THE GUNNING MACHINE

UNATAKA WENGER AONDOKE? BASI MWOMBEE KIFO.
                   "Arsene Wenger afukuzwa Arsenal"

Arsene Wenger

Akili yangu inaniambia ni rahisi mtu kufufuka kuliko kuchapishwa kwa kichwa cha habari kama hiki kikimaanisha ukweli.
Jumamosi ya Februari 16, tulishuhudia Arsenal ikiondolewa kwenye kombe la FA na timu ya Blackburn Rovers.  Blackburn Rovers hivi sasa ni timu ya ligi daraja la kwanza pale England baada ya kushuka daraja msimu uliopita.
 
 
Hasira za mashabiki wa Arsenal zikaelekea moja kwa moja kwa kocha Arsene Wenger wakimtuhumu kuwa alipanga kikosi dhaifu katika mchezo huo ili kupumzisha wachezaji wake kwa ajili ya mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Bayern Munich.
Bahati mbaya Arsenal wakapoteza michezo yote miwili, yani ule wa kombe la FA na ule wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich laiti kama wangeshinda kila mtu angemwona Wenger shujaa.
 
 
Kombe la Klabu bingwa Ulaya haliwaumi mashabiki wa Arsenal kwa sababu wanajua kuwa hawawezi kuchukua. Hata dunia igeuke leo na Arsenal amfunge Bayern 0-5 pale Alians Arena, March 13, 2013 bado Arsenal hawatachukua kombe la ligi ya mabingwa msimu huu.
Kinachowauma mashabiki wa Arsenal ni kupoteza nafasi ya kutwaa kombe la FA. Unajua kwa nini?
Kwa sababu unaweza kucheza fainali ya FA bila kukutana na Man UTD, Man City au Chelsea. Lakini huwezi kutwaa kombe la Klabu bingwa Ulaya bila kukutana na sura za kutisha kama za akina Messi, Rooney, Ribery, Ronaldo,Robin Van Perse, Lewandowski nk.
 
 
Wakati mashabiki wa Arsenal wakimtaka Arsene Wenger aondoke, kuna tetezi kuwa kocha huyo yupo kwenye mipango ya kusaini mkataba mpya utakaomweka Arsenal kwa muda mrefu zaidi.
Yeye mwenyewe amekanusha hilo lakini kwani aliwahi kukanusha mangapi?
Siyo Wenger aliyesema hawezi kumuuza Robin Van Persie kwa ada ya chini ya £40m?
Basi usishangae ukigundua kuna ukweli kwenye tetesi hizi.
Ukiniuliza mimi kuhusu Arsene Wenger nitaungana na akina Jack Wilshere na Thomas Varmaelen.
"Wenger ndiye mtu sahihi wa kuifundisha Arsenal"
Tatizo kubwa la Arsene Wenger ni kwamba hana presha nyuma yake. Presha ya kumfanya awe na chaguo moja tu katika mechi ambalo ni USHINDI.
Roberto Manchini, Alex Ferguson na Jose Mourinho wana bahati ya kupata presha hii.
Katika kila mechi iliyopo mbele ya Man UTD, akili ya Ferguson huwa inawaza ushindi tu, tena hasa hasa ikichezwa katika uwanja wa nyumbani.
Hali hii haipo Arsenal. Kama ulitazama mechi ya Februari 19 kati ya Arsenal na Bayern Munich utakubaliana na mimi kwamba hakuna mechi msimu huu ambayo Arsenal walicheza kwa kujituma na kujitolea kama mechi hiyo. Walifungwa kwa sababu Bayern ni bora kuliko wao lakini wachezaji walitoa kila walichonacho katika mchezo huo.
 
 
 
Walifanya hivyo kutokana na presha waliyoipata baada ya kuondolewa kwenye kombe la FA. Arsene Wenger alitumia dakika 40 kuwafokea wachezaji wake baada ya mchezo dhidi ya Blackburn. Wachezaji wakajiuliza, wakaamua kufanya kazi.
Kama wangecheza hivo katika mechi zote msimu huu wasingekua hapa walipo hivi sasa. Wasingefungwa na Bradford, Swansea wala Blackburn.
Arsenal wana kila kitu. Wenger ni moja kati ya Makocha wanaolipwa pesa nyingi duniani.
Ivan Gazidis ni mmoja kati ya wakurugenzi watendaji wanaolipwa pesa nyingi duniani.
Andrey Arshavin ni mmoja kati ya wachezaji wa akiba wanaolipwa pesa nyingi duniani. Lakini wanachokosa ni presha tu.
Hakuna wa kumuuliza Wenger kwamba ni kwa nini madirisha mawili ya usajili yamepita bila kusajili kiungo wa kuziba pengo dhahiri la Alex Song.
Hakuna wa kumuuliza mwenzake kwamba ni kwa nini Robin Van Persie aliuzwa wakati klabu ingeweza kutumia mishahara ya Arshavin na Squilacci (ambayo kwa ujumla ni £120,000) kumbakisha.
Hakuna wa kumuuliza mwenzake ni kwa nini watu kama Carlos Vela, Park Ju Young, Nicklas Bendtner, Johan Djourou, Denilson, Andre Santos, Joel Campbel na wengine wengi wanaendelea kuitwa wachezaji wa Arsenal wakati ukweli ni kwamba klabu haiwahitaji kwa maisha ya baadae. Kweli kuna siku Denilson atarudi kuichezea Arsenal?
Kwa maana hiyo hakuna wa kumfukuza Wenger Arsenal. Kama unadhani unataka Wenger aondoke, labda umwombee kifo. Na hiyo ndiyo sababu inayomfanya hata yeye asiwape presha wachezaji wake.
Gervinho hana hofu yoyote hata akikosa goli la wazi wala Giroud hahofii chochote kupaisha mpira dalika ya 90.
 
>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>><<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<
 
 
Imeandikwa na Richard Leonce Chardboy kutoka Wapenda Soka Kandanda group.
Nipate katika chardboy77@yahoo.com au 06583993

2 comments:

  1. Yeah we Richard ni hatari, much respect!

    ReplyDelete
  2. Rich anatema sana cheche halafu ni kati ya mashabiki wachache wa Arsenal ambao wanajua udhaifu wa timu yao
    wengi wanafata mkumbo wa kumtaka Wenger asepe

    ReplyDelete

Powered by Blogger.