
Kuna watu watatu ambao wanaweza kucheza kama washambuliaji, nao ni Theo Walcott, Gervinho na Lucas Podolski.
Natamani kikosi kitakachoanza kiwe na Podolski na Walcott. Hawa ndiyo watu wanaoweza kufanya lolote kwa muda wowote ndani ya kikosi cha Arsenal kwa sasa.
 
Sitakuwa na imani nikimwona Gervinho anacheza namba 10, lakini tumwachie kocha kazi yake.
Jack Wilshere siyo mtu muhimu sana kwa sasa, Arsenal wameweza kushinda michezo muhimu bila Wilshere kuwepo. Mfumo wanaotumia Arsenal unamruhusu mtu yeyote kuongoza mashambulizi na sasa hivi timu ni muhimu kuliko mchezaji.



Nawatakia mashabiki wote wa Arsenal mchezo mzuri na nadhani tunaweza kushinda mchezo huo.
 
Tukutane ... Kinondoni Uhuru Peak (Opposite na Mango Garden). Nitakuwepo hapo na wadau wengine kutoka Wapenda Soka(kandanda) Group kucheki mechi hiyo
Imeandaliwa na Richard Leonce ChardBoy kutoka Wapenda Soka (Kandanda) Group katika ukurasa wa facebook.
Napatikana sasa kupitia wapendasoka@gmail.com, chardboy77@yahoo.com na @chardboy77 kwenye twitter.

1 comment:

Powered by Blogger.